Israel ilifanya mashambulizi ya angani katika vitongoji vya kusini mwa Beirut siku ya Jumapili, baada ya kuamuru kuhamishwa kwa wakazi waliokuwa wakiishi katika jengo ambalo ilisema lilikuwa linatumiwa na kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah.

Shambulio hilo lilitokea licha ya usitishaji mapigano ulioanza kutekelezwa miezi mitano iliyopita ambao ulimaliza mzozo kati ya Israel na kundi la kijeshi.

Israel ilisema kuwa ililenga hifadhi ya Hezbollah ya “makombora ya kuongozwa kwa usahihi” ambayo “ilisema ni tishio kwa Israeli na raia wake”.

Ofisi ya rais wa Lebanon ililaani shambulizi hilo na kuzitaka Marekani na Ufaransa – ambazo zilisimamia usitishaji mapigano mwezi Novemba – kuishinikiza Israel kusitisha mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo.

Shambulio hilo linadaiwa kuwa la kwanza kwa karibu mwezi mmoja ambapo Israel imeshambulia vitongoji vya kusini mwa Beirut – vinavyoitwa Dahieh – ambapo Hezbollah ina makao yake.

Hii itaweka shinikizo zaidi kwenye usitishaji mapigano. Licha ya makubaliano hayo, Israel imefikia malengo ambayo inasema yanahusishwa na Hezbollah karibu kila siku. Serikali ya Israel imesema kuwa itajibu vitisho vyovyote kutoka kwa Hezbollah.

Maafisa wa nchi za Magharibi, waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, wameiambia BBC kwamba kundi hilo la wanamgambo limekuwa likizingatia kwa kiasi kikubwa mapatano hayo, huku wakiishutumu Israel kwa ukiukaji mwingi unaojumuisha mashambulizi ya anga na ufuatiliaji wa ndege zisizo na rubani.

Kanda za moja kwa moja zilizorushwa na Reuters zilionyesha moshi mwingi ukifuka kutoka kwa jengo lililolengwa saa moja baada ya jeshi la Israel kutoa agizo la kuondoka kwa wakaazi wa kitongoji cha Hadath.