Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) huenda ikaanzisha upya mchakato wa kuongeza ama kutoongeza muda wa leseni kwa miezi 55, baada ya mchakato wa mwanzo baada ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kuomba leseni hiyo kusitishwa, huku aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, akisimamishwa kazi.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Juni 11, mwaka huu. Kauli ya Waziri Mkuu, ilikuja punde tu baada ya Ewura kusitisha tangazo lao la kukusanya maoni kutoka kwa wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuongeza muda wa leseni ama kufuta.

Juni 6, mwaka huu, Ewura ilitoa tangazo la kupokea maombi ya IPTL kuongeza muda wa leseni na kulifuta siku tano baadaye.
“Ewura imepokea maombi ya IPTL kuongeza muda wa leseni kwa miezi 55, kuanzia Julai 2017 hadi Julai 2022. Naomba ieleweke kwamba leseni ya kuzalisha umeme hutolewa na Ewura kulingana na pamoja mambo mengine mkataba wa kuuziana umeme yaani Power Purchase Agreement (PPA) kati ya Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (Tanesco) na wazalishaji umeme,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Ewura.
Mkataba wa mauziano ya umeme baina ya IPTL na Tanesco ilisainiwa mwaka 1995 kwa miaka 20 (from Commercial Operation Date (COD). Leseni ambayo imekuwa ikitumiwa na IPTL ni ile iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka 21.

“Maombi yaliyoletwa na IPTL ni kuongeza muda wa leseni uweze kuendana na mkataba wa mauziano ya umeme. Maombi ya yaliyoko Ewura kwa sasa sio ya kuidhinisha mkataba wa mauziano ya umeme, bali kuhakikisha uzalishaji wa umeme ambao unafanyika na IPTL unafanyika kisheria kwa kupata leseni kutoka Ewura.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Umeme na Sheria ya Ewura, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Tanesco, ni wadau ambao wameombwa kutoa maoni yao kuhusu maombi haya. Wananchi pia wameomba maoni yao kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya EWURA na kifungu cha 8 cha Sheria ya Umeme,” inasomeka taarifa kutoka Ewura.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kwamba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, ameishauri Wizara ya Nishati na Madini, kurejesha jambo hilo Ewura, ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Katika ushauri huo, Masaju amenukuu vifungu 5 na 8 vya sheria ya umeme, (sura 131) (The Electricity Act, Cap 131), huku akisisitiza ili IPTL waweze kuendelea kuzalisha na kuwauzia Tanesco umeme, wanapaswa kuwa wamepata leseni ya kuzalisha umeme kutoka Ewura.

JAMHURI limeona waraka wa ushauri huo ambao umelenga kusaidia kutorudia makosa. Amesisitiza “mkataba wa kuuziana umeme (Power Purchase Agreement) kati ya Tanesco na IPTL unawataka Tanesco kutekeleza jukumu la kuhakikisha kwamba wanawezesha IPTL kupata vibali, ridhaa na leseni kwa ajili ya kuzalisha umeme,”
Katika hatua nyingine, JAMHURI limefahamishwa kwamba, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe, ameshatoa maelezo kwa Ewura. Japo haijafahamika mchakato huo utaanza rasmi lini.
Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano ya umeme baina ya IPTL na Tanesco ibara zake 3,4na 5 Tanesco wana jukumu la kulipia umeme wanaouziwa na kutumia (energy charge) na kulipia ukodishaji wa mtambo wa IPTL (Capacity Charge) hata kama Tanesco hawatakuwa wametumia umeme wowote kutoka IPTL.
Serikali iliingia mkataba (Implementation Agreement) na IPTL kuhusu utekelezaji wa mkataba kati ya Tanesco na IPTL ambapo katika ibara za 6 na 7, Serikali ilibeba jukumu kuhakikisha kwamba IPTL wanapata vibali, ridhaa na leseni na kuwaunga mkono IPTL.

Kwa mujibu wa mkataba wa kuuziana umeme kati ya Tanesco na IPTL na mkataba (Implementation Agreement) kati ya Serikali na IPTL , Tanesco na Serikali, pamoja na mengineyo wanalo jukumu la kuwawezesha IPTL kupata vibali, ridhaa na leseni kwa ajili ya uendeshaji wa mradi/mtambo wao wa kuzalisha umeme katika kipindi chote cha uhai wa mikataba hiyo.
Ili EWURA iliiweze kutoa leseni ya uzalishaji umeme kwa IPTL inapaswa iwe imezingatia vigezo na masharti kadhaa kama yanavyotajwa katika kifungu cha 9 cha sheria (The Energy and Water Utilities Regulatory Act) (Cap 414), Kwa mfano, kwa mujibu wa kifungu 9(2), mambo ambayo EWURA inapaswa kuyazingatia kabla ya kuwapatia IPTL leseni ni pamoja na:
(f) the legal, technical, economic and financial capacity to conduct the proposed activities. (g) the cost of the activities and the effect on electricity prices to customers; (h) any representations and objections to the proposed activities made by the public; (i) Other public interests which may be affected by the proposed activities.

