Muhsin Hendricks, mtu mashuhuri aliyejulikana kama imamu wa kwanza duniani aliyejitangaza hadharani kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, ameuwa kwa risasi nchini Afrika Kusini.

Kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 57 alikuwa anaongoza msikiti mmoja katika jijini la Cape Town uliolenga kuwa mahali salama na kimbilio kwa waumini wa kiislamu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wale waliotengwa na jamii.

Alipigwa risasi Jumamosi asubuhi baada ya gari alilokuwa akisafiria karibu na jiji la kusini la Gqeberha kushambuliwa.

“Washukiwa wawili wasiojulikana wakiwa wamefunika nyuso zao walitoka kwenye gari ingine na kuanza kulimiminia risasi nyingi gari hilo,” polisi walisema katika taarifa yao.

Habari za kifo cha Hendricks zimeleta mshtuko mkubwa katika jamii ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ+ ) na kwingineko, huku kukitolewa salamu nyingi za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Julia Ehrt, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la International Lesbian, Gay, Bisexual, Trans and Intersex Association (ILGA), ametoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi wa kina juu ya kile kinachohofiwa kuwa “huenda ni uhalifu unaohusisha chuki”.

“Aliwasaidia na kuwaelekeza watu wengi nchini Afrika Kusini na duniani kote katika safari yao ya kiimani, na maisha yake yalikuwa mfano wa uponyaji unaotokana na mshikamano wa jamii mbalimbali,” alisema.

Hendricks aliuawa baada ya kuripotiwa kufungisha ndoa ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, ingawa hili halijathibitishwa rasmi.

Taarifa za tukio hilo zilifichuliwa kupitia picha za video za CCTV zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Video hiyo inaonyesha gari likisimama na kuziba njia ya gari alilokuwamo Hendricks kabla ya kuanza kushambuliwa.

Kwa mujibu wa Polisi, imamu huyo alikuwa amekaa kwenye kiti cha nyuma.