Nianze kwa habari njema. Nimeandika kitabu cha pili kiitwacho ‘Kufanikiwa ni haki yako.’ Ni kitabu ambacho kimebeba maarifa, visa vya kusisimua na mikasa kuhusu safari za maisha ya mafanikio ya watu mbalimbali waliofanikiwa duniani.
Kwa mfano, katika kitabu hiki ninakuletea kisa cha mzee mmoja alie tajiri mpaka sasa; ambae miaka ya nyuma kuna siku alikubali kulala lupango kwa kosa la kutolipa kodi ya kichwa shilingi mia sita, wakati mfukoni alikuwa na laki tatu!
Askari walishangaa sana, lakini yeye akawaambia “Hii laki tatu ni kwa ajili ya kununulia mabati, sijaipanga kulipia kodi, nilazeni tu kituoni ila sivurugi malengo yangu”. Utakisoma kisa hiki kwa urefu na utajifunza funzo kubwa kuhusu njia za kupita ili ufanikiwe. Kitabu hiki, kitakuchekesha, utashangaa, utahamasika na hautakuwa ulivyokuwa. Kisipokufundisha kitu naahidi tutakurudishia fedha yako!
Kitabu hiki kitauzwa kwa njia ya mtandao. Kwa nini nimeamua kuandika kitabu kitakachouzwa na kusoma kwenye mtandao? Kwa hivi sasa Tanzania kuna matumizi makubwa ya simu za kisasa maarufu kama “screen touch” yaani zile simu ambazo hazina buttons.
Wabunifu wa simu hizi mbali ya kupiga na kupokea simu wamezibuni maalumu kwa ajili ya kusomea vitabu na ndio maana zina programu maalumu zinazowezesha kutunza na kusoma vitabu kwa starehe. Wengi hawajaitumia fursa hii ipasavyo ndio maana nimekuja kuitendea haki hii fursa.
Kitabu hiki kipo katika mfumo wa “pdf”. Unakinunuaje? Pengine ndio swali la msingi. Utatuma fedha kwa simu na kisha utatujulisha email yako, nasi tukishathibitisha malipo tunakutumia kitabu ndani ya masaa 24, unakipakua na kuanza kukifurahia iwe ni katika simu ama kompyuta yako. Raha yake ni kwamba utakisoma popote katika simu ama laptop, badala ya kupoteza muda unaposubiri daladala ama appointment ama unaposubiri wateja dukani, unakuwa ukisoma na kuongeza ufahamu.
Kitabu kinauzwa Sh. 5,000. Nambari za kutumia pesa ni hizi zifuatazo: 0688 726442 (Airtel Money), 0766 742414 (M-PESA), 0719 127 901 (Tigo-Pesa). Namba zote zitasoma Albert Sanga. Huhitaji kutuma pesa ya kutolea, wewe lipa pesa kamili. Ukishatuma pesa, tuma ujumbe wa kutujulisha na email yako ama namba yako ya whatsapp ili tukukabidhi kitabu chako.
Na sasa ngoja nieleze kidogo namna unavyotakiwa kufanikiwa kibiashara ukiwa hai na baada ya kufa kwako. Nianze kwa kukupatia mchapo wa kweli unaomuhusu ndugu yangu wa karibu.
Nina ndugu yangu mmoja wakati akifariki katikati ya miaka ya tisini alikuwa ni mmoja ya wafanyabiashara waliokuwa wakipanda kwa kasi kubwa kibiashara. Akiwa ameshakusanya uzoefu wa kusafiri kibiashara hadi nchi za jirani ikiwemo Malawi alifariki na kuacha biashara ambazo zilikuwa zimesitawi sana.
Baada ya kuondoka kwake mke wake alijaribu kuvaa viatu vyake; lakini mambo yalimuendea kombo! Alipambana kuzisuka upya biashara zile, akabadilisha jina na kutafuta masoko mapya. Ni kama alikuwa akianza upya kabisa kwa sababu mtangulizi wake (mume wake) hakuacha urithi kamili wa kimfumo.
Haikupita miaka mingi sana kabla ya mwanamama huyo kuyumba kutokana na kuzidiwa na changamoto na ushindani wa kibiashara. Sababu kubwa ya mama yule kushindwa kuhimili mikiki ya biashara zile ni kwa sababu wakati wa uhai wake mumewe, hakumshirikisha mama kwa asilimia mia moja kuhusu uendeshaji wa biashara zile.
Ingawa mwanamama alikuwa akisimamia maduka kwa maana ya kuuza; lakini hakuwa akijua mali zinachukuliwa wapi, hakuwahi kusafiri nae kufuata bidhaa, hakujua biashara zina madeni kiasi gani na pia hakuwa anaelewa kiukamilifu mfumo kamili wa biashara zile kwa ujumla.
Ndugu zangu Wakinga (na mimi ni mkinga pia) wengi wao wana tatizo hili. Licha ya kuwa wana mafanikio makubwa sana katika tasnia ya biashara lakini ni wachache sana ambao wanawashirikisha wake zao kwa asilimia mia moja kwenye biashara zao.
Ninao jamaa zangu Wakinga wanaotamba na maduka ya nguo maeneo ya Kariakoo, wakiwa wanafuata bidhaa zao nchini China, Uingereza na Dubai; lakini wengi wao wake zao hawajui hata tiketi ya ndege inavyofanana. Ndio maana kumekuwa na uvumi (myths) mwingi kuwa wakinga wengi wanapofariki biashara huwa zinawafuata makaburini.
Uvumi huo husemwa kuwa ni kwa sababu ya kutumia ushirikina. Stori za Wakinga na janja yao ya biashara za kishirikina zimetapakaa sana hasa mikoa yetu hii ya Nyanda za Juu Kusini; ambako Wakinga ndio wanatamba kibiashara. Hata hivyo kuna sababu ya kisayansi zaidi ya hizo vumi kutokana na suala la mtu kufariki na kisha biashara zake kumfuata kaburini. Hili la ushirikina nitalichambua katika makala inayojitegemea huko mbeleni.
Kwa bahati mbaya ni kuwa sio wakinga pekee; isipokuwa biashara nyingi za watanzania ndivyo zilivyo. Ni biashara chache sana ambazo hufanikiwa kuhimili ama kukua ndani ya miaka kumi mara baada ya mmiliki wake kufariki dunia. Ni kwa nini mambo haya hutukia kwa namna hii?
Watanzania wengi tunaendesha biashara kienyeji. Hatuna mifumo ya kibiashara, hatuna malengo ya biashara na wala hatuna mwelekeo wa kibiashara. Wengi wetu tunategemea kudra za mwenyezi Mungu kutufikisha mwakani, hatuna uhakika na tunakoenda wala hatujui tutafika lini. Tuna macho ya kuitazama leo tu, hatuna malengo ya angalau hata muongo mmoja.
Watanzania wenzetu wenye asili ya Kihindi na Kiarabu wametuzidi sana katika hili. Wenzetu hawa wana tamaduni imara sana za kibiashara kiasi ambacho matajiri wengi tunaowasikia sasa wenye asili hii; mali hizo wamerithi eidha kutoka kwa baba ama babu zao. Muhindi ama Muarabu hawezi kuanzisha biashara halafu ikafa kirahisi!