Leo (wiki iliyopita) gazeti la Mtanzania limeripoti kufungwa kwa Hotel kadhaa za kifahari kutokana na sababu mbalimbali, lakini sababu kuu iliyotajwa ni hatua ya Serikali kuzuia mikutano yake kufanyika hotelini, badala yake ifanyike kwenye kumbi za Serikali na kudaiwa kodi (Mtanzania, Julai 14, 2016, uk.3 na 4).

Nilitamani kufanya uchambuzi wa kina kuhusiana na hali hii, lakini nizungumze kwa kifupi kwa sababu niko ‘field’ huku kwa Wanyantuzu natafuta karo ya shule ya mwanangu. Nionavyo uamuzi huu wa Serikali una faida na hasara zake.

 

Faida kwa kifupi

Mosi; Mzunguko wa fedha utapungua na hivyo kusaidia sana ku-control inflation rate (mfumko wa bei, unaotokana na monetary factor sio production factor). Sifa mojawapo ya fedha ni isiwe holela. Pesa ikiwa holela inazaa mfumuko wa bei (inflation by monetary factor). Hivyo pesa inatakiwa ipotee kidogo, iwe adimu lakini si adimu sana (money should be scarce but not very scarce).

Kwahiyo pesa ikipotea kidogo hata bei ya bidhaa na huduma itashuka. Maana yake ni kwamba bidhaa zitakuwepo, lakini pesa hamna. Kwa hiyo itabidi zishuke bei. Hii itawaumiza wafanyabiashara, lakini itawasaidia sana walaji.

Na hii ni mbinu nzuri sana ya kudhibiti uchumi. Bidhaa na huduma vitapungua bei sana. Kwa mfano Hotel ambayo ulikuwa ukilala kwa Sh 400,000 kwa usiku mmoja, muda si mrefu utaanza kulala kwa Sh 100,000 na zile za Sh 100,000 zitashuka hadi Sh 40,000. Mfuko wa saruji kama unanunua Sh 15,000 tegemea kununua Sh 8,000 muda si mrefu. Hii ni habari njema kwa walaji (Consumers), lakini habari mbaya kwa wazalishaji (Producers) na wafanyabiashara.

Pili, njia hii itasaidia sana kuleta “nidhamu ya kazi”. Kwa kuwa mzunguko wa pesa utakuwa mdogo itawalazimu watu kufanya kazi kwa bidii kupata pesa. Enzi za kupata pesa kiulaini zimekufa. Enzi za kumuandikia Mkuu wa Idara “minutes” na kujifanya mlikuwa na kikao, halafu mkuu wa Idara anasaini mjilipe posho, enzi hizo zimekwisha rasmi. Sasa ni kazi tu.

Kama unataka pesa fanya kazi, kama hutaki utakula jeuri yako. Kwa hiyo kuanzia sasa watu watafanya kazi kwa bidii na uchumi wa nchi utakua kwa kasi. Utashangaa kuuziwa mfuko wa saruji Sh 7,000, lakini utashangaa zaidi kwamba unafanya kazi siku mbili hiyo Sh 7,000 huipati. Kutakuwa hakuna namna nyingine zaidi ya kuongeza bidii!

Tatu, njia hii itasaidia sana kuimarisha sarafu yetu. Moja ya mambo yaliyokuwa yakichangia kuporomoka kwa sarafu yetu ni mfumko wa bei kuwa mkubwa sana. Sasa kwa utaratibu huu wa JPM mfumko utakuwa umedhibitiwa, kwa hiyo pesa itapotea mitaani.

Na pesa ikipotea maana yake itatafutwa. Na ikitafutwa inamaanisha mahitaji yake yanaongezeka. Na mahitaji yakiongezeka ina maana thamani yake pia inaongezeka. Kwa hiyo usishangae hadi kufika mwaka 2020 dola 1 ya Kimarekani ikauzwa Sh 1,000 au chini ya hapo.

Pia kwa kuwa mzunguko wa pesa utakuwa mdogo watu hawatafanya tena ununuzi nje ya nchi. Kwa hiyo watanunua zaidi bidhaa za ndani na hivyo kusaidia kuimarisha sarafu yetu.

Nne, njia hii itasaidia kuleta nidhamu ya matumizi. Yaani mtu akipata hela ataitunza vizuri na kuweka akiba maana hajui kama kesho atapata tena. Unajua watu hawakuwa na nidhamu kabisa ya matumizi. Ulikuwa unakuta mtu anaenda baa mwisho wa wiki moja anatumia milioni moja inaisha.

Wiki inayofuata anaenda tena na milioni baa inateketea. Ananunulia watu pombe, anahonga kila mwanamke anayemrembulia, akienda “Live band” kila jina lake likitajwa anatoa Sh 100,000. Lakini kuanzia sasa nidhamu itakuwepo. Hakuna mtu atakayekuwa na ujasiri wa kufanya mbwembwe za kijinga tena kama hizo. Nidhamu ya matumizi itaongezeka sana.

Tano, itasaidia kupunguza ombwe (gap) kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. Ngoja nikupe mifano michache. Kuna watumishi ambao mishahara yao haizidi milioni moja, lakini walikuwa na uhakika wa kuingiza milioni 5 hadi 6 kila mwisho wa mwezi kwa “deals” mbalimbali. Mara vikao, mara safari, mara ununuzi (procurement wanakula 10%), n.k.

