Jeshi la Israel limesema “lipo tayari kwa hali yoyote inayoweza kujitokeza” baada ya kufanya shambulio katika mji mkuu wa Lebanon Beirut na kumuua naibu kiongozi wa kundi la Hamas.
Shambulizi hilo limezusha hofu ya vita vya Gaza kutanuka na kuwa mzozo mkubwa zaidi wa kikanda.
Afisa wa ngazi ya juu wa usalama nchini Lebanon ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Saleh al-Aruri ameuawa pamoja na walinzi wake katika shambulio lililofanywa na Israel.
Kufuatia tukio hilo, kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh amesema kuwa vuguvugu “ambalo viongozi wake wanafariki kama mashahidi kwa ajili ya hadhi ya watu na taifa lao kamwe halitashindwa”.
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati amelaani mauaji hayo na kusema “yanalenga kuitumbukiza Lebanon” katika vita hivyo. Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari hakuzungumzia moja kwa moja juu ya mauaji hayo, lakini ameeleza kuwa wamejiandaa kwa hali yoyote.