Na Mary Gwera, JamhuriMedia,Mahakama
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi amepongeza ushirikiano wa watumishi wa Kanda hiyo uliowezesha kupunguza mlundikano wa mashauri kutoka mashauri 595 Desemba, 2022 kufikia mashauri 162 tarehe 15 Juni, 2023.
Akizungumza hivi karibuni wakati akifungua Mafunzo ya siku mbili ya Mahakimu Kanda ya Dar es Salaam yanayofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Temeke jijini humo, Maghimbi alisema kuwa, wakiendelea kuweka jitihada na ushirikiano katika kazi, Kanda hiyo itaweka historia ya kutokuwa na mlundikano au mlundikano wa mashauri machache.
“Nawapongeza pia washiriki ambao ni Mahakimu wa ngazi mbalimbali mlio mstari wa mbele katika utoaji haki kwa kuonyesha uwajibikaji ambao unanufaisha wananchi. Mmewajibika kwa kusikiliza mashauri na kutoa maamuzi kwa kuzingatia muda iliowekwa kisheria,” amesema Maghimbi.
Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi, hadi kufikia Desemba, 2022 Kanda hiyo ilifunga mwaka ikiwa na jumla ya mashauri 2,460 na kuanzia Januari 2023 hadi kufikia tarehe 15 Juni mwaka huu jumla ya mashauri 1,053 yamefunguliwa na mpaka tarehe hiyo jumla ya mashauri 1,726 yamesikilizwa na yamebaki 1,554.
Amesema, Kanda hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zinazolenga kuondosha mashauri ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mashauri ya mlundikano yanaisha au kupungua, hatua hizo ni pamoja na kuendesha vikao maalum ‘special sessions’ vinavyohusisha Majaji wa ndani na wa nje ya Kanda hiyo.
“Ninatambua kuwa kwa Mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam, hivi sasa ina mashauri ya mlundikano 162 tu, kutoka mashauri 595 ambayo yalibaki mwezi Desemba 2022, natambua pia kwamba, mashauri haya yamekwisha ndani ya muda mfupi sana, huku kukiwa na vikao vya Mahakama ‘sessions’ takribani 13 ambavyo vimeisha tarehe 15 Juni, 2023, naamini kupitia ‘session’ hizo, Kanda ya Dar es Salaam itaendelea kupunguza mashauri ya mlundikano mengi zaidi,” ameeleza Maghimbi.
Kwa upande wa Mahakama za chini ‘Surbodinate Courts’ ambazo ni Mahakama za Mwanzo, Wilaya na za Hakimu Mkazi zilizopo ndani ya Kanda hiyo, Maghimbi amepongeza kazi wanayofanya huku akiwasisitiza Watumishi wa Mahakama hizo kuongeza kasi zaidi ya uondoshaji wa mashauri.
“Tujitathimini kwa utendaji wa haki kwa kuzingatia vigezo vinavyotajwa katika Ibara ya 107 A (2) ya Katiba (1977), yaani kuzingatia sheria wakati wa kusikiliza na kutoa uamuzi, kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi, kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka na mengine,” amesisitiza.
Akizungumzia mafunzo hayo,Maghimbi amesema kwamba chimbuko la mafunzo hayo ni Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano (5) 2020/2021 – 2024/2025 ambao unasisitiza kuwajengea uwezo watumishi wa ngazi zote za Mahakama, lengo kuu likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi na weledi majukumu waliyokasimiwa.
“Lengo la mafunzo haya ni kujenga uwezo kwenu katika maeneo mbalimbali ya utoaji haki kama vile; usimamizi wa mashauri na mienendo ya mashauri katika upokeaji wa vielelezo vya ushahidi wa kielektroniki kwenye mashauri ya madai na jinai, utaratibu wa usuluhishi (Arbitration) hapa Tanzania,” ameeleza Jaji Maghimbi.
Ameongeza kuwa, mada ya utaratibu wa usuluhishi (Arbitration) hapa nchini itatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Usuluhishi iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019, kadhalika mada za maadili ya Maafisa wa Mahakama pamoja na utekelezaji wa tuzo kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai nazo zitatolewa kwa Mahakimu hao.
Kadhalika Jaji Mfawidhi huyo, amewasihi Mahakimu hao kutumia Mafunzo hayo kama nafasi ya majadiliano na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi baina yao pamoja na wanazozipitia ili kuboresha huduma.
Maghimbi ameeleza kwamba, ana imani kuwa mafunzo hayo yatatoa matokeo chanya katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa maamuzi sahihi ya kimahakama na kwa wakati, kuleta uwazi, uwajibikaji, weledi na hatimaye kuongeza kuimarika kwa kiwango cha kuridhika kwa wateja wa Mahakama.