Wakati uongozi wa Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club ya jijini Dar es Salaam unaingia madarakani Agosti 2009, ulitoa ahadi nyingi ambazo wanachama waliwaamini na kujenga imani nao.
Viongozi waliochaguliwa kuingia madarakani kwa miaka minne ni Mwenyekiti Ismail Aden Rage, Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye sasa amejiuzulu, na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Francis Waya, Salehe Pamba, Joseph Itang’are, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ na Swed Nkwabi.
Ahadi zilizokuwa kama silaha ya uongozi huo kupata ridhaa ya wanachama ni ujenzi wa uwanja utakaomilikiwa na klabu, ujenzi wa ghorofa katika makao makuu ya klabu pamoja na kuwa na kikosi bora ambacho kitavunja rekodi ya michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Africa (CAF) na ile ya Kagame.
Haikuchukua muda mrefu uongozi huo ulileta wakandarasi kutoka Uturuki, kwa ajili ya kufanya usanifu kabla ya kuanza ujenzi huo na ramani ya uwanja ikatoka na uwanja huo ungeitwa Simba Arena.
Baada ya muda ikagundulika kuwa Simba haikuwa na eneo la kujenga uwanja huko Bunju kwa vile haikumaliza deni pamoja na hati ya kutoka Wizara ya Ardhi.
Wanachama waliamini kuwa kauli ya Rage kuwa uwanja utakuwa unaingia watu 30,000 pamoja na maduka na hotel ya kisasa, kungeweza kuiondoa Simba katika hali ya umasikini.
Lakini cha kushangaza; hali ya Simba sasa ni aibu. Klabu haina fedha, uongozi umekuwa haulewani, aliyekuwa kocha wa timu hiyo Circovic Milovan alikuwa anadai shilingi milioni 40 kabla ya kulipwa na mfadhili wa timu hiyo, Rahma Al Kharous maarufu kama Malkia wa Nyuki.
Hali hiyo imesababisha Simba kufanya vibaya katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 5-0, bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na 4-0 katika Uwanja wa Liboro nchini Angola.
Kitendo cha Malikia wa Nyuki kuingia katika Simba na kupewa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, ndiyo kama viongozi hao wametua mzigo kwa mama huyo.
Kitendo hicho kimefanya uongozi kutangaza shida za klabu kwa malkia huyo ambaye kwa sasa anaabudiwa na uongozi huo. Hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari vilimwonesha Mwenyekiti wa Simba, Rage hali akimfungulia mlango malkia huyo akifananishwa na ‘Bodigadi’ wake.
Mama huyo alilipa deni la Sh milioni 11 walilokuwa wanadaiwa na hoteli moja jijini Arusha walikoweka kambi kabla ya kucheza na Liboro.
Kutokana na ukata huo na uongozi wa Simba kutoeleweka, kumesababisha baadhi ya wachezaji nyota wa klabu hiyo kuondolewa katika timu kwa kile kilichoitwa utovu wa nidhamu, kumbe walikuwa wakidai malimbikizo ya fedha zao.
Wachezaji wa kikosi cha kwanza waliosimamishwa ni Haruna Moshi (Boban), Juma Nyosso, Amir Maftaha, Abdalah Juma, Konambili Keita, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Paul Ngalema.
Sasa swali la kujiuliza ni je, tambo za Rage za kujenga Simba Arena, ghorofa la kisasa na kuifanya timu hiyo kama Zamalek zimeishia wapi?