Sehemu ya waraka wa ushauri kwa Wizara ya Nishati na Madini, kutoka kwa Mwanasheria Mkuu, Masaju, unashauri EWURA kuzingatia ipasavyo vigezo/masharti katika kifungu cha 9 cha sheria hiyo.
“Ewura wako katika nafasi nzuri ya kuamua kuwapatia au kutokuwapatia IPTL leseni ya kuzalisha umeme. Kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha sheria hiyo, EWURA wanayo mamlaka kusitisha leseni kwa muda (suspend), kurekebisha leseni (vary) au kuifuta (revoke) leseni,” inasomeka sehemu ya ushauri wa Mwanasheria Mkuu.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba IPTL wamefunguliwa kesi kadhaa ndani na nje ya nchi kupinga umiliki wao wa mtambo husika. Serikali na TANESCO nao wameshitakiwa katika International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID) na Standard Chartered Bank (Hong Kong) ltd wakidai kwamba Serikali imetaifisha mtambo wao na kwamba wao ndio wamiliki halali wa mtambo huo; wanataka walipwe mapato yote na riba inayotokana na matumizi ya mitambo hiyo.

Mwanasheria Mkuu, ameonesha namna ambavyo IPTL tangu mikataba kati ya Tanesco na IPTL na kati ya Serikali na IPTL iliyoingiwa mwaka 1995, IPTL walikuwa na fursa ya kutumia pia gesi ili wazalishe umeme nafuu lakini hawajawahi kuchukua hatua za kugeuza mtambo huo kutumia gesi ili kuleta unafuu kwa Tanesco na watumiaji wa umeme.
“Kwa hiyo Ewura na Tanesco wako katika hali nzuri zaidi ya kushauri na kuamua kama katika mazingira yaliyopo IPTL waendelee kupewa leseni kwa kuzingatia sheria ya umeme, Sura 131.
“Kabla ya EWURA kufanya uamuzi kuhusiana na leseni ya kuzalisha umeme inayoombwa na IPTL , Tanesco wanapaswa kujiridhisha kama bado wanahitaji umeme unaozalishwa na IPTL kwa sasa na kuishauri EWURA na serikali ipasavyo,” inasomeka sehemu ya waraka wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Huku akisisitiza kwamba, endapo Tanesco bado wanalazimika kutumia umeme unaozalishwa na IPTL, itabidi serikali na Tanesco kujadiliana na IPTL viwango vipya vya bei ya umeme wanaoutumia kutoka IPTL na kuutumia ili kupata unafuu kama masharti ya sheria ya Ewura yanavyoelekeza katika vifungu vya 6 na 9 vya sheria ya Ewura sura 414.
Amesema mikataba iliyopo baina ya Tanesco na IPTL na Serikali inaruhusu marekebisho katika mikataba husika endapo washiriki wa mikataba hiyo wamekubaliana.
Mwanasheria Mkuu, amesisitiza kuwa umiliki wa mtambo wa IPTL bado una utata na umiliki huo unabishaniwa Mahakamani Tanzania na ICSID, ameishauri Tanesco kufikiria kusitisha kwa muda malipo ya kila mwezi ya kodi ya mtambo huo hadi hapo mashauri husika yaliyopo mahakamani yatakapo kuwa yamekamilika na mmiliki halali kujulikana.
Ameshauri kwamba,Tanesco na Serikali inapaswa kujiridhisha kama tangu IPTL ianze kulipwa capacity charge ikiwemo na fedha za Escrow Account zilizochukuliwa na watu wanaodai kuwa wamiliki wa mtambo wa IPTL, bado tu haijaweza kurejesha gharama za uwekezaji wake katika mradi wa mtambo huo wa IPTL na kuchukua hatua ipasavyo.
“Kama Tanesco bado inauhitaji mtambo wa IPTL kwa ajili ya uzalishaji umeme, itabidi mtambo huo uwe pia na uwezo wa kuzalisha umeme kwa kutumia njia ya kutumia gesi kama ilivyokwisha kubaliwa na wanaodai kuwa wanahisa wa IPTL.

“Kuzalisha umeme bila kuwa na leseni ni kosa la jinai dhidi ya kifungu cha 8 (1) (5) cha Sheria ya Umeme sura 131,” amesema Masaju.
Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, Dk. Alexander Kyaruzi, amesema IPTL hawaiuzii umeme Tanesco kwa sasa kwa sababu leseni yao imekwisha tangu Julai 15, mwaka huu.
“Nani amekwambia wanauza umeme Tanesco, hawauzi kwa sababu hawana leseni ya kuzalisha umeme, kama huna leseni huwezi kuuza umeme, wameacha kuuza umeme tangu leseni yao ilipoisha Julai 15, mwaka huu,”amesema Dk. Kyaruzi

