Ni vyema nianze kwa kuweka wazi kwamba nilikuwa sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa hadi katikati ya mwaka 2016. Ilikuwa tukio la kihistoria kwangu baada ya kuvifuatilia kwa kina vyama vyote kwa muda mrefu.

Katika kuelezea kilichonisukuma hadi kufikia uamuzi huo, si vibaya kuanza kwa kukumbuka maneno murua aliyotamka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa anang’atuka uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, mwezi Agosti 1990, juu ya jukumu la chama cha siasa.

Namnukuu: “Chama cha siasa ni chombo kinachowaunganisha kwa hiari watu wenye itikadi moja na shabaha moja. Na katika utaratibu wowote ule, chama kinahitaji kuzitambua waziwazi hizo shabaha zake: Kinataka kufanya nini na kwa nini?”

Kwa kuwa kila chama hudai kuwa kinaitakia nchi mambo mema na mema yote hayawezi yakafanywa wakati ule ule, basi ni vizuri kiwe na hakika pia juu ya mpangilio wa umuhimu wa shabaha zake.

Ni lazima baadhi ya shabaha zitekelezwe kabla ya nyingine; na hii angalau kwa muda inaweza ikaleta uwiano mbaya baina ya shabaha moja na shabaha nyingine.

Hakuna ubishi kwamba vyama vyote vya siasa hapa nchini, kwa muda mrefu vimekuwa na matatizo ya aina mbalimbali. Kutokana na ukubwa wa vyama viwili vya CCM na Chadema, na kwamba, Chadema kimeandika historia kwa kuwa na idadi kubwa kidogo ya wabunge, sina budi kuvitazama kwa jicho la tatu.

Nikianza na CCM, matatizo yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku tangu Mwalimu alipoanza kukiponda waziwazi zaidi ya miaka ishirini iliyopita.

Sijui kwa kweli leo hii angezungumza nini juu ya chama hicho maana pamoja na mabadiliko ya kiutendaji anayojaribu kuonyesha Rais John Magufuli, wakati nchi yetu inapata uhuru, Mwalimu aliandika juu ya umuhimu wa mabadiliko yanayoambatana na utulivu.

Si vema wananchi wanaamka asubuhi na wasijue kitakachotokea siku hiyo. Changamoto mbalimbali ndani za CCM zimepata kuelezwa hata na mmoja wa viongozi wa juu wa Serikali ya CCM, Profesa Mark Mwandosya, ambaye aliandika kitabu kizuri, ambacho inaelekea kabisa viongozi wengi wa nchi kama kawaida yao hawakukisoma maana wangehakikisha kwa vyovyote vile wanazingatia mambo mengi tu ya msingi yaliyomo katika kitabu hicho.

Katika kuelekea mchakato wa kihistoria wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka jana, ambako tulishuhudia watu zaidi ya arobaini wakigombania fomu kana kwamba ofisi hiyo haina uzito wowote. Na kibaya zaidi hadi Mkuu wa nchi alitamka kwamba huko ni kukua kwa demokrasia.

Tukio hilo likanikumbusha kilichotokea mwezi Oktoba 2015 katika nchi maskini kabisa katika ukanda wa Amerika, Haiti. Nchi hiyo inasifika zaidi kwa masuala ya ushirikana na mapinduzi ya kijeshi.

Katika uchaguzi wao mkuu, watu takriban arobaini waligombea urais kupitia vyama tofauti, jambo ambalo linaonyesha kuna mzaha mkubwa sana kuhusu nafasi hiyo.

Nikirejea kwa Profesa Mwandosya, katika kitabu chake amejitahidi kufafanua nini maana ya makundi katika Chama kwa kuchukua mfano wa Chama cha ‘Labour’  cha Uingereza, Chama ambacho kina uhusiano wa kijadi na CCM.

Profesa Mwandosya katika kitabu chake hicho, aliipiga kijembe dhana ya Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru kuhusu makundi katika Chama.

Anaandika: “Makundi au yanayojiita makundi katika Chama chetu ni tofauti kabisa. Ni makundi ya ushabiki wa watu. Ni kama zile zinazoitwa ‘Fan Club’ ambazo vijana wanampenda mpiga muziki au msanii kwa sababu wanampenda,”

Anaendelea kuandika; “Ni ushabiki zaidi kuliko makundi. Ndio maana yanajitokeza wakati wa uchaguzi. Na makundi mengine yanasema waziwazi kwamba wakati wa uchaguzi ni wakati wa ‘mavuno’.”

Sidhani ni busara kuyatukuza hata kuyatambua makundi hayo. “Hadithi ya CCM, hasa ukizingatia mchango wake katika ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, ni ya kusikitisha! Na isitoshe mpaka leo hii chama hicho kinaendelea kujitambulisha kama cha kijamaa.

Nikikitazama Chadema, hakika kuna wakati fulani chama hicho kilisaidia kuongeza mwamko kwa Watanzania juu ya kutambua haki za kiraia. Ila kuna matukio mengine makubwa yaliyozua maswali kuliko majibu.

Nitazungumzia jambo moja tu ambalo linanitatiza. Sote tutakumbuka kwenye Bunge la Katiba, namna ambavyo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alivyokuwa na ushawishi mkubwa kwa upande wa wabunge wa CCM.

Hoja nzito ilikuwa ni Serikali ngapi zinatakiwa kwenye Serikali ya Muungano. Na ndipo tuliposhuhudia baadhi ya vyama vya upinzani vikiunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Lowassa alikuwa ni muumini wa Serikali mbili, huku wale wa Ukawa wakihitaji serikali tatu. Kufuatia kukatwa kwa Lowassa kwenye mbio za urais ndani ya CCM, akageuka kuwa muumini wa Serikali tatu na kusema kwamba kwa miaka mingi alikuwa ni muumini wa Serikali tatu.

