Na Bashir Yakub
Kila wakili ni mwanasheria, lakini si kila mwanasheria ni wakili. Wakili ni zaidi ya mwanasheria. Ili uwe wakili unaanza kuwa mwanasheria.
Mwanasheria ni mtu yeyote aliyesoma kozi ya sheria katika chuo kinachotambulika na kuhitimu, kufaulu na kupata shahada ya sheria (@LLB).
Huyu sasa ndiye anaitwa mwanasheria. Moja ya kazi anazoweza kufanya ni pamoja kutoa ushauri wa kisheria katika baadhi tu ya mambo.
Wakili. Huyu ni mtu yeyote aliyesoma kozi ya sheria katika chuo kinachotambulika na kuhitimu, kufaulu na kupata shahada ya sheria (@LLB).
Kisha baada ya kupata shahada hiyo ya sheria (@LLB) akajiunga na kusoma Shule ya Sheria kwa vitendo (Law School), akafanya mitihani na kufaulu, kisha akaapishwa na Jaji Mkuu, hivyo kuitwa WAKILI.
Yapasa kujua kuwa hata ukiwa na masters ya sheria (LLM), au PHD ya sheria, au uwe profesa wa sheria, kama haujaenda Shule ya Sheria na kufaulu bado hauwezi kuitwa wakili, utabaki kuwa mwanasheria.
Na hii ni hata ukiwa hakimu au jaji na hata jaji mkuu unaendelea kuwa mwanasheria mpaka ufuate utaratibu huo.
Kwa hiyo uwakili ni hatua ya pili baada ya uanasheria. Unaanza kuwa mwanasheria, kisha unakuwa wakili.
Kazi anazoweza kufanya wakili ni pamoja na kumuwakilisha mtu mahakamani, kutoa ushauri wa kisheria, kuandaa nyaraka za kisheria, kuruhusiwa kufungua ofisi ya uwakili, kusimamia mikataba ya aina yote, kumiliki muhuri n.k.
Hizi kazi kama kumuwakilisha mtu mahakamani, kuandaa baadhi ya nyaraka za kisheria, kuruhusiwa kufungua ofisi ya uwakili, kusimamia mikataba n.k, haruhusiwi kufanya mwanasheria.
Mwanasheria hawezi pia kumiliki muhuri. Ndiyo maana muhuri huo huwa umeandikwa ADVOCATE (WAKILI), na si LAWYER ( MWANASHERIA).
Wapo wanasheria ambao si mawakili, ambao hujitambulisha kama mawakili, hivyo kufanya kazi za mawakili, yumkini huwa ni makosa makubwa.
Na unajuaje kuwa huyu ni wakili ama si wakili? Ni rahisi sana, andika neno ‘eWAKILI’ kwenye Google.
Itakuletea eneo la kuandika jina la mtu unayemtafuta. Andika jina la mtu huyo eneo hilo kisha bofya neno ‘TAFUTA/SEARCH’.
Kama mtu huyo ni wakili, itakuletea jina na picha yake na kama si wakili jina na picha havitatokea na itakuandikia: ‘Hakuna wakili aliyepatikana.’
Basi, kila wakili ni mwanasheria, lakini si kila mwanasheria ni wakili.