Wabunge kadhaa wamejiandaa kuhoji matumizi ya Sh bilioni 6 zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa Ikulu.
Kiasi hicho cha fedha kimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Wabunge wanahoji kiasi hicho kikubwa hasa kutokana na kuonekana kuwa kila mwaka wa fedha hutengwa mabilioni ya shilingi kwa kazi hiyo ya ukarabati.
Mwaka 2010/2011 zilitengwa Sh bilioni 7.257; na mwaka 2011/2012 zilikuwa Sh bilioni 10.257.
“Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa hasa ikizingatiwa kuwa ni miaka ya karibuni ambako kulitumika mabilioni ya shilingi kuikarabati Ikulu,” amesema mmoja wa wabunge hao.
Wabunge kumbana Waziri Mgimwa
Katika hatua nyingine, wabunge wamejiandaa kuhoji uhalali wa kufutwa kwa misamaha ya magari kwa waliokuwa wakifaidika nayo.
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alitoa msimamo huo wa Serikali alipokuwa akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2012/2013.
Alisema, Serikali inapendekeza, “Kufuta msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo isipokuwa kwa miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mkataba, mashirika ya dini, balozi, ofisi za balozi, wanabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic Missions). Aidha, haitahusu kampuni za madini zenye mikataba yenye kutoa misamaha.”
Wabunge na watumishi wa Serikali ni miongoni mwa waliokuwa wakinufaika kwa msamaha huo.
Hata hivyo, kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu ya wadau mbalimbali, wakiwamo wabunge, ya kutaka misamaha ya kodi ipunguzwe. Kwa sasa misamaha ya kodi ni zaidi ya asilimia tatu ya pato la taifa. Kiwango hicho kinatakiwa kishuke hadi asilimia moja kama yalivyo makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baada ya Dk. Mgimwa kusoma mapendekezo hayo, wabunge waliguna na kwa nyakati tofauti wameahidi kupambana ili waendelee kunufaishwa na msamaha huo.
Mjadala wa bajeti ya Serikali ulianza jana, huku wabunge wengi wakionekana kujiandaa vema kuibana Serikali.
Ujenzi Barabara ya Makutano-Loliondo
Ujenzi wa barabara iliyoibua mvutano mkali ya Makutano-Nata-Mugumu/Loliondo-Mto wa Mbu, umetengewa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Barabara hiyo, hasa kipande chenye urefu wa kilometa 53 kinachopita ndani ya Hifadhi ya Serengeti kimekuwa kikipigiwa kelele na wadau kadhaa wa ndani ya nchi na katika jumuiya ya kimataifa.
Wanaoendesha mapambano hayo kwa kiasi kikubwa ni raia wa Kenya ambao wanaamini kuwa kujengwa kwake kutavuruga uhamaji wa nyumbu na wanyamapori wengine kutoka Serengeti kwenda katika hifadhi ndogo ya Maasai Mara nchini humo.
Hata hivyo, msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kwamba barabara hiyo haina budi ijengwe ili kufungua mawasiliano kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa mingine nchini.
Wilaya mpya taabani kifedha
Katika bajeti ya mwaka 2012/2013 zimetengwa fedha kwa wilaya na mikoa yote nchini. Tanzania Bara ina mikoa 25 na wilaya 133.
Hata hivyo, wilaya mpya zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha, kwani wilaya kama ya Butiama imetengewa shilingi zisizozidi milioni 130.
Hiyo ina maana kwamba ujenzi wa nyumba za watumishi na ofisi hautakuwa wa kasi iliyotarajiwa.