Mataifa makubwa ya magahribi yametangaza orodha mpya ya vikwazo dhidi ya Iran wanayoituhumu kuipatia Urusi makombora ya masafa marefu ambayo inaaminika Moscow itayatumia dhidi ya Ukraine.
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimetangaza kuifuta mikataba yote ya sekta ya anga na jamhuri hiyo ya Kiislamu na kuliwekea vikwazo shirika la ndege la Iran Air. Mataifa hayo matatu yamesema hatua hizo zinachukuliwa kujibu uamuzi wa Iran wa kupuuza onyo la kutoipatia Urusi silaha.
Marekani kwa upande wake nayo imetangaza vikwazo vya pamoja na Uingereza dhidi ya watu inaowatuhumu kuratibu mipango ya kupeleka makombora ya Iran nchini Urusi.
Hata hivyo Iran yenyewe ilisema madai yanayotolewa na nchi za magharibi ni “njama chafu” ya “kuwafumba macho na kuwapumbaza walimwengu” juu ya shehena ya silaha ambazo mataifa hayo zinaipatia Israel iliyo hasimu mkubwa wa Iran.