Jaji Firmin Matogolo anayesikiliza shauri la mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Scolastica ya Himo, Humphrey Makundi, ameingia kwenye mvutano na waandishi wa habari wanaoripoti kesi hiyo baada ya kuwapiga marufuku kutonukuu chochote juu ya mwenendo wa shauri hilo.
Badala yake, jaji huyo kutoka Mahakama Kuu Divesheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi akawataka waandishi hao kuingia mahakamani na kusikiliza shauri hilo kama wananchi wa kawaida kwa kile alichoeleza kuwa si utaratibu kwa wanahabari kuandika kila kinachosemwa mahakamani hapo kwani jukumu hilo ni lake pamoja na mawakili.
“Naona kuna watu wanaandika-andika hapo nyuma…ni kina nani hao? Si utaratibu kuandika kila kinachosemwa hapa, wanaoruhusiwa kuandika ni mawakili waliopo hapa kwa ajili ya kumbukumbu na mimi ninayesikiliza,” alisema.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa shule hiyo, Edward Shayo, ambaye ni mshtakiwa wa pili, Hamis Chacha aliyekuwa mlinzi wa shule hiyo ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Laban Nabiswa aliyekuwa mwalimu wa nidhamu ambaye ni mshtakiwa wa tatu.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita muda mfupi baada ya shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, Dk. Alex Mremi, kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC kumaliza kutoa ushahidi wake na wakati shahidi wa pili upande huo wa Jamhuri, Koplo Augustino akiendelea kutoa ushahidi ndipo Jaji Matogolo alipowazuia waandishi hao.
Pamoja na waandishi wa habari kujitambulisha kwamba walipata ruksa ya kuripoti shauri hilo kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Jaji Matogolo alishikilia msimamo wake wa kutowaruhusu waandishi kunukuu chochote.
Katika hali ambayo si ya kawaida, Jaji Matogolo aliwataka waandishi hao wa habari mara baada ya kusikiliza kinachoendelea mahakamani hapo wawasiliane na Naibu Msajili huyo wa Mahakama, Frank Mahimbari, ili awapatie taarifa za kesi hiyo.
Tukio hilo ambalo ni nadra kutokea kwa waandishi wa habari kuzuiwa kuripoti mashauri mbalimbali mahakamani hapa nchini liliwashitua waandishi waliokuwemo katika chumba cha mahakama huku baadhi yao wakitoka nje ya ukumbi huo.
Baadhi ya waandishi wa habari waliokumbana na kadhia hiyo wamelaani kitendo hicho cha Jaji Matogolo kuwazuia kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuhabarisha umma kupitia kalamu zao huku wengine wakidai kitendo hicho kinawanyima wananchi wanaofuatilia tukio hilo kujua kinachoendelea mahakamani hapo.
“Kuna wazazi wana watoto wao hapo Shule ya Scolastica wanafuatilia kwa umakini hilo tukio na mwisho wangependa kujua mwenendo wa kesi na waandishi wa habari pekee ndiyo wanaoweza kuwafikishia ujumbe wa kinachondelea kupitia kalamu zao, leo unapowazuia waandishi wasinukuu chochote maana yake unawanyima wananchi haki ya kupata habari,” amesema mwandishi mmoja.
Hata hivyo waandishi wa habari kwa kushirikiana na viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Kilimanjaro (MECKI) wakiongozwa na katibu wao, Nakajumo James, waliendelea kupaza sauti kulalamikia kitendo cha jaji huyo kuwazuia kuripoti mwenendo wa kesi hiyo.
Juhudi hizo zilizaa matunda baada ya kukutana na Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya Moshi na baada ya mazungumzo yaliyochukua zaidi ya dakika 20 nje ya mahakama hiyo, hatimaye waliruhusiwa kuendelea na majukumu yao.
