Israel imesema ililenga shabaha nchini Lebanon Jumatatu jioni baada ya kuapa kulipiza kisasi kwa shambulio la Hezbollah kwenye kituo cha kijeshi, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa kukiuka usitishaji vita wa wiki iliyopita.
Takriban watu tisa waliuawa na mashambulizi ya Israel katika vijiji viwili vya kusini mwa Lebanon, kulingana na wizara ya afya ya umma ya nchi hiyo.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema lilifikia maeneo lengwa ya Hezbollah na miundombinu “Lebanon nzima”, huku likirejelea kujitolea kwake kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hezbollah ilisema ilikuwa ikijibu “ukiukaji” wa Israel na kuongeza kuwa ilifanya shambulizi la “kujilinda kama onyo”, ikifyatua risasi kwenye kituo cha jeshi la Israel katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel.
Israel ilisema hakukuwa na majeruhi katika mashambulizi ya Hezbollah kwenye eneo la Mlima Dov – linalozozaniwa kwenye mpaka wa Israel-Lebanon linalojulikana kimataifa kama Mashamba ya Shebaa.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alielezea shambulio la Hezbollah kama “ukiukaji mkubwa wa usitishaji mapigano”, na kuapa kuwa Israel “itajibu vikali”.
Wakati makubaliano ya kusitisha mapigano yalipotangazwa kwa mara ya kwanza, Netanyahu alisema nchi yake haitasita kufanya mashambulizi ikiwa Hezbollah itavunja masharti.
Ghasia za Jumatatu ni dalili ya jinsi usitishaji vita uliokubaliwa hivi karibuni unavyoyumba, ambao unaolenga kumaliza mzozo wa miezi 13 kati ya Israel na Hezbollah.