Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo ametoa muda wa siku 7 kwa Wafanyabiashara na Wananchi Wenye Mifuko ya plastiki iliyokatazwa kuisalimisha kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kupitia kikosi kazi au Kwenye Kiwanda walichochukulia Mzigo.
Pia Waziri Jafo amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kwa Operesheni ya kukamata Mifuko hiyo.
Waziri Jafo ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara kwenye Kiwanda Swallow investment Ltd kilichopigwa faini ya Shilingi Milioni 100 kwa kosa la kuzalisha Mifuko iliyokatazwa ambapo zaidi ya Tani 41 za Mifuko hiyo zimekamatwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Jafo amempongeza RC Makalla kwa kufanikisha kukamatwa kwa Shehena ya Mifuko hiyo kupitia Operesheni aliyotangaza na kuelekeza Mikoa mingine kuiga mfano wa Mkoa wa Dar es salaam.
Aidha Waziri Jafo amemtaka Mmiliki wa Kiwanda hicho kulipa faini aliyopigwa ndani ya siku 14 na kuhakikisha anatoa gharama zote za uteketezaji wa mzigo uliokamatwa na Mifuko iliyoingizwa sokoni ahakikishe anaikusanya.
Pamoja na hayo Waziri Jafo ameelekeza Kiwanda hicho kuanza mchakato wa kupata cheti Cha tathimini ya athari za mazingira na kuzitaka Mamlaka za TRA, TBS, NSSF na Taasisi nyingine kufika kiwandani hapo kuona Kama wanazingatia taratibu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) alipozungumza amewataka wawekezaji kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, pamoja na Kanuni zake ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea ikiwemo kutozwa faini au kuchukuliwa hatua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amemshukuru Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Mazingira kwa kumuunga mkono kwenye Operesheni hiyo.