Israel inasema inawashambulia kwa kuwalenga Hezbollah kusini mwa Lebanon baada ya roketi kurushwa kutoka huko kuelekea Israel kwa mara ya kwanza tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa mnamo Novemba.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema alikuwa ameagiza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) “kuchukua hatua kali dhidi ya walengwa kadhaa wa kigaidi nchini Lebanon”.
IDF ilisema kuwa roketi tatu zilidunguliwa katika mji wa Metula, kaskazini mwa Israel, Jumamosi asubuhi. Hakuna majeruhi walioripotiwa. Hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulio hilo, huku Waziri Mkuu wa Lebanon akionya dhidi ya nchi yake “kuingizwa katika vita vipya”.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa yalimaliza miezi 14 ya mapigano na Hezbollah, kundi lenye silaha la Lebanon linaloungwa mkono na Iran. Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (Unifil) limesema lina “wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa machafuko”, likizitaka Israel na Lebanon “kuzingatia ahadi zao”.
Ripoti za ndani nchini Lebanon zilisema kuwa mashambulizi ya mizinga yamefanywa katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yamekuwa dhaifu: Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga karibu kila siku kwenye kile inachodai kuwa wanawalenga Hezbollah, na imeashiria kuwa mashambulizi yataendelea ili kuzuia kundi hilo kujiimarisha upya kwa silaha.
Mbali na hayo, jeshi la Israel bado linakalia maeneo matano kusini mwa Lebanon, jambo ambalo serikali ya Lebanon inasema ni uvunjaji wa mamlaka ya nchi hiyo na ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo yaliamuru kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel.
Israel inasema jeshi la Lebanon bado halijapelekwa kikamilifu katika maeneo hayo, na kwamba inahitaji kubaki hapo ili kuhakikisha usalama wa jamii zake za mpakani.
Shambulio la roketi la Jumamosi dhidi ya Israel litaongeza shinikizo kwa serikali ya Lebanon, na huenda likatumiwa na Israel kama uthibitisho kwamba jeshi la Lebanon halina udhibiti kamili wa maeneo ya mpakani.
