Katika sehemu ya kwanza ya makala hii tuliona kuwa mtu unapaswa kuishi kwa kufuata ndoto yako. Ndoto yako isiongozwe na maneno ya watu. Acha wakuseme wawezavyo lakini wewe pambana kutimiza ndoto yako. Acha leo wakuone kichaa ili kesho wakushangae. Endelea…
Ishi kabla ya kufa. Kuna watu wanakufa kabla ya kuishi. Kivipi watu wanakufa kabla ya kuishi? Ninakujibu nisikilize kwa umakini. Mtu yeyote aliyekata tamaa ya maisha ni kama amekufa ingawa bado anavuta hewa katika sayari hii ya dunia.
Kila mara tunapoacha kufanyia kazi ndoto zetu tulizonazo au tunapoamua kuacha kutumia vipaji ni kama tunaanza kufa. Tunapoacha kutenda matendo yenye kuleta ustawi kwetu na kwa wenzetu, tunaanza kufa. Tunapolalamika kwa kila jambo ni kama tunaanza kufa. Unaposoma makala ya kitabu hiki fufuka. Fufua ndoto zako upya.
Ota ndoto kubwa katika maisha yako.
Ota kufanya mambo makubwa na mazuri katika dunia hii. Mwanahabari Ruge Mutahaba anasema: “Sipendi ndoto ndogo. Napenda ndoto kubwa. Ukiwa na ndoto ndogo huwezi kuifikia ndoto kubwa.”
Penda ndoto kubwa. Ndoto yako haitakufa mpaka utakapokufa wewe. Ndoto kubwa inaacha alama duniani. Mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote anasema: “Baada ya kifo changu, ninataka nikumbukwe kama mmiliki mkubwa sana wa viwanda Afrika.” Hii ni ndoto inayoishi milele.
Mwandishi Wayner Dyer katika kitabu chake cha The Power of Intention anasema: “Nia yetu inaumba uhalisia wetu.” Nia njema ni roho ya mafanikio. Aliye na nia ya dhati ya kufanikiwa na anajua kuwa ana nia ya kufanikiwa ‘Atafanikiwa’. Siku moja bondia Floyd Mayweather alionekana akifanya mazoezi saa 11 alfajiri na mwandishi wa habari alimuuliza: “Ni jambo gani linakufanya uzidi kufanikiwa?” Mayweather alimjibu: “Wakati wenzangu wamelala mimi ninafanya mazoezi, wakiamka mimi ninafanya mazoezi, wakirudi kulala mimi ninafanya mazoezi.”
Hii ndiyo siri ya mafanikio ya bondia Floyd Mayweather. Hata wewe leo unaweza ukaitumia kanuni yamafanikio ya bondia Mayweather na ukafanikiwa. Mwandishi wa kitabu cha I Can, I Must, I Will, Dk. Reginald Mengi anasema: “Nimekulia kwenye umaskini, lakini siku zote nimekuwa nikiona umaskini kama changamoto. Habari njema ni kwamba unaweza kuushinda umaskini kama uko tayari kulipa gharama. Gharama hiyo ni kufanya kazi kwa bidii.”
Mwanasayansi wa Ufaransa, Louis Pasteur, alipoambiwa na marafiki zake kuwa anafanya kazi kupita kiasi alisema: “Nahisi kama ninaiba kama nikiruhusu siku ipite bila kufanya kazi.”
Tumeumbwa kufanikiwa. Tumeumbwa kushinda. Tazama huu ushuhuda wa John Paul DeJoria. John Paul DeJoria akiwa katika shule ya sekondari ya juu (kidato cha tano na sita) mwalimu wake alimwambia: “Wewe John hauwezi kufika popote kwa sababu hauna akili za kimasomo.”
DeJeforia hakukatishwa tamaa na maneno ya mwalimu wake. Aliendelea kuhangaika kutafuta maisha yake. DeJeforia alioa, lakini kuna wakati maisha yalimwendea kombo. Akayumba sana kiuchumi. Mke wake alipoona maisha yamekuwa magumu alimkimbia na kumwachia mtoto mmoja wa miaka miwili.
DeJeforia alianza kuokota chupa tupu zilizotumika na kuziuza ili amtunze mwanae. Siku zote alimwambia mwanae: “Tutatoka kimaisha pamoja.”
DeJeforia alianza pia kufanya biashara ya kuuza magazeti mlango mmoja baada ya mwingine. Ilifika hatua akaamua kuanzisha kampuni. Watu walimbeza na wakamwambia kwamba hana elimu yoyote ya biashara na hana pesa za kutosha za kuendesha biashara. DeJeforia aliendelea kukomaa.
Mwaka 2015, jarida maarufu la Forbes lilimtaja kama tajiri namba 234 kati ya matajiri 400 kutoka Marekani akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.8 za Marekani. Dejeforia pia ni mwanzilishi wa bidhaa za nywele zinazojulikana kama Paul Mitchel. Usikate tamaa katika maisha. Pambana.