Na Mwandishi Wetu JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo amemwagiza mkandarasi kampuni ya LI JUN Construction ya China anayejenga jengo la Metrolojia la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kukamilisha kwa wakati na kwa ubora waliokubaliana kwenye mkataba.

Waziri Jafo alitoa maelekezo hayo jana alipotembelea ujenzi wa jengo hilo unaoendelea chuoni hapo ambalo litatumika kwaajili ya masomo ya metrolijia na vipimo.

Waziri Jafo alipongeza uongozi wa CBE kwa kuanzisha ujenzi huo ambao alisema utaweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi wengi wa fani hiyo kusoma katika mazingira bora na tulivu.

“Nawashukuru wasimamizi wa kazi hii nimeona imefikia asilimia 50 na kazi inakwenda vizuri ila mkandarasi ahakikishe azingatie ubora kwa kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika kama nondo vinapimwa kwenye maabara zetu na mshauri anayefanyakazi kwa niaba ya serikali awe makini kuona ubora unazingatiwa,” alisema

Alisema serikali imewekeza kwenye miundombinu ya serikali ili kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata elimu bora na yenye kuzingatia mahitaji ya ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

“Naomba niwasisitiza watanzania watumie fursa ya masomo haya wachangamkie kwasababu tunahitaji wataalamu wa ndani hatutakiwi kutegemea wan je lazima tuzalishe wataalamu wetu wenyewe,” alisema

Naye Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga alisema jengo hilo litakaloitwa Metrology Complex litakuwa na kumbi za mihadhara, karakana na maabara kwaajili ya kuchukua wanafunzi zaidi 4,000.

“Metrolojia ni sayansi ya vipimo na viwango na inasoko kubwa kwa watu wanaohitimu fani hiyo kwa hiyo napenda kuwahamasisha watanzania waje wasomeee fani hii,” alisema Profesa Lwoga

Alisema jengo hilo litakalogharimu bilioni 24 lilianza kujengwa Mei 2023 na awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika mwaka 2026 na baada ya hapo itaanza awamu ya pili ya ujenzi ambayo inatarajaiwa kukamilika mwaka 2029.

Mwakilishi wa Kampuni ya LI Jun Construction Titus Kizito, alisema ujenzi unaendelea vizuri na wanatarajia kukamilisha awamu ya kwanza mwaka 2026 kama walivyokubaliana na mteja kwenye mkataba wa ujenzi huo.

“Tumechukua maagizo ya waziri kwa uzito mkubwa sana na tutahakikisha tunazingatia ubora wa kazi kama tulivyokubaliana kwenye mkataba na jengo likamilike kwa wakati,” alisema.