WAPIGANAJI wa kundi la Taifa la Kiislamu la Iraq na Levant (ISIL), wanazidi kuwatesa Wamarekani, kiasi kwamba hata Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), limekiri kwamba mapambano dhidi ya waislamu hao ni magumu.
Rais Barack Obama ametangaza vita dhidi ya ISIL ambao kwa sasa wako katika mpaka wa Syria na Iraq, lakini majasusi wake, wamemwambia kwamba “Hatutakwenda huko kwa kukurupuka kwa sababu wako wengi. ”
Taarifa ambazo CIA walizitoa mwishoni mwa wiki iliyopita ni kwamba ISIL ina wapambanaji wengi wanaofikia zaidi ya 30,000, tofauti na 10,000 iliyotangazwa awali.
“Wako wa mataifa yote, wako wa Iraq pia wa Syria, pia wako wa kutoka mataifa mengine,” ilisema taarifa ya CIA ambayo ilikwenda kwa Rais Obama ambaye ametangaza vita dhidi ya kundi hilo lililoanza uasi mapema mwaka huu kwa lengo la kuanzisha taifa la Kiislamu katika mpaka wa Syria na Iraq.
Obama amecharuka zaidi mara baada ya waasi hao kuwaua kwa kuwakata vichwa waandishi wa habari wa Marekani na Uingereza.
Taarifa zaidi zinasema kwamba mataifa 10 ya Kiarabu yamekubaliana kuisaidia Marekani na Uingereza katika vita dhidi ya wapiganaji hao.
Saudi Arabia, ndio wameongoza nchi hizo kuingia makubaliano hayo baada ya kushawishiwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, John Kerry. Kerry alikutana viongozi wa nchi hizo, mjini Jeddah.
Kwa kuanzia tu, nchi hizo zimeamua kusimamisha misaada ya fedha kwa wapiganaji hao ambao kwa sasa wanashikilia sehemu kubwa katika mpaka huo wa Syria na Iraq.
Mwisho.