Jaji Mkuu wa Tanzania (CJ), Othman Chande (pichani) Ijumaa iliyopita alifanya ziara ya ghafla katika ofisi za Gazeti la JAMHURI zilizoko katika Jengo la Matasalamat Mansion, barabara ya Samora jijini Dar es Salaam na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Wahariri na Waandishi wa Gazeti la JAMHURI.
Jaji Mkuu Chande alipoingia chumba cha habari, alikutana na wafanyakazi na kusema: “Nilidhani mmechukua floor nzima? Hivi JAMHURI mko hapa kumbe?” alihoji Jaji Chache kwa utaratibu huku akisema kazi inayofanywa na JAMHURI mtu anaweza kudhani linaendeshwa na mamia ya waaandishi.
Aliwakuta Meneja Matangazo, Manyilizu Maghembe na Msanifu Kurasa, Lucas Gordon wakatambulishwa, kabla ya kuingia ofisi ya Mhariri Mtendaji na Naibu wake, Deodatus Balile na Manyerere Jackton.
Akiwa na viongozi hao, Jaji Mkuu aliwakuta wakiandaa habari ikiwamo kusoma mkataba wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL Group) ambapo walimwonyesha baadhi ya vifungu vinavyotumiwa na mwekezaji wa SABmiller kukwepa kodi, akaishia kutikisa kichwa.
Baada ya utambulisho mfupi, Mhariri Mtendaji Balile alimweleza kwa kifupi Jaji Mkuu Chande namna JAMHURI linavyofanya kazi jambo ambalo alisifu kuwa kazi inayofanyika ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wafanyakazi.
Akizungumza kuhusu JAMHURI, Jaji Mkuu Chande alisema: “Hakika mnafanya kazi kubwa. Hongereni, keep it up. Nimefarijika. Sikudhani kama mko hapa. Nilijua mna ofisi kubwa. Labda mko wengi. Safi sana, endeleeni. Kwa sababu mnafanya kazi kubwa. Ahsante sana.”
Kadhalika alisifu namna baadhi ya wafanyakazi walivyojitoa kujiendelea kielimu katika fani mbalimbali hasa Mhariri Mtendaji Deodatus Balile ambaye amesomea pia Shahada ya Sheria na kuwapa moyo Alfred Lucas anayefanya kozi ya Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam na Manyerere anayesoma Shahada ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu Huria (OUT).
“Someni. Nimegundua siri yenu. Nimejua sababu ya kufanya vema. Basi leo mimi yangu yalikuwa hayo tu, nilitaka kupita kuwasalimia tu, safi sana. Endeleeni kuchapa kazi, tunawategemea,” alisema Jaji Mkuu Chande.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Gazeti la JAMHURI limesifiwa na viongozi wawili wanaoongoza mihimili ya dola.
Kabla ya Ijumaa iliyopita, Jaji Mkuu Chande anayeongoza Mhimili wa Mahakama kufanya hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alilisifu JAMHURI hadharani.
Rais Dk. Magufuli alilipongeza JAMHURI Februari 13, mwaka huu na kulitaja kama gazeti bora na mfano wa kuigwa nchini kutokana na habari zake za uchunguzi uliobobea.
Rais Magufuli alikuwa akizungumza na wazee wa Dar es Salaam ambako alilipa gazeti la JAMHURI heshima ambayo haijapata kutolewa kwa gazeti lolote tangu nchi hii ipate uhuru mwaka 1961.
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI , Deodatus Balile, alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi wakati huo alisema: “Rais Magufuli ametupa heshima ya aina yake. Tangu nchi hii ipate uhuru, haijapata kutokea Rais aliyepo madarakani akatambua kazi ya gazeti lolote kwa kulitaja hadharani. Magazeti miaka yote yamekuwa ya kulaumiwa tu na Serikali. Rais Magufuli ameweka historia mpya, nasi tunafarijika na tunamshukuru mno kwa kutambua kazi yetu.”
Balile alisema wakati wanaanzisha gazeti hilo miaka mitano iliyopita, walipanga kuanzisha chombo kitakachoandika habari za uchunguzi, kitakachokuwa na mawazo huru na kuchangia maendeleo ya taifa, hivyo wachagua kaulimbiu ya ‘Tunaanzia Wanapoishia Wengine’.