Alipoulizwa kama baada ya leseni ya IPTL kwisha, umeme unaozalishwa kwa sasa utatosheleza kwa mahitaji ya nchi, amesema hawezi kuendelea kujibu maswali hayo kwa sababu yanawahusu watendaji ndani ya Tanesco.
“Hayo maswali ni mambo ya kiutendaji, nakuomba mtafute Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Dk. Tito Mwinuka atakujibu mimi najibu mambo ya kisera,”amesema.
IPTL ilikuwa na mkataba wa kuiuzia umeme Tanesco katika kipindi cha miaka 21 iliyopita. Katika kipindi hicho cha mkataba na Tanesco, ilianza kufanya biashara na Tanesco miezi 55, kipindi ambacho kilihusisha kufanya uwekezaji.
Wakati IPTL inakuja mezani kuomba leseni kwa Wakala wa Udhibiti wa Nishati na Maji, (Ewura), tayari kumekuwepo na manung’uniko kutoka kwa wananchi kuhusu namna IPTL ilivyoshiriki kuchota mabilioni ya fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), tayari kimejitokeza hadharani kueleza azma yake ya kupinga kampuni ya kufua umeme ya IPTL kupewa leseni na Ewura ili iweze kufanya biashara na Tanesco.
LHRC imetangaza kuweka kusudio la kupinga IPTL kupewa leseni ya kuendelea kuliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku wakihoji usafi na makandokando dhidi ya kampuni hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, amenukuliwa akisema wanamalizia kuandaa pingamizi lao la kisheria ambalo wataliwasilisha Ewura.
Henga amesema IPTL haina sifa tena ya kuendelea kuuza umeme nchini, hasa baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Suala hili tumekuwa tukilifuatilia tangu zamani na tuna ushahidi kwamba IPTL haipaswi kupata sabuni hii kwa kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Bunge kuhusu kampuni hiyo bado hayajatekelezwa.
“Tutapeleka maoni yetu Ewura, tutawaandikia jinsi tunavyoona, lakini kwa hali ya kawaida kwa IPTL, Ewura hawakuhitaji hata kuomba maoni ya wananchi katika kufanya uamuzi kwa kuwa sifa mojawapo ya kupatiwa leseni ni uadilifu wa muhusika,” amesema Henga.
Amesema moja ya mapendekezo yaliyotolewa na iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, hayakutekelezwa, ikiwamo kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), kufanya uchunguzi juu ya umiliki na uwepo wa rushwa katika utendaji kazi wa IPTL na wabia wake.

Maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
1. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalum wa Malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja naTakukuru imeonesha kwamba kwamba Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (‘TANESCO’) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing (‘VIP’);

Kwa kuwa, kwa sababu ya kuhusika kwa watu hao na miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Escrow imeliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha za umma zinazotokana na kutokulipwa kwa kodi mbali mbali za Serikali na kushindwa kwa Tanesco kukokotoa upya kiwango cha malipo ya gharama za uwekezaji (‘capacity charges’) wa IPTL;
Kwa kuwa, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi na maafisa wa serikali kama vile Mawaziri, Majaji, Wabunge, Wenyeviti wa Kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.

Na kwa kuwa, vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria makosa mbali mbali ya jinai kama vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;
2. Kwa kuwa, vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;
3. Kwa kuwa, katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco;
Na kwa kuwa, Bunge na/au Kamati zake za Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge;

4. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
Kwa kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’) imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji;
Kwa kuwa, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji;
Na kwa kuwa, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania;

5. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP katika benki hiyo;
Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba akaunti za PAP katika Stanbic Bank Tanzania Ltd. zimekwishafungwa baada ya fedha zote zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kumalizika na Akaunti ya ya VIP katika Mkombozi Commercial Bank imebakiza kiasi fulani cha fedha;

Na kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba kuna uwezekano fedha zilizotolewa kutoka kwenye akaunti za PAP na VIP zilipelekwa katika benki nyingine;
Na kwa kuwa, vitendo vya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwenye Akaunti ya Escrow ni vitendo vya jinai kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of money laundering concern);
6. Kwa kuwa, vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, hujuma ya uchumi na ufisadi vimeongezeka, kushamiri na kushirikisha viongozi wa kisiasa na maafisa wa serikali pamoja na wafanya biashara wakubwa;
Kwa kuwa, kwa mujibu wa sheria iliyoiunda, TAKUKURU inashughulikia vitendo vya aina zote za rushwa zikiwemo rushwa ndogo ndogo (petty corruption) na rushwa kubwa na ufisadi (grand corruption) na matumizi mabaya ya madaraka;

Na kwa kuwa, kwa sababu ya majukumu yake mapana kisheria, Takukuru inaelekea kuelemewa katika vita ya kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa letu kiuchumi, kijamii na kisiasa;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa;
7. Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo Tanesco imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;
Kwa kuwa, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba Tanesco itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
8. Kwa kuwa, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na makampuni binafsi ya kufua umeme imeisababishia Tanesco hasara ya mabilioni ya fedha na hivyo kutishia uhai wake wa kifedha;
Kwa kuwa, Bunge lilikwishaazimia kwamba serikali iwasilishe mikataba husika Bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali;
Na kwa kuwa, Serikali haijatekeleza Azimio hilo la Bunge hadi sasa;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.