Cha kustaajabisha zaidi, ni jinsi ambavyo watu waliokuwa wanalilia Serikali tatu, walivyomkubali kirahisi mtu wa Serikali mbili. Maana yake ni kwamba ndani ya vyama hivi viwili vikubwa imani si lolote, si chochote.

Haiwezekani mtu aliyefikia ngazi ya kuwa Waziri Mkuu, ghafla aseme yeye ni muumini wa Serikali tatu. Vilevile hata Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye. 

Pia, nimejikuta najiuliza maswali kuhusu umakini wa chama hicho kwenye masuala ya nje ya nchi. Yaani Chadema, kwa kadri nilivyowafuatilia kwa miaka mingi kimataifa, walikuwa ni marafiki wa karibu wa chama cha Orange Democratic Movement nchini Kenya.

Lakini hapo hapo ukiangalia itikadi ya Chadema, wao ni sehemu ya International Democrat Union  na ODM ni sehemu ya Liberal International. Katikati yao sasa ni Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ambaye amekuwa akishirikiana kwa karibu na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kiasi cha kukaribishwa kuhutubia mkutano mkuu wa ODM mwaka 2012.

Chadema kwenye mkutano ilikuwa kama haipo kabisa japokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2013, ilitaarifiwa kukisaidia ODM kiasi cha kudhihakiwa na baadhi ya viongozi wa CCM baada ya matokeo kutangazwa.

Katika mazingira hayo nilijikuta najiuliza maswali mengi bila kupata majibu kuhusu hivi vyama viwili vikubwa vya siasa. Ni nini hasa wanachokisimamia? Ina maana Chadema ilikuwa inajikomba zaidi kwa ODM ili pengine ipate msaada kutoka nje?

Katika kufikia uamuzi wangu wa kujiunga na UDP, nimetafakari sana hadi kuona ni vyema kujiunga na chama hicho.

Sababu ya kwanza inanirudisha uchaguzi wa 1995, kufuatia nchi kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi. Kwa kifupi, baadhi ya Watanzania watakumbuka mdahalo wa kihistoria wa wagombea urais uliofanyika kwenye hoteli ya Kilimanjaro.

Wagombea wakati huo walikuwa ni Benjamin Mkapa wa CCM, Augustine Mrema wa NCCR Mageuzi, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na John Cheyo wa UDP. Ni mdahalo huo uliosababisha Watanzania wengi kuanza kumwita mzee Cheyo kwa jina la Bwana Mapesa.

Alikuwa na ujumbe mahsusi kwa wananchi. Nadiriki kusema aliwafunika wagombea wengine wote na pengine isingekuwa mazingira magumu ya kisiasa ya wakati huo, angepigiwa kura nyingi zaidi. Msimamo wa UDP miaka yote unapingana na msemo kwamba “maendeleo sio fedha” kutokana na kwamba unaficha umuhimu wa fedha katika kuleta maendeleo.

Sina budi nisisitize pia UDP tunaamini sana katika midahalo na mijadala kwa ngazi zote nchini. Kwa bahati mbaya tangu mwaka 1995, suala la midahalo kwa wagombea urais limeota mbawa kiasi cha kuifanya nchi ya Kenya ionekane imepiga hatua kubwa kufuatia mdahalo uliofanyika nchini humo wa wagombea urais mwaka 2013 kwa mara ya kwanza.

Ni jambo la ajabu sana kwa kweli kwamba kwenye uchaguzi mkuu wa 2015, uliokuwa na joto kubwa kuwahi kutokea nchini, wagombea wote wa vyama viwili vikubwa, Dk. John Magufuli na Edward Lowassa, hawakushiriki.

Katika kutaka kuona nchi inajenga utamaduni wa midahalo, UDP tunasisitiza kwamba katika shule zetu na vyuo vyetu vikuu, wanafunzi wanapaswa kushiriki mara kwa mara. Si jambo mwafaka Rais wa nchi anapowaambia wanafunzi wasijihusishe na siasa vyuoni. Hivi viongozi wa kweli watapikwa wapi vizuri kama si vyuoni?

Popote vyuo vya juu ni chemchem ya mawazo juu ya mambo mbalimbali.  Itakumbukwa zamani Chuo Kikuu cha Dar es salaam kilikuwa ni maarufu sana kwa wanafunzi kujihusisha na masuala makubwa kitaifa na hata ya kimataifa kwa njia ya midahalo kiasi cha kuandamana ikibidi.

UDP tunapenda sana kuona wanafunzi ambao wanajitambua kwamba wamepata bahati ya kufika kwenye elimu ya juu hivyo wahakikishe wanajiendeleza kwa kila hali kwa faida ya ndugu zao ambao hawakupata bahati hiyo.

Na kupitia kuwezesha Watanzania kwenye fursa za kiuchumi na kuwajengea utamaduni wa kulipa kodi, miaka yote UDP inaamini katika uwezo wa kutoa huduma ya elimu mpaka ngazi ya chuo kikuu bure, sera ambayo imedandiwa na CCM. 

Ni muhimu kusisitiza pia kwamba UDP katika kutaka kuona Watanzania wana uwezo wa kuthubutu kwenye masuala makubwa, haiamini kabisa katika siasa za umaskini ambazo maana yake barani Afrika ni kutumia ugumu wa maisha kuhakikisha viongozi na wananchi wanabaki wanyonge. Itaendelea wiki ijayo. 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784 219535