Kwa hiyo unakuta mtu ana kipato cha milioni 7 au 8 kwa mwezi, anajiona juu kuliko wewe ambaye kipato chako ni 800,000. Anafanya ununuzi Nakumat wewe unanunua Mwenge. Lakini kuanzia sasa ngoma droo. Wote mnaenda kuhemea sokoni Buguruni Malapa.

Sita, maskini wataanza kumiliki ardhi na bei ya ardhi na viwanja itaanza kuwa affordable (kuhimilika) katika maeneo mengi. Unajua ardhi ilikuwa inapandishwa na “wapiga dili”.

Mtu amepata hela zake bila jasho anaenda kununua ardhi kwa mamilioni na kuifanya ardhi ya eneo hilo kupanda thamani. Kama mnakumbuka ile skendo ya boss mmoja wa shirika moja la hifadhi ya jamii aliyenunua ardhi Arusha kwa Sh milioni 5 halafu akaiuza kwa shirika analoliongoza kwa Sh bilioni 1.

Sasa imagine (fikiria) ardhi imepanda thamani kutoka Sh milioni 5 hadi Sh bilioni 1 ndani ya mwaka mmoja. Kwa hiyo wenye ardhi jirani na hapo wakiona mwenzao kauza bilioni 1 nao wanapandisha bei. Lakini kuanzia sasa discipline (nidhamu) itakuwepo. Mfumuko wa bei katika ardhi hautakuwepo tena. Kwa hiyo hata maskini watakuwa na uwezo wa kununua na kumiliki ardhi.

 

Hasara kwa kifupi

Mosi, watu wengi sana watapoteza ajira kutokana na sekta nyingi za uzalishaji kufungwa. Jiulize hoteli zote zilizofungwa wafanyakazi wanakwenda wapi? Na sio kwenye hoteli tu, viwanda vitafungwa, kampuni na mashirika yatapunguza wafanyakazi. Wote hao wataenda kurundikana mtaani na kugeuka kuwa tegemezi.

Pili, taasisi nyingi za fedha zitafilisika. Benki zilizozoea kukopesha wafanyabiashara kwa riba kubwa sasa hivi zitakosa wateja, na hivyo “ku-run bankrupt”. Kwa hiyo tutegemee benki nyingi kufa na chache zitakayo-survive zitapunguza wafanyakazi na kufunga baadhi ya branches (matawi) zake.

Tatu, sekta nyingi za uzalishaj na fursa za ujasiriamali zitadumaa. Hii ni kwa sababu hazitakuwa na mitaji na pia wananchi hawatakuwa na purchasing power (nguvu ya ununuzi) ya kuweza kumudu gharama ya baadhi ya bidhaa.

Kwa mfano mtu alikuwa anaweza kwenda benki akakopa Sh milioni 500 akaanzisha duka la kuuza vitu vya ndani kama furniture (samani), mafriji, TV set, na akapata wateja wengi ndani ya mwaka mmoja akarudisha mkopo wa benki akaanza kula faida.

Lakimi kuanzia sasa hivi wajasiriamali wengi hawatathubutu kukopa. Na wakikopa hawatakuwa na uwezo wa kulipa. Kwa hiyo mfanyabiashara akinunua bidhaa za Sh milioni 500 akaziweka dukani, halafu baada ya mwezi mauzo ni Sh 600,000, lazima atafute sumu ya panya atangulie akhera madukani!

Nne, kuyumba kwa bei katika soko la hisa kwa sababu baadhi ya wanahisa katika kampuni nyingi wanaweza kuuza hisa zao kufidia mikopo yao benki. Na kwa kuwa fedha itakuwa adhimu (scarce) watalazimika kuuza hata kwa bei ya hasara hali itakayolifanya soko la hisa kuyumba.

Tano, kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu. Kwa kuwa watu wengi watapoteza kazi, wengine biashara zao, wengine watapoteza dili zao za kuwaingizia kipato, watalazimika kutafuta njia nyingine ya kuishi. Na njia Rahisi ni kujiingiza katika vitendo vya kihalifu kama ujambazi, ukahaba, utapeli, wizi. n.k.

Kwa hiyo tutegemee kusikia matukio mengi ya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha katoka maeneo kama benki, super markets, Bureau de change na hata majumbani. Hakuna mtu atakayekuwa tayari kukuona unatoa Sh milioni 1 ATM akakuacha hivihivi wakati yeye ana siku ya pili hajala.

 

Hitimisho

Sisemi Rais aendelee kubana matumizi au aache. Ninachotaka kusema ni kuwa apime kati ya faida na hasara kisha afanye uamuzi kwa maslahi ya nchi. Zipo faida na hasara nyingi zaidi ya hizi. Hapa nimeeleza kwa kifupi tu, lakini najua Rais anao washauri wazuri wa masuala ya kiuchumi watamsaidia kumshauri vizuri kwa maslahi ya “Mama Tanzania”.

 

Godfrey Malisa ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na amejitolea kuwapa elimu ya biashara na fedha Watanzania akiamini huo utakuwa mmoja wa michango yake hapa duniani. Mchungaji Malisa anapatikana kwa simu 0716810677.