Wiki iliyopita nilieza kwa sehemu namna wachambuzi na wahubiri wengi wanavyoeleza habari za shetani (Freemason, Illuminat, n.k) katika mitazamo hasi kiasi ambacho hofu imetanda miongoni mwa jamii. Ilivyo sasa ni kuwa watu wengi wamebaki njia panda, hawajui cha kufanya baada ya kugundua kuwa kila wanachokigusa ama kinachowazunguka kimebandikwa hatimiliki ya Freemason ama jumuiya nyingine za waabudu shetani.

‘Ok’ huyu msomaji, muumini ama msikilizaji akishafahamu kuwa fedha anazotumia zinatawaliwa na shetani unamsaidiaje kukabiliana na hilo? Unadhani atakua na mtazamo gani kuhusu fedha? Sana sana ataamini kua utajiri ni Freemason! Akiamini hivyo utakua umemsaidia ama umempoteza?

Mathalan, kuna watu mpaka leo wameaminishwa kuwa alama “nyoka aliyezunguka mti” kwenye noti ya shilingi mia tano ni uwakilishi wa Freemason na nguvu za shetani. Hiki ni kitu cha kuchekesha sana, kwanza yule anaedhaniwa kuwa ni ‘nyoka’ kiuhalisia sio nyoka! Ngoja nikueleze chimbuko la alama hii.

Kule nchi za mashariki ya kati karne nyingi zilizopita walikuwa na tatizo la kushambuliwa na minyoo. Aina ya minyoo iliyokuwa ikiwashambulia ilikua ni mikubwa na ilikua inachomoza na kutoka nje ya mwili kupitia ngozi. Mtu akikumbwa na minyoo hii na ikaanza kuchomoza katika ngozi yake; walikuwa wakiivuta kwa kuiviringisha kwenye kijiti mpaka mnyoo mzima utoke nje.

Baadae wakaja kugundua dawa ya minyoo hiyo hivyo wakaamua kutumia alama ya mnyoo aliyeviringishwa kwenye kijiti kama alama ya ushindi wa tiba dhidi ya magonjwa. Kile kinachoonekana kama nyoka aliyeviringishwa kwenye mti ni mnyoo aliyeviringishwa kwenye kijiti! Na hiyo ni alama inayotumika kuwakilisha tiba za asili (na kisasa) dunia nzima. Kwa makusudi ama kwa kutokutambua baadhi ya wachambuzi na wahubiri wanapotosha watu.

Nimetoa ufafanuzi wa alama hii ya mnyoo anaedhaniwa kuwa ni nyoka baada ya msomaji mmoja kunitumia ujumbe ufuatao, “Bw Sanga nakupongeza kwa makala yako yenye mtazamo chanya. Lakini amini usiamini hawa Freemason wameenea sana maeneo mengi.”

“Kuna chuo kikuu cha (anakitaja kwa jina) ingawa ni cha dini lakini kwenye nembo yao kuna alama ya nyoka kama yule aliyepo kwenye hela ya shilingi mia tano. Hata chuo cha (anakitaja kwa jina) ingawa ni cha serikali lakini kwenye majengo yake kuna alama hii ya nyoka wa Freemason.” Mwisho wa kumnukuu.

Habari za shetani zimeendelea kuzalisha migongano isiyo ya lazima baina ya wananchi na serikali. Unaposema serikali inayomwongoza ni ya Freemason unadhani mwananchi atakuwa na mtazamo gani kuhusu serikali na maendeleo ya nchi yake?

Badala ya kuwaombea viongozi wa nchi yake atakuwa akiwakemea kwenye maombi! Moja kwa moja utakuwa umempoteza kiroho na kulitia hasara taifa! Umeshamweleza amejua kuwa nguo anazovaa ni za Freemason, sawa! Sasa afanyaje? Je, atembee uchi ili kuwakimbia Freemason? Kama huna suluhu ya nini afanye, ujue umemuachia maumivu ya kisaikolojia!

Ngoja nitoe mchapo mwingine kuhusu hilo; kuna wakati nilikua nikisafiri kutoka Songea kwenda Iringa mjini na nikasimama Njombe mjini kwa muda kuoanana na rafiki yangu wa utotoni. Nilipokutana nae ndio kwanza alikuwa ametoka kuzisikia habari za Freemason.

