Serikali ya Tanzania imekubali ombi la Serikali ya India, la kutaka kuwekeza katika sekta ya nishati na madini nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (pichani kulia), amethibitisha hatua hiyo katika mkutano na ujumbe wa India uliofanyika Dar es Salaam, hivi karibuni.
Ujumbe wa India umeongozwa na Waziri wa Chuma, Beni Prasad Verma, aliyefuatana na Katibu wa wizara hiyo, Dileep Singh Chaudhary, miongoni mwa viongozi wengine.
Waziri Verma amebainisha kuwa Serikali ya India inahitaji kuwekeza katika uchimbaji wa madini aina ya chuma, dhahabu na almasi, chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
Miongoni mwa masharti yaliyotajwa na Waziri Muhongo ni pamoja na Serikali ya Tanzania kutoza kodi na kumiliki sehemu ya hisa za uwekezaji huo.
“Sisi [Tanzania] tumekubali tuna madini mengi, waje kuwekeza, lakini siku hizi tumeacha kutegemea kodi pekee bali tunahitaji na hisa,” amesema Profesa Muhongo.
Pia Waziri Muhongo ameutahadharisha ujumbe huo wa India, kuwa Tanzania inataka uwekezaji wa wazi usioruhusu mwanya wa vitendo vya rushwa na ujanjaujanja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, na Katibu wa Wizara ya Chuma wa India, Chaudhary, wamesaini makubaliano ya uwekezaji huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya India, kuangalia uwezekano wa kuwapatia vijana kadhaa wa Kitanzania ufadhili wa masomo nchini humo kila mwaka.