“Tumeona hata kwenye mitandao ya kijamii mmelalamika na hata viongozi wetu wameona na kutupigia simu wakitaka kujua nini kimetokea lakini mheshimiwa jaji hakuwa na nia mbaya maana hakuwa anafahamu kama ninyi ni waandishi wa habari,” amesema msajili huyo.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili huyo, Jaji Matogolo pia alitilia shaka weledi wa baadhi ya waandishi katika kuripoti mashauri mbalimbali mahakamani baada ya kuwepo kwa baadhi ya waandishi wa habari (si wanaoripoti kesi hiyo) kupotosha baadhi ya kile kinachozungumzwa mahakamani.
“Kwanza poleni kwa usumbufu mlioupata, lakini baada ya kuliona hilo tumezungumza na mheshimiwa jaji na amewaruhusu muendelee kuripoti hilo shauri, lakini nawaombeni mzingatie weledi na pale mtakapoona kuna jambo halijaeleweka vizuri msisite kuonana na mawakili walioko mahakamani au mimi,” amesema.
Tukio lilivyotokea
Marehemu Humphrey Makundi aliripotiwa kutoweka shuleni hapo Novemba 6, mwaka 2017 na baadaye Novemba 10 mwili wake ukaokotwa ndani ya Mto Ghona unaotajwa kuwapo umbali wa mita 300 kutoka shuleni hapo ingawa mwili huo uliandikishwa kama mwili wa mtu mzima.
Mwili huo uliopolewa na polisi kutoka Kituo cha Polisi Himo na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi na ulizikwa siku iliyofuata na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga.
Polisi kwa kushirikiana na baba wa marehemu, Jackson Makundi, waliendelea na uchunguzi baada ya kutilia shaka mwili uliozikwa na Manispaa ya Moshi, kisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwasilisha ombi mahakamani la kuomba kibali cha kuufukua mwili huo.
Novemba 19, mwaka 2017 Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ilitoa kibali na mwili huo ukafukuliwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na baadaye ulimwagiwa maji usoni ambako baba mzazi wa marehemu aliweza kuutambua kuwa ndiye mtoto wake.
Mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako ulifanyiwa uchunguzi ulioshuhudiwa pia na baba mzazi wa marehemu, na baada ya uchunguzi ikabainika marehemu kukutwa na jeraha kwenye paji la uso.
Kesi yanguruma mahakamani
Upande wa Jamhuri umeita zaidi ya mashahidi 34 kwa ajili ya kuthibitisha kosa pamoja na vielelezo 15 vya nyaraka yakiwamo maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Hamis Chacha, aliyoyatoa polisi na kwa mlinzi wa amani.
Vielelezo vingine ni pamoja taarifa ya kifo cha marehemu, mawasiliano ya simu kutoka mtandao wa simu wa Vodacom yanayoonyesha washtakiwa kuwa waliwasiliana siku na muda wa tukio.
Tayari mashahidi sita wamekwisha kutoa ushahidi wao akiwamo baba mzazi wa marehemu ambaye alikuwa shahidi wa pili upande wa mashtaka na daktari bingwa kutoka KCMC, Dk. Alex Mremi, ambaye aliongoza jopo la madaktari kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.
Mashahidi wengine ni daktari bingwa wa kinywa na meno kutoka KCMC ambaye naye alikuwa kwenye jopo la uchunguzi wa mwili, Koplo Augustino kutoka Kituo cha Polisi Himo ambaye alishiriki kuuopoa mwili wa marehemu kutoka Mto Ghona na Anastazia Januari – muuguzi wa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi ambaye alikuwa zamu usiku wakati mwili marehemu ukipelekwa kuhifadhiwa.
Pia yupo Koplo Shaaban Omary kutoka Ofisi ya RCO Kilimanjaro ambaye Novemba 20, mwaka 2017 alikabidhiwa sampuli za vinasaba kwa ajili ya kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.
Akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na Wakili Joseph Pande ambaye ni wakili wa serikali mkuu na kiongozi wa jopo la mawakili wa mashtaka, shahidi huyo alidai kuwa sampuli hizo zilikuwa kwa ajili ya kuchunguza uwiano wa vinasaba (DNA) kati ya mwili wa marehemu uliookotwa na wazazi Jackson Makundi pamoja na mkewe, Joyce Makundi.