…………………………………..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali inatarajia kunufaika na takribani shilingi trilioni 2.44 kwa mwaka kutokana na Biashara ya Kaboni.
Amesema hayo leo Julai 14, 2023 wakati akifungua Majadiliano ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kuhusu Biashara ya Kaboni kilichofanyika jijini Dar es Salaam kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) jijini Dar es Salaam leo Julai 14, 2023.
Dkt. Jafo amesema kuwa Pamoja na kukuza uchumi wa nchi pia mapato hayo yatasaidia katika kupambana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inayoyakabili baadhi ya maeneo nchini.
Kutokana na umuhimu huo amepongeza jitihada za wadau wanaojihusisha na uhifadhi wa mazingira akisisitiza Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa Biashara ya Kaboni.
Aidha, Waziri Jafo ameongeza kuwa kwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika uhifadhi wa mazingira Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wawekezaji hao kwa kuwapa nafasi ya kutumia fursa zilizopo katika biashara hiyo.
“Tumshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika hifadhi ya mazingira na kutokana na hatua hiyo tuna imani kubwa kuwa sekta ya mazingira katika nchi yetu itazidi kuimarika,” amesema huku akiongeza kuwa limetengwa eneo la ekari milioni 48.1 kwa ajili ya Biashara ya Kaboni.
Amesema kuwa kwa kutambua jitihada za wadau katika utunzaji wa mazingira, Serikali tayari imeandaa Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2022 ambazo zinatoa mwelekeo kwa wadau wenye nia ya kuwekeza katika biashara hiyo.
Dkt. Jafo amefafanua kuwa tangu Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iandae kanuni na mwongozo huo idadi kubwa ya wawekezaji wa Biashara ya Kaboni na wamejitokeza ambapo Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo Chuo mjini Morogoro kimesajili kampuni 21 zinazojihusisha na Biashara ya Kaboni.
“Ni matarajio yetu kuwa Biashara ya Kaboni itasaidia kupunguza kiwango cha gesijoto kwa asilimia 30 hado 35 ifikapo mwaka 2023 hivyo tutaendelea kuongeza nguvu katika kushirikiana na wadau katika kufanikisha hatua hii,” amesema Dkt. Jafo.
Akitoa neno la ukaribisho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TPSF Bw. Raphael Maganga ameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kukabilianja na athari za mabadiliko ya tabianchi na katika nyanja mbalimbali hapa nchini.
Amesema majadiliano hayo yatasaidia kujenga uelewa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kuhusu changamoto za mazingira na mbinu mbalimbali za kuweza kukabiliana nazo.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya dunia na kuwa inasabaisha athari mbalimbali kwa mazingira na afya hivyo ni muhimu kuendelea kutoa elimu ya kukabiliana nazo.