Haben Girm ni mwanamke aliyezaliwa akiwa haoni wala kusikia. Haben Girm alizaliwa katika familia maskini sana.
Haben alipozaliwa akiwa haoni wala kusikia watu walimshauri mama yake amtupe kichakani. Mama yake alikataa kata kata. Mama yake alisema: “Siwezi kumtupa mtoto wangu kichakani kisa ni kipofu.”
Haben alikulia katika mazingira magumu sana. Kila mtu, wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki walimtazama Haben kama hasara katika familia yake. Kitu kimoja ambacho watu wengi walikuwa hawakifahamu ni kuwa Haben alikuwa na ndoto ya kuwa mwanasheria.
Siku moja Haben alimwambia kaka yake: “Nitakuwa mwanasheria na hiyo ndiyo ndoto yangu.” Kwa haraka kaka yake alimjibu: “Hapana. Hauwezi kuwa mwanasheria. Wewe ni kiziwi na kipofu”. Haben alimjibu kaka yake kwa kusema: “Udhaifu wangu hauwezi kunizuia kuwa mwanasheria.”
Ndoto ya Haben kuwa mwanasheria ilitimia. Mwaka 2005 Haben alitunukiwa shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani. Lisilowezekana linawezekana.
Watu unaowafahamu wanaweza wakawa ndio maadui wako wa kwanza katika maisha yako. Ndoto ya Haben kuwa mwanasheria ilitaka kuzimwa na kaka yake. Kamwe katika maisha, usikubali watu wautumie udhaifu wako kama kigezo cha kuizima ndoto yako. Usiruhusu mazingira magumu ya sasa yaue ndoto yako ya kesho. Kila ndoto kubwa ina mashambulizi makubwa. Ilinde sana ndoto yako.
Watu wote huota ndoto. Kuna ambao wanaota ndoto wakiwa wamesinzia lakini kuna ambao wanaota ndoto wakiwa macho. Ndoto ni maono. Ndoto ni kesho yako.
Katika karne ya 19 ndugu wawili walikuwa na wazo ambalo liligeuka kuwa mbegu ya ukweli. Ndugu hao ni Orvile Wright na Wilbur Wright wa Marekani. Wakiwa vijana mwaka 1896 walikuwa ni mafundi wa kutengeneza baiskeli. Mwaka 1899 walifanya jaribio la kurusha tiara. Wakapata wazo la kutengeneza chombo kinachoweza kuruka angani. Walifikiria kutengeneza meli ya angani. Walichekwa sana.
Wazo la kurusha ndege angani walianza nalo mwaka 1899 kwa kufikiria namna ambavyo rubani anaweza kurusha ndege angani na asianguke kama vile mtu anavyoweza kuendesha baiskeli na asianguke.
Gazeti la New York Times la nchini Marekani la mwaka 1903 liliripoti kwa kusema: “Wanasayansi wasipoteze muda na pesa kwa majaribio ya chombo cha angani.” Wiki iliyofuata ndugu hao walifanikiwa kurusha ndege angani.
Ajabu ni kwamba, ndugu hawa hawakuwa na shahada ya chuo kikuu chochote. Hii ndiyo nguvu ya kung’ang’ania maono. Katika safari ya mafanikio, njiani utakutana na watu ambao watakucheka kama Orvile Wright na Wilbur Wright walivyochekwa.
Wengine watakuona kama mwendawazimu. Usiogope kuchekwa. Endelea kuchapa kazi. Endelea kutimiza malengo uliyojiwekea katika maisha yako. Endelea kuitengeneza kesho yako.
Mafanikio ya kweli nyuma yake na mbele yake kuna maadui unaowafahamu na usiowafahamu. Jijaze ujasiri wa kupambana na maadui hawa. Usiwakimbie. Kabiliana nao. Watu wengi wameshindwa kutimiza ndoto zao, kwa sababu wengine walikatishwa tamaa na watu na wao wakakubali kukata tamaa. Nguvu uliyonayo ni kubwa kuliko nguvu inayotoka kwa maadui wako. Unapokubali kukata tamaa, unakuwa umekubali kuua nguvu kubwa ya maono iliyoko ndani yako.
Naomba kukufundisha jambo hapa. Haijalishi unafanya kazi au hufanyi kazi, ni lazima watu watakusema tu. Bila kujali wewe ni mwema kiasi gani, lazima kutakuwa na watu ambao watakushambulia. Bila kujali wewe ni mkimya kiasi gani, lazima utakutana na watu wa kukutungia maneno.
Kazi ya mdomo ni kusema. Usiogope kusemwa. Kwa mfano: Mtu akiwa mkarimu kuna watu watakaojitokeza na kusema: “Anajitangaza.” Asipokuwa mkarimu watasema: “Ana gundi vidoleni.” Mtu akitoa hotuba fupi sana, kuna watu watajitokeza na kusema: “‘Hakujiandaa.” Akitoa hotuba ndefu watasema: “Hajui kutunza muda.”
Akiwa mtoto mchanga watasema ni ‘Malaika’. Akiwa mtu mzima watasema: “Achana na yule shetani.” Akiwa mcha Mungu watasema: “Ni Mkatoliki zaidi ya Papa.” Asipokuwa mcha Mungu wanasema: “Shetani amemweka mfukoni.” Akiaga dunia katika umri mdogo watasema: “Angefanya mengi mazuri.” Akifikia umri wa uzee watasema: “Miaka yake aliiharibu tu bila kufanya chochote.”
Ndoto yako isiongozwe na maneno ya watu. Acha wakuseme wawezavyo lakini wewe pambana kutimiza ndoto yako. Acha leo wakuone kichaa ili kesho wakushangae.