• Asisitiza kuendelea kwa zoezi la kudijiti nyaraka za Mahakama kwa urahisi wa rejea
Na Mary Grwera, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 09 Julai, 2024 amefanya ziara ya ukaguzi wa maeneo matatu ya kuhifadhi nyaraka za mashauri ambapo ameonesha kuridhishwa na mpangilio wa nyaraka hizo zilizopo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Akizungumza leo akiwa ofisini kwa Jaji Kiongozi mara baada ya kufanya ukaguzi katika maeneo hayo, Mhe. Prof. Juma ameupongeza Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kueleza kuwa ameona na kuridhishwa na mpangilio wa majalada/nyaraka kwa ujumla.
“Nimeona majalada ya kesi yapo katika mtiririko mzuri sana tofauti na nilipotembelea awali, ni muhimu kuendelea kutunza na nyaraka hizi kwa urahisi wa rejea na hata kuweka vizuri historia ya Mahakama,” amesema Jaji Mkuu.
Hata hivyo, Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Viongozi wa Mahakama kuendelea kuweka sawa nyaraka hizo katika mfumo wa nakala laini ‘soft copy’ kwa kuendelea kudijiti ili kuwa na rejea ya nyaraka hizo kabla ya kupelekwa Kituo cha Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (RAMD) kwa ajili ya hifadhi.
Kadhalika, Jaji Mkuu amewataka Viongozi wa Mahakama, kufanyika kazi kwa kuchambua na kukusanya vitabu mbalimbali ambavyo havipo katika mpangilio mzuri viwekwe vema kwa kuwa kwenye baadhi ya vitabu hivyo vingine vinaweza kuwa rejea ya kuandika historia ya Mahakama nchini.
Akitoa taarifa ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Mkuu, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amesema kuwa, mnamo mwaka 2022 kulifanyika zoezi la kuorodhesha majalada ya miaka ya nyuma kwa ajili ya kuyapeleka Dodoma kwa hifadhi.
“Majalada hayo ni ya kati ya mwaka 1930 hadi 2018, ambapo jumla ya majalada yaliyochambuliwa na kuorodheshwa yalikuwa 60,245 na yaliyopelekwa Dodoma ni 28,204. Majalada yaliyobaki yalikuwa 32,041 ambayo ni ya kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2018,” amesema Mhe. Maghimbi.
Mhe. Maghimbi amesema kwamba, kwa sasa wanasubiri zoezi la kudijiti likamilike ili waendelee na zoezi la kusafirisha majalada yote ya miaka ya nyuma hadi kufikia mwaka 2023 kwenda Dodoma kwa ajili ya hifadhi.
Akielezea kuhusu utunzaji wa kumbukumbu (data base), Jaji Mfawidhi huyo amesema kutokana na wingi wa mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama hiyo, walitengeneza ‘database’ iliyorahisisha kupatikana kwa majalada.
Ameongeza kwamba, utunzaji wa kumbukumbu (database) uliotengenezwa uliandaliwa katika maeneo matatu ambayo ni Mashauri ya Madai, Mashauri ya Ardhi na Mashauri ya Jinai na kwamba ‘database’ hiyo ina taarifa zote muhimu za kuwezesha upatikanaji wa wa majalada kwa urahisi.
Kuhusu zoezi la kudijiti, Jaji Maghimbi amesema kuwa, Mahakama Kanda hiyo ilifanya zoezi la kudijiti majalada ambapo kwa upande wa Mahakama Kuu ilikuwa na majalada 33,330 yenye kurasa 3,174,077 ambapo kati ya kurasa hizo zilizochapwa ni 2,640,640 na kubakiwa na kurasa 533,437 ambazo hazijachapwa.
Aidha, Majalada ya Kudijiti kwa upande wa Mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Maghimbi amesema kulikuwa na jumla ya majalada 29,968 yenye kurasa 785,227 ambapo kati ya kurasa hizo zilizochapwa ni 532,530 na ambazo hazijachapwa ni kurasa 244,393.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo, amezungumzia kuhusu taarifa za majalada ya kudijiti kwa upande wa Mahakama za Mkoa wa Pwani na kusema kwamba, jumla ya majalada 7,095 yenye kurasa 173,457 yapo kwenye zoezi hilo, jumla ya kurasa 169,847 tayari zimechapwa na 3,610 bado hazijachapwa.
Maeneo ya kuhifadhi nyaraka za mashauri aliyotembelea Jaji Mkuu ni ‘Basement Archive’ sehemu ambayo inatumika kuhifadhi majalada yaliyomalizika muda mrefu na ambayo yapo katika hatua ya kupelekwa Dodoma-Kituo cha Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (RAMD). Majalada yaliyopo humo ni yaliyomalizika kati yam waka 1930 hadi 2018.
Sehemu nyingine aliyokagua ni Masjala inayofanya kazi ‘Active Registry’ ambayo inatumika kwa ajili ya kuhifadhi majalada yanayoendelea mahakamani na eneo lingine ni ‘Semi Active Registry’ ambayo ni sehemu inayotumika kuhifadhi majalada yaliyomalizika miaka ya karibuni kuanzia mwaka 2019 hadi 2023 na ambayo huwa yanahitajika kwa rejea.
Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu aliambatana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Hillary Herbert, Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam pamoja na Maafisa kadhaa wa Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyenyoosha mkono) akizungumza jambo wakati alipokuwa anakagua sehemu ambayo inatumika kuhifadhi majalada yaliyomalizika muda mrefu ‘Basement Archive’. Mhe. Prof. Juma amefanya ziara hiyo leo tarehe 09 Julai, 2024 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo (kulia) akimueleza jambo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) wakati Jaji Mkuu alipotembelea sehemu ambayo inatumika kuhifadhi majalada yaliyomalizika muda mrefu ‘Basement Archive’ iliyopo katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikagua Masjala inayofanya kazi ‘Active Registry’ ambayo inatumika kwa ajili ya kuhifadhi majalada yanayoendelea mahakamani.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia) akikagua rejesta iliyopo katika Masjala inayofanya kazi wakati alipokuwa akikagua Masjala hiyo leo tarehe 09 Julai, 2024
Ukaguzi ukiendelea ndani ya Masjala inayofanya kazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kulia) akizungumza jambo wakati Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipofanya ziara mapema leo kutembelea maeneo matatu ya kuhifadhia nyaraka za mashauri ya Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) pamoja Viongozi wengine wa Mahakama wakiwa ndani ya Masjala inayotumika kuhifadhi majalada yaliyomalizika miaka ya karibuni na ambayo huwa yanahitajika kwa rejea ‘Semi Active Registry’. Wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na kushoto kwa Jaji Maghimbi ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi ndogo ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyopo Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza jambo mara baada ya ukaguzi wa maeneo matatu ya kuhifadhi nyaraka za mashauri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akifurahia jambo wakati akiwa kwenye mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha). (Picha na Mary Gwera, Mahakama)