Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewashauri wazazi/ walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto kwani ndugu na jamaa wa karibu ndio wanaongoza kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto.
Kwa mujibu wa mtandao wake waziri huyo ameandika hayo kutokana na kifo cha mtoto wa mfanyabiashara, Zainab Shaban maarufu ‘Jojo’
Kwa mujibu wa taarifa ya waziri huyo, alimuacha mtoto huyo na dereva wa bodaboda wa Ilazo Extension aliyefahamika kwa jina la Kelvin Gilbert. Alisema tafiti zinaonesha ndugu na jamaa wa karibu ndiyo wanaoongoza kuwafanyia watoto ukatili ukiwamo ubakaji, ulawiti na hata mauaji.
“Nimesikitishwa na kitendo kilichofanywa kwa mtoto, Graison Kanyenye (6) kwa kuuawa kikatili na watu wasiojulikana. Wizara imepokea taarifa hizi za kusikitisha za kifo cha mtoto huyu wa umri wa miaka sita aliyekuwa anaishi eneo la llazo jijini Dodoma,’’
“Taarifa za awali zinaonesha kuwa mama wa mtoto alitoka nyumbani na rafiki yake na kumkabidhi mtoto kwa mtu aliyemwamini na baada ya kurudi mzazi huyo alikuta mtoto amefariki dunia kwa kuuliwa’’ aliandika Dk Gwajima.
Alisema ni simanzi kubwa kwani mtoto huyo amekatishwa uhai wakati ndiyo kwanza alikuwa anaanza safari ya ndoto za maisha yake.
“Ninatoa pole nyingi kwa wazazi wa mtoto, ndugu na jamaa kwa msiba huu mkubwa uliogusa hisia za wengi,” alisema Dk Gwajima.
Alieleza anayo imani vyombo vya kusimamia sheria vitafuatilia jambo hilo kwa kadri iwezekanavyo, wahusika wabainike na haki ya mtoto ipatikane na kuwa funzo kwa wengine wanaofanya ukatili kwa watoto.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, mauaji hao yametokea asubuhi ya Desemba 25, mwaka huu saa 1:00 asubuhi ambapo mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.
“Desemba 25, mwaka huu, saa 1:00 asubuhi katika Mtaa wa Bwawani Ilazo Extension jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed, kulitokea tukio la mtoto wa miaka sita kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa matembezini,” alieleza Kamanda Katabazi.
Aliongeza: “Mama wa mtoto huyo alitoka na mume wake kwenda matembezini na kumwacha mtoto huyo chini ya usimamizi wa dereva bodaboda wa Ilazo Extension aliyefahamika kwa jina la Kelvin Gilbert”.
Kwa mujibu wa Katabazi, katika uchunguzi wa awali wamebaini bodaboda huyo alifahamiana na familia hiyo na walimtumia katika shughuli mbalimbali.
Alieleza kuwa kutokana na ukaribu huo, walimuachia mtoto huyo amwangalie kipindi ambacho wawili hao watakuwa katika matembezi na hivi sasa wanamshikilia na kumuhoji huku uchunguzi ukiendelea kuwabaini washukiwa wengine.
Aidha, Jeshi la Polisi limewasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo ya kikatili.