Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuongeza siku mbili zaidi za zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Dar es Salaam ambapo sasa zoezi hilo litamalizika Machi 25, 2025.

Hatua hiyo imetangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Machi 23, 2025 kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioanza Machi 17 na uliotarajiwa kumalizika leo Machi 23 mwaka huu.

“Hivyo basi, napenda kuwatangazia wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa, Tume imeongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari kwa tarehe 24 na 25 Machi, 2025 na zoezi litakamilika tarehe 25 Machi, 2025 saa 12:00 jioni,” amesema Jaji Mwambegele.

Aidha, Jaji Mwambegele amefafanua kuwa baada ya siku hizo mbili Tume haitaongeza muda zaidi.

Amesema wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao tangu siku ya kwanza ya zoezi hilo Machi 17, 2025 ambapo Tume iliongeza mashine za BVR pamoja na watumishi.

“Kutokana na mwitikio mkubwa Tume ilichukua hatua za kuongeza mashine za BVR kits pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi na hatua hii imewezesha zoezi kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote,” amesema Jaji Mwambegele.

Alisema baada ya kuongeza mashine za BVR na watumishi katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa na changamoto ya watu wengi iliwezesha kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa misongamano kwenye baadhi ya maeneo.

Jaji Mwambegele amesema Tume inawapongeza wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza, kuboresha au kuhamisha taarifa zao na kupata kadi mpya kwa wale ambao kadi zao zimepotea au zimeharibika.

Katika hatua nyingine Jaji Mwambegele alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa zoezi hilo halihusishi ubadilishaji wa kadi zilizotolewa tangu 2015.

“Napenda kuwakumbusha kuwa zoezi hili halihusishi ubadilishaji wa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Jaji Mwambegele.

Ameongeza “Hivyo, wananchi wote ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea, hawajahama kutoka kata au halmashauri hawahusiki na zoezi hili”.

Aidha, Jaji Mwambegele ameonya kuwa kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria na anayefanya hivyo akitiwa hatiani anaweza kufungwa jela, kutozwa faini au vyote kwa pamoja. Kosa hilo ni kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024.

“Mtu yeyote akithibitika amejiandikisha zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani,” amesema.

Jaji Mwambegele ametoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Tume na kuhakikisha kuwa wanaokwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao vituoni ni wale tu ambao wanastahili kufanya hivyo.

Tume imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 30. Kwa mujibu wa ratiba, ambapo sasa uboreshaji upo katika mzunguko wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari kwa awamu ya kwanza. Mzunguko huu unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee.