Wakati Afrika ikijiandaa na mkutano wake jijini Kigali, Rwanda, viongozi mbalimbali wa dunia wametembea nchi mbalimbali wakitafuta kupenyeza ajenda zao.

Viongozi wakubwa waliotembelea Afrika ni pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na yule wa India, Narendra Modi. Ziara yao barani Afrika haikuwa bahati mbaya.

Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Roma Peter, anasema ziara ya Modi nchini Tanzania ilikuwa muhimu. Anasema Waziri Mkuu wa India nchini Tanzania alikuwa na ajenda kuu nne. Ya kwanza ni kuendelea kushirikiana na India kwenye sekta ya maji.

“Itakumbukwa India imeendelea kuwa mshirika wa kutumainiwa wa Tanzania kwenye sekta hiyo… wengi bado tunayo kumbukumbu ya mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria pamoja na unaoendelea kukamilika katika Jiji la Dar es Salaam,” anasema Roma.

Anasema ajenda nyingine ilikuwa ni Tanzania kujifunza kutoka kwa India kuhusu muundo wao wa kutumia viwanda vidogo na vya kati katika kuongeza ajira na mauzo nje ya nchi. Itakumbukwa, siri ya India ni viwanda vidogo na wana sera mahsusi ya kuendeleza viwanda vidogo.

“India imekuwa na sera mahsusi ya kuweka asilimia fulani ya mikopo kwa mabenki kukopesha kwa ajili ya ukuzaji wa sekta hiyo, na wameweza kufanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha,” anasema Roma.

India inayo sera ya kuweka asilimia kadhaa ya ununuzi kwenye Serikali Kuu na serikali za majimbo kuyawezesha yawe kwenye viwanda vidogo na vya kati. Kupitia India, Serikali imekubaliana na Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO) ishirikiane na Shirika la Taifa la Viwanda Vidogo vidogo nchini India (NSIC) ili  taasisi hizo zishirikiane kwa karibu.

Anasema kulikuwa na makubaliano kwamba kwa kuanzia, India itatoa fungu kwa ajili ya kuanzisha atamizi (incubators) ambazo zimelenga kuanzishwa kila mkoa kwa lengo la kuhamasisha ubunifu na kujiajiri.

Katika harakati za kuhakikisha kwamba Tanzania inanufaika na ziara iliyofanywa na Waziri Mkuu Narendra Modi, hoja ya kushirikiana katika sekta ya uwekezaji ilikuwa muhimu kwa pande zote mbili. Waziri Mkuu Modi aliambatana na wafanyibiashara 50 ambao walifanya mazungumzo na wafanyabiashara wenzao.

Roma anasema Tanzania pia inaweza kunufaika na ushirikiano katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Kuna kila dalili kwamba Tanzania itanufaika na mafunzo ya TEHAMA kutoka nchini India.

“Lengo letu ni vijana wetu wajengewe uwezo wa kuweza kutengeneza programu wenyewe ili kutupunguzia gharama za kununua programu,” anasema.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya diplomasia ya kimataifa, Elius Justus, anasema ilitarajiwa ujio wa Waziri Mkuu wa India uwe na ajenda mahsusi, kwani Tanzania bado inao ushawishi katika nchi za Maziwa Makuu.

“India imekuwa inapambana sana huko duniani kuhakikisha inaingia kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Inahitaji uungwaji mkono na nchi za Afrika. Hata ukiangalia Narendra Modi amekwenda katika nchi ambazo anaona zinaweza kusukuma ajenda ya India,” anasema Elius.

Anasema Modi anatafuta suluhu ya tatizo la kisiasa nchini India ambapo yuko kwenye wakati mgumu kutokana na bei ya mazao jamii ya kunde, ambacho ni chakula kikuu cha watu wengi wa India kuendelea kuadimika huko.

“Bahati mbaya anayesafirisha bidhaa hizo amekuwa anawauzia kwa bei mbaya. Amekuwa ananunua kwa bei nafuu hapa na kuwauzia kwa bei ya kuruka. Tanzania inaweza kuwa suluhu kwao kwani wanahitaji takribani tani milioni 6 kwa mwaka,” anasema Elius.

Kuhusu ajenda yao ya kuomba kuungwa mkono na Afrika kupata nafasi ya India kuwa Mjumbe wa Kudumu kwenye Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kimsingi nchi nyingi za Afrika wanakubaliana na India kwa sharti la nchi hiyo pia kuunga mkono Afrika kwenye mchakato wa kupata uwakilishi katika Baraza hilo.

“Ndiyo maana amekuja katika kipindi ambacho AU itaelekea Kigali ambapo pamoja mambo mengine kutakuwa na masuala ya mabadiliko katika Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,” anasema.

Anasema ajenda nyingine ilikuwa kujaribu kuwadhihirishia wapinzani wake kwamba misaada wanayotoa kwa Afrika inaleta tofauti kwa wanufaika. Amekuwa akikosolewa kwamba anatoa misaada, lakini Wahindi hawaoni faida yake ikiwa ni pamoja na kupata zabuni.

Mchambuzi mwingine, John Alfred, anasema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilibidi aje barani Afrika, maana hakuwahi kuja Afrika kama Waziri Mkuu, kwa hiyo si jambo la busara kiongozi wa taifa kubwa kama hilo kutoonesha kiu yake ya kufanya biashara na upande pekee wa dunia ambao una rasilimali nyingi na fursa za kutosha.

Anasema jambo jingine ambalo lilimleta Waziri Mkuu Netanyahu ni pamoja na ajenda ya kisiasa. Israel inatafuta nchi ya kuwapeleka wahamiaji, kwani wameshasaini mikataba na Rwanda na Uganda wahamiaji ilionao wahamishiwe nchini humo kwa hiyari.

“Baada ya kusaini, hawakuleta pesa. Inaonekana Israel hawakuleta pesa, kwa hiyo ilikuwa ni fursa ya kuja kuwahakikishia msimamo wao kuhusiana na mpango husika,” anasema Alfred.

Anasema Israel walikuwa na jambo kuhusu masuala ya ugaidi, Afrika Mashariki ni moja ya maeneo yanayochukuliwa kama mazalia ya ugaid kwani kuna vijana wengi wa Afrika Mashariki kwenye makundi ya kigaidi na baadhi wana vyeo kwenye makundi hayo.

“Kuna vijana wengi wako Somalia, wengine Yemen na Syria… hawa ipo siku watarudi nyumbani na kwa uhakika wana taasisi zinazowarubuni vijana kujiunga na makundi hayo. Israel lazima iguswe na mwenendo huo,” anasema Alfred.

Anasema ni dhahiri kwamba Israel ingependa kuungana na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kupunguza athari za ugaidi zisiendelee. Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki yalitokea mauaji ya sheikh pale Kigali, mauaji kama hayo yamekuwa yakitokea Mombasa.