Na Mary Gwera,JamhuriMedia
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mustapher Mohamed Siyani amefungua Kongamano la Kimataifa linalohusu masuala ya Haki Miliki, Alama za Biashara na Usuluhishi wa Migogoro ya Miliki Bunifu ‘Judicial Colloquim on Copyrights, Trademarks and Mediation of IP Disputes’ huku akiwasisitiza washiriki wakKongamano hilo kuwa na usikivu makini ili kushughulikia vyema migogoro inayohusu masuala ya Haki Miliki.
Akifungua kongamano hilo jana kwa njia ya Mkutano Mtandao ‘Video Conference’ akiwa ofisini kwake Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam,Siyani amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Miliki Bunifu Duniani (WIPO) kwa kushirikiana kwa karibu na Mahakama ya Tanzania kuandaa kongamano linaloitwa “Judicial Colloquium on Copyright, Trademarks and Mediation of IP disputes for the Judiciary of the United Republic of Tanzania”.
“Tukio la leo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano kati ya Mahakama ya Tanzania na WIPO kwa lengo la kuimarisha mifumo na huduma za Mahakama katika ulinzi wa miliki bunifu,” alisema Siyani.
Alisema kuwa Miliki Bunifu (Intellectual Property) ni jambo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yoyote hususani katika kipindi hiki cha kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia, hivyo amesisitiza kuwa, ni muhimu kwa Maafisa wa Mahakama kuwa na maarifa na uelewa wa kina kuhusu suala hilo.
Aidha; Jaji Kiongozi amebainisha kwamba, kwenye nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kuna uelewa mdogo miongoni mwa Maafisa wa Mahakama kuhusu masuala ya Miliki Bunifu ‘IP’, hivyo ana imani kuwa, kupitia Kongamano hilo, litakalowapa nafasi ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu litasaidia kuongeza uelewa pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama kuhusu eneo hilo muhimu.
Jaji Kiongozi ameongeza kwa kulishukuru Shirika hilo kwa kuendelea kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu wa Mahakama nchini, kuchapisha maamuzi yanayohusu miliki Bunifu yanayotolewa na Mahakama ya Tanzania kwenye mtandao wa ‘WIPO Lex Judgment Database’, uandaaji wa makongamano na semina mbalimbali na kadhalika.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo kwa njia ya Mkutano Mtandao ‘Video Conference’, naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi wa Mahakama ya WIPO, Bi. Eun Joo Min amesema Shirika hilo linashiriki katika kusaidia nchi mbalimbali duniani kuwezesha kutatua migogoro inayohusiana na masuala ya Haki Miliki.
Kadhalika, Bi. Eun ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Shirika hilo na kuahidi kuwa Mafunzo zaidi yataendelea kutolewa kwa Maafisa wa Mahakama.
“Tangu tumeingia katika makubaliano ya ushirikiano, Tanzania ni moja kati ya nchi inayofanya vizuri, kwa mwaka jana mwezi Februari tuliweza kutoa Mafunzo kwa Majaji na Mahakimu 60,” alieleza Mkurugenzi huyo.
Katika siku ya kwanza ya Kongamano hilo, jumla ya Washiriki 170 wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani (T), Majaji wa Mahakama Kuu, Wasajili na Mahakimu wameweza kushiriki.
Kongamano hilo la siku tatu (3) lenye lengo la kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu katika kushughulikia mashauri yanayohusu miliki bunifu litakuwa na Wawezeshaji mbalimbali kutoka Marekani, Uswisi, Uingereza, Tanzania, Taasisi ya Uongozi wa Mahakama ya WIPO na kadhalika, na Mada kadhaa zitatolewa ambazo ni pamoja na; Majukumu ya WIPO na Kazi zake kwa Mahakama, Mifumo ya Kisheria na Haki Miliki za Kimataifa na Kikanda, Jukumu la Mahakama katika uvumbuzi na Haki Miliki, Masuala ya alama za Biashara katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za Kitaifa.
Shirika la WIPO lilianza kushirikiana kwa karibu na Mahakama ya Tanzania tangu mwaka 2018 ambapo hivi sasa wanashirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa majumuisho ya sheria na maamuzi yanayohusu miliki bunifu, uaandaji wa nyenzo za kufundishia (Training Materials) na Utatuzi wa Migogoro kwa njia usuluhishi.