Jafo: Athari za mazingira zimesababisha mfumuko wa bei
JamhuriComments Off on Jafo: Athari za mazingira zimesababisha mfumuko wa bei
………………………………………………………………..
Imeelezwa athari za kimazingira nchini zimechangia kupanda kwa bei ya vyakula ikiwemo unga wa mahindi kutoka na kukosekana kwa mvua na hata maeneo ilikonyesha ilikuwa ni chini ya wastani.
Hayo yameelezwa leo Juni 1,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt.Selemani Jafo,wakati akishiriki zoezi la kupanda miti katika shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku mazingira Duniani itakayofanyika Juni 5, mwaka huu.
Waziri Jafo amesema kuwa ili kukabilina na hali hiyo serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na athari hizo za kimazingira ikiwepo kuzindua kampeni ya upandaji miti pamoja na ile soma na mti katika shule za msingi na sekondari nchini.
“Nitoe shukrani kwa Rais wetu kuwa mfano na kuhamasisha utunzaji wa mazingira tangu akiwa Makamu wa Rais lakini pia Ilani ya uchaguzi ya CCM YA mwaka 2020, inaelekeza kila halmashari nchini kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka”amesema Dkt.Jafo
Aidha Dkt. Jafo ameagiza vibali vya ujenzi vinavyotelewa katika halmashauri nchini kuelekeza wamiliki wa maeneo kupanda miti kabla ya kuanza ujenzi ili kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo Waziri Jafo amewataka watanzania kuungana kwa pamoja kushiriki maadhimisho ya wiki ya mazingira Kwa kupanda miti ili kukabiliana na athari za Mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, amesema wameshiriki katika kampeni ya upandaji miti na kupiga marufu ya matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
”Nampongeza Rais Samia kwa kuendeleza juhudi za kutunza mazingira katika mkaoa wa Dodoma tangu akiwa makamu wa Rais mpaka sasa.”amesema RC Senyamule
Naye Mwanafunzi wa Kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Kiwanja cha Ndege Shadia Ramadhan Kimaro,amesema kuwa watahakikisha wanatunza miti hiyo walio ipanda ili kuhakikisha lengo la serikali la kupanda miti katika maeneo mbalimbali nchini linatimia.