Wakati maelfu ya raia wa Lebanon wakirejea kwenye makazi yao, Israel imesema inaendelea kupambana na wanamgambo wa Hezbollah licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari, wanajeshi wa Israel jana waliwaua wapiganaji kadhaa wa Hezbollah katika eneo la kusini mwa Lebanon.

Uwepo wa wapiganaji katika eneo hilo kulikiuka makubaliano hayo na Hagari amesisitiza kuwa “kila ukiukaji wa vifungu vya mkataba huo wa usitishaji vita, utajibiwa kwa mashambulizi.

Vikosi vya Israel vimesema pia, vinawazuia watu kadhaa waliokuwa wakikaribia maeneo kusini mwa Lebanon ambako wanajeshi wa Israel wanaendelea kuweka kambi, ingawa wanatakiwa kuondoka kwa awamu kutokana na masharti muhimu ya mkataba huo wa kusitisha mapigano.


Makubaliano hayo ya muda wa miezi miwili yameweka wazi kwamba kundi la Hezbollah linapaswa kuwaondoa wapiganaji wake katika eneo la kusini mwa Lebanon na kuelekea upande mwingine wa mto Litani, takriban kilometa 30 kaskazini mwa mpaka wa Israel na Lebanon.

Wanajeshi wa Israel wanatakiwa pia kurejea nchini mwao. Jeshi la taifa la Lebanon kwa ushirikiano na walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL, ndio wenye jukumu la kulinda usalama katika eneo hilo la mpakani.