Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha misaada, mikopo na usaidizi mwingine kutoka Serikali Kuu ya shirikisho, kulingana na taarifa iliyovuja ya Serikali na kuthibitishwa na CBS News.
Katika taarifa hiyo, kaimu mkuu wa Ofisi ya Usimamizi na Bajeti (OMB) anatoa wito kwa mashirika ya serikali kuhakikisha matumizi yanaendana na vipaumbele vya Trump.
Athari ya usitishwaji huu bado hazijabainika, ingawa taarifa hiyo inabainisha kuwa bima ya afya ya Medicare na Usalama wa Jamii havitaathirika. Inakuja siku chache baada ya Marekani kusitisha karibu misaada yote ya kigeni.
Hatua hiyo imekosolewa na wanachama wa chama pinzani cha Democratic ambao wanaonya juu ya “athari mabaya” kwenye programu ambazo watu hutegemea misaada na mikopo.
Seneta wa Washington, Patty Murray na Mbunge wa Connecticut Rosa DeLauro – walituma barua kwenda Ikulu ya Marekani siku ya Jumatatu jioni wakielezea:
“Tunawaandikia leo kuwasihi kwa nguvu zote mzingatie sheria na Katiba na kuhakikisha rasilimali zote za shirikisho zinatumika kwa mujibu wa sheria.”
Naye Diane Yentel wa Baraza la Kitaifa la Mashirika Yasiyo ya Faida anasema agizo hilo linaweza kukwamisha utafiti wa saratani, usaidizi wa chakula na simu za dharura za kuomba msaada wa ushauri.
Waraka huo, uliotiwa saini na kaimu mkuu wa OMB, Matthew Vaeth, unatoa wito kwa mashirika ya serikali kusitisha kwa muda programu zao za usaidizi wa kifedha, ili waweze kukagua matumizi ambayo yanaweza kuathiriwa na maagizo ambayo Trump ameyatia saini.
Ikulu ya Marekani bado haijatoa kauli rasmi kuhusu waraka huo uliovuja.