Katika mazungumzo yetu nilimuuliza swali hili, “Inakuwaje uchumi wa Marekani unaporomoka kwa kasi kiasi hiki? Manake wale wakiporomoka na Tanzania ndio msiba zaidi!?” Nilishangaa sana jibu alilonipa ukizingatia ni msomi wa chuo kikuu, “Wanaofanya hivyo ni Freemason!”. Kwa kuwa nilikuwa naelewa kwa undani sana habari hizi za shetani nikajua kinachomsumbua, “hofu na taarifa zilizotiwa chumvi mno”

Baadae rafiki yangu huyu akanieleza kuwa baada ya kuzijua alama za Freemanson amegundua kuwa zipo kwenye nguo na baadhi ya vifaa vyake hivyo akavichoma moto! Baada ya mwezi mmoja akanipigia simu akinieleza habari hizo hizo lakini safari hii akiwa mnyonge sana,

“Bwana Albert, nimeamini ulichonieleza ya kuwa nisihangaike na kuzijua habari hizi za Freemason badala yake nikazane kumjua Mungu. Naona sasa habari hizi zinanichanganya, eti wamesema kiongozi wetu mkuu wa dhehebu letu ni Freemason!”. Nikacheka sana na kumjibu “..ukijikita kumjua Mungu kuna uweza ambao utakushindia katika mambo mengi hata hizo hatari za Freemason zinazokutisha”.

Naelewa kuwa wachambuzi na wahubiri wengi wanatumia hoja ya kwamba “Ukimjua adui ni rahisi kumshinda”. Hilo sawa! Lakini kitu ambacho mimi niko kinyume nacho ni namna adui anavyohubiriwa na kujulikana

Nami nitawauliza swali? Unawezaje kumshinda adui hata kama unamfahamu kiasi gani; ikiwa hauzijui silaha zako wewe mwenyewe? Kitakachotokea ni kuwa, kwa sababu umewekeza muda na akili nyingi kujifunza habari za adui pasipo kuzijua silaha zako; utabaki ukimtafakari adui na kinachozaliwa ni hofu! Matokeo ya hofu ni kushindwa na kupigwa!

Kwanza binafsi nadhani waabudu shetani wenyewe wamevujisha habari zao kwa makusudi ili wajipatie umaarufu. Ni ushahidi ulio wazi kwamba kinachowafanya watu wayaogope sana makundi haya ya kishetani ni kwa sababu hawana imani kubwa (ama niseme maarifa) kwa Mungu wao. Na wahubiri pamoja na waandishi kwa kujua kua wanafuatiliwa kwa ukaribu sana; wanazidi kuwasha moto kila kukicha kwa habari hizi.

Hizi ni habari ambazo wakati mwingine zinaleta uchonganishi katika jamii, zinaleta uvivu na zinaharibu fikra za wanajamii. Kuna watu wanaamini kuwa ili ufanikiwe kifedha ni lazima uwe Freemason! Kinachotokea? Watu hawajitumi ipasavyo wakiamini kua walioandikiwa fedha ni wanachama wa Freemanson!

Lakini mitaani watu (kwa alama na sababu wanazohubiriwa) wameshawawekea ‘lebo’ watu mbalimbali kwa madai kua ni Freemason. Kinachotokea? Watu wanawachukia wenzao na kuona kama mashetani. Sitashangaa nikija kusikia kuna watu wanachomwa moto kwa sababu ni Freemason.

Hivi sasa watu wanaamini kua kila ajali inayotokea barabarani inasababishwa na Freemason. Kinachotokea? Watu wanaendelea kuwa wazembe katika matumizi ya barabara kwa sababu wanaamini kuwa Freemason wakiamua ugongwe na gari ama basi lianguke basi wanakuua! Huu ni upuuzi, mmempa Shetani umaarufu asiostahili!

Nimesoma kwenye mitandao pamoja na baadhi ya magazeti yakieleza kua kifo cha msanii maarufu kilichotokea hivi karibuni kilisababishwa na Freemason kwa sababu alikua ni mwanachama wa Freemason. Si kazi yangu kuthibitisha ama kukanusha hili lakini kuna upande nataka tuuone ambao ni atahari za kuenea kwa taarifa hizi.

Nini kinatokea baada ya kuvuma kwa taarifa hizi? Watu wanaamini kua huwezi kuwika na kung’aa katika sanaa kama hautakuwa Freemason! Hata sasa watu wanaunganisha mafanikio waliyonayo baadhi ya wasanii wa filamu na muziki; na Freemason. Vijana na watoto wenye vipaji wanakata tamaa ya kujaribu kuviendeleza na kung’aa kwa sababu wanaamini kuwa bila kujiunga na Freemason hutoki!

Wataalamu wa mambo ya saikolojia na ustawi wa kijamii wameeleza kisayansi kanuni iitwayo, “Law of Attraction”. Kwa mujibu wa kanuni hii ni kuwa “Mtu huyavuta yale mambo anayoyafikiria na kuyawaza muda mwingi”. Ukitaka mafanikio, waza mafanikio, ukitaka kumjua Mungu mtafakari Mungu!

Huwezi kumjua Mungu kwa kuzitafakari kazi za shetani. Utapata unachokiwaza! Nadhani ndio maana Daudi katika Biblia alisema, “Jambo nililoliogopa sana, ndilo lililonipata” Tuziepuke ‘taarifa zilizotiwa chumvi kupitiliza;’ ambazo zinaamsha hofu bila kutupatia majawabu!

Watanzania tuanahitaji ushindi wa kifikra!

[email protected] 0719 127 901