Ni jambo lisilopingika kuwa Ilala ndiyo Dar es salaam, na kama kuna mtu yeyote anayepinga na ajitokeze hadharani kupinga ili tupingane kwa hoja. 

Pamoja na ukweli huo, bado Halmashauri ya Manispaa ya Ilala haijajitambua hata kidogo kwenye uwajibikaji katika maeneo nyeti na hivyo kuifanya isiwe mfano bora wa kuigwa pamoja na kuwa iko karibu zaidi na mamlaka zote halali za nchi!

Hata hivyo, kwa leo nitazungumzia maeneo mawili tu ya miundombinu na usafi wa mazingira.

Si suala la kuzusha wala la majungu kuwa Manispaa ya Ilala imekuwa na miundombinu ya barabara zisizokidhi viwango na hivyo kuifanya ikose sifa ya kuwa kioo cha Dar es Salaam. Barabara ya kutoka Kitunda kwenda Kivule ni mahandaki makubwa, mahandaki ambayo hayastahili kuwa ndani ya Manispaa ya Ilala ambayo ndiyo makao makuu ya nchi. Kwa sasa kuna kifusi cha matope kiko pale na kusababisha msongamano zaidi ya wiki mbili sasa bila kusawazishwa japo ni matope!

Vilevile Daraja la Kivule lilivunjika zaidi ya miaka miwili iliyopita na kusababisha kero kubwa sana kwa wananchi wa eneo hilo, achilia mbali ndugu zetu wasio na hatia waliopoteza maisha kutokana na kuvunjika kwa daraja hilo, hadi sasa hakuna kilichofanyika katika kulitengeneza, tunasubiria maafa mengine? Manispaa ya Ilala bado iko usingizini?

Hebu angalia barabara ya Kitunda-Mwanagati-Buza ambayo kwa miaka mingi haijawahi kuonja hata tone la kifusi, achilia mbali kupitisha hata greda! Barabara hii shukuru Mungu wananchi wa Mwanagati hujichangisha vijisenti vyao na kujitengenezea barabara baada ya kutelekezwa na manispaa! je, ni kutokana na ufinyu wa bajeti au siyo kipaumbele? Angalia eneo la Majohe nako ni kama Kitunda, hazifai barabara zake.

Hata hivyo, eneo hili la miundombinu ya barabara huhitaji fedha, yawezekana ndiyo maana kuna mahandaki makubwa yasiyo mithili ya chochote. Hata hivyo, kuhusu usafi wa mazingira hapa sitarajii kuomba radhi kwa namna yoyote ile. Naomba niseme kwa uwazi kabisa kuwa uongozi wa Manispaa ya Ilala umeshindwa kazi! Ni aibu kuona dampo katikakati ya mji kama ilivyokuwa pale eneo la Banana Ukonga takriban miaka miwili iliyopita kabla sijaikemea kwa kuiandika kwenye gazeti la JAMHURI  kwa kuipa kichwa cha maneno“Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na tajiri wa takataka”. 

Baada ya kuiandika kwenye gazeti hilo, siku ya pili tu Halmashauri ya Ilala ilishtuka na kutoka usingizini na kupeleka tingatinga na malori kwenda kuundoa uchafu huo uliokuwa umekuwa donda ndugu. Kwenye makala yangu hiyo nilihoji kama kuna fedha zozote za kigeni zinazohitajika kuliondoa dampo hilo! Hata hivyo kufumba na kufumbua nilipata jibu kuwa hapana, fedha za kigeni hazihitajiki, kwani haraka ile ya kuiondoa siku mbili tu baada ya kuanikwa hadharani isingetoa muda wa kutafutwa kwa fedha za kigeni kwa ajili ya dampo hilo. Hapa jibu ni uzembe na kutowajibika, hakuna jingine!

Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania, aliwaongoza Watanzania katika kufanya usafi Desemba 9, 2015, tulishangilia na kujitokeza kufanya usafi. Lengo likiwa ni kuwaonesha Watanzania kuwa uchafu ni janga kubwa lisilo stahili kufumbiwa macho, na hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anakuwa nalo mbali. Pamoja na juhudi hizo za dhati za kiongozi mkuu wa nchi ambaye aliipa heshima siku hiyo baada ya kukerwa na uchafu, lakini bado juhudi zake zimeendelea kupuuzwa na watendaji! Ninauliza tena, je, kuondoa uchafu kunahitaji fedha za kigeni? Kwa kweli mimi sina hakika kama fedha hizo zinahitajika, bali ni uzembe uliotopea. 

Mheshimiwa Rais, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilivunjwa mwaka 1996 na Waziri Mkuu wa wakati huo, Frederick Sumaye, kutokana na kukithiri kwa uchafu ndani ya jiji. Leo hii zaidi ya miaka 20 jiji la Dar es Salaam ambalo Ilala ni makao yake makuu ni chafu kuliko kipindi hicho.

Kama ninasema uongo naomba ufanye ziara ya kushtukiza kwenye maeneo mawili tu. Naomba nikuchagulie maeneo hayo. Anzia Mtaa wa Lindi na Msimbazi uangalie mifereji/mitaro iliyo jengwa vizuri na kufunikwa kwa mifuniko mizuri ya zege pembeni mwa mtaa wa Lindi ilivyogeuzwa maeneo ya kutupia takataka. Wafanyabiashara wa maeneo hayo hufunua mifuniko hiyo na kutumbukiza uchafu unaotokana na biashara zao kwenye mitaro hiyo. Je, watendaji hawapo? Je, maafisa afya hawapo? Je, hili hawalioni au wanasubiri uwashtukizwe?

Eneo jingine ni Shule ya Msingi Lumumba ambayo iko takriban meta 100 kutoka makao makuu ya Manispaa ya Ilala. Majengo yake yanatisha, achilia chemchemi ya maji machafu yanayotiririka kila mara mbele ya lango la shule hii ambayo ilistahili kuwa shule ya mfano ndani ya Manispaa, tena hata ikibidi kwa upendeleo maalum, leo hapafai kutokana na mazingira yake yalivyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri amka utumie sheria za nchi kuwaondoa ombaomba ambao wamekuwa tatizo kubwa ndani ya Manispaa yako, ninajua kuwa una mamlaka hayo kisheria. Amka kwani hawa ndugu ni chimbuko la baadhi ya maradhi kama vile kipindukipindu. Hebu sote tujiulize maji yale wanayokunywa pale eneo la Maktaba na Bibi Titi, Mnazi Mmoja na maeneo mengine maarufu kwa ombaomba hao wanayatoa wapi? Je, haja kubwa na ndogo wanakwenda wapi? Maji ya kunawa wanayatoa wapi? Nenda pale nyuma ya Shule ya Shree Hindu Mandal Mtaa wa Bibi Titi uone walivyopafanya! 

Wakati sasa umefika kwa Watanzania kutofumbia macho tabia ya uzembe kwani tumefika hapa kwa sababu ya uzembe wa watu wachache ambao wamejisahau na kushindwa kutimiza wajibu wao. Tumetengeneza mazingira ya baadhi ya magonjwa kwa uzembe na kutowajibika. Jipu la Ilala limeiva, litumbuliwe.

 

[email protected]