Katika kipindi hiki cha kuelekea fainali za soka za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil kuanzia Juni 12, mwaka huu, JAMHURI imeona vema kuwakumbusha mashabiki, wapenzi na wadau wa soka kwa jumla, historia ya mashindano hayo.

Historia ya Kombe hilo iliandikwa kwa mara ya kwanza mwaka 1928, wakati Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wakati huo, Jules Rimet, alipoamua kuandaa michuano mikubwa zaidi duniani inayohusisha mataifa mbalimbali. 
Ufunguzi wa mashindano hayo ulifanyika miaka miwili baadaye (mwaka 1930) nchini Uruguay, wakati timu 13 zilipoalikwa kushiriki. 
Kabla ya michuano ya Kombe la Dunia, mechi ya kwanza ya kimataifa ya soka duniani ilichezwa mwaka 1872 ikizihusisha England na Scotland. Kipindi hicho ilikuwa ni mara chache kwa mchezo wa soka kuchezwa nje ya Uingereza. 
Hata hivyo, kuanzia mwaka 1900 mchezo wa soka ulipata umaarufu duniani kote na vyama vingi vya soka vikaanzishwa. Mechi ya kwanza rasmi ya kimataifa kuchezwa nje ya Uingereza ilikuwa kati ya Ufaransa na Ubelgiji iliyochezwa Paris, Mei 1904. 
Mchezo huo ulileta msukumo wa kuanzishwa kwa FIFA Mei 22, 1904. Shirikisho hilo lilianzishwa na vyama vya soka vya Ufaransa, Ubelgiji, Denmark, Uholanzi, Hispania, Sweden na Uswisi huku Ujerumani ikiomba kujiunga. 
Mchezo wa soka ulianza kutambulika kama mchezo rasmi wa michezo ya Olimpiki mwaka 1904 katika kipindi cha majira ya joto. Baadaye FIFA ilianza kusimamia michuano ya Olimpiki upande wa soka katika kipindi cha majira ya joto mwaka 1908. 
Wakati huo, mchezo wa soka ulikuwa unajumuisha wachezaji wa ridhaa huku ukichukuliwa kama mchezo wa maonesho kuliko ushindani. 
Timu ya soka ya taifa ya ridhaa ya England ilishinda michuano hiyo ya Olimpiki mwaka 1908 na mwaka 1912. Baadaye FIFA ilijaribu kuanzisha michuano mingine ya soka ya kimataifa bila ya kuhusisha michuano ya Olimpiki. 
Majaribio haya yalianzishwa mwaka 1906 nchini Uswisi. Zilikuwa siku za mwanzo za soka la kimataifa. Historia rasmi ya FIFA inaelezea kwamba mkutano huo ulishindwa kuzaa matunda. 
Huku michuano ya Olimpiki ikiendelea kushindanisha timu za ridhaa, michuano ya timu za kulipwa nayo ilianza. Michuano ya Torneo Internazionale Stampa Sportiva ilifanyika jijini Turin, Italia mwaka 1908. Hii ilikuwa ya kwanza na mwaka uliofuata Sir Thomas Lipton alianzisha michuano iliyofahamika kama ‘Kombe la Sir Thomas Lipton’ iliyofanyika Turin. 
Michuano hiyo ilikuwa inashirikisha klabu na si timu za taifa. Klabu moja ilikuwa inawakilisha taifa zima nyumbani. Kwa sababu hii, hakuna michuano ambayo ilichukuliwa kama mfano wa Kombe la Dunia kabla ya uwepo wa Kombe hilo. 
Mwaka 1914, FIFA ilikubali kuitambua michuano ya Olimpiki kama ‘Michuano ya Dunia ya Ridhaa’ na ilikubali kuwajibika kuandaa michuano hiyo. Hii ilisababisha uwepo wa michuano ya kwanza ya kimataifa ya soka katika Olimpiki ya mwaka 1920, ambapo Ubelgiji alitwaa ubingwa, huku Uruguay ikishinda michuano hiyo mwaka 1924 na 1928. 
Mwaka 1928, FIFA ilichukua uamuzi wa kuandaa michuano yao. Huku Uruguay ikiwa imeshinda mara mbili michuano ya Olimpiki na ikijiandaa kusherehekea mwaka mmoja baada ya kupata uhuru, FIFA iliamua kuipa Uruguay uenyeji wa michuano hiyo ya kwanza ya Kombe la Dunia mwaka 1930. 
Michuano ya mwaka 1932 ya kipindi cha majira ya joto ilifanyika jijini Los Angeles na haikupanga kuujumuisha mchezo wa soka kutokana na umaarufu mdogo wa mchezo huo Marekani. 
FIFA na IOC zilikuwa zimeshindwa kukubaliana masuala kadhaa ya michuano hiyo, kwa hiyo mchezo wa soka ukaondolewa katika orodha ya mashindano ya mwaka huo. 
Rais wa FIFA, Jules Rimet, ndiye aliyeamua kuandaa michuano hiyo iliyofanyika Uruguay mwaka 1930. Vyama kadhaa vya soka viliteuliwa kupeleka timu zao, huku chaguo la uenyeji likienda kwa Uruguay. 
Hakuna timu yoyote ya Ulaya ambayo ilithibitisha kupeleka timu mpaka ilipobaki miezi miwili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo. Kwa juhudi binafsi za Rimet alifanikiwa kuzishawishi nchi za Ubelgiji, Ufaransa, Romania na Yugoslavia kusafiri. 
Nchi 13 zilishiriki michuano hiyo huku saba zikitoka Amerika ya Kusini, nne kutoka Ulaya na mbili kutoka Amerika ya Kaskazini. 
Mechi mbili za kwanza zilichezwa mfululizo huku Ufaransa ikiichapa Mexico 4-1 na Marekani ikiinyuka Ubelgiji 3-0. Bao la kwanza katika historia ya Kombe la Dunia lilifungwa na Lucien Laurent wa Ufaransa. 
Siku nne baadaye dunia ilishuhudia Bert Patenaude akifunga mabao matatu kwa mpigo (hat trick) katika ushindi wa 3-0 wa Marekani dhidi ya Paraguay. Katika pambano la fainali lililochezwa Montevideo, wenyeji Uruguay waliitandika Argentina 4-2 mbele ya mashabiki 93,000 na kuingia katika historia ya timu iliyotwaa kwa mara ya kwanza taji hilo. 
Hivyo ndivyo michuano ya Kombe la Dunia ilivyoanza. 
Mechi ambayo ilihudhuriwa na mashabiki kidogo zaidi katika Kombe la Dunia ni kati ya Romania na Peru katika fainali za mwaka 1930 nchini Uruguay. Waliingia mashabiki 300.

Hakuna nchi yoyote ya Ulaya iliyopata kutwaa Kombe la Dunia nje ya Bara la Ulaya.

Diego Maradona ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi akiwa nahodha. Alicheza mechi 16.

Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 ziliandaliwa katika nchi za Japan na Korea Kusini. Ugomvi mkubwa baina yao ulikuwa ni jina la nchi gani litokee kwanza katika tiketi za mechi hizo.

Hakuna nchi yoyote ambayo ilipata kufungwa pambano lake la kwanza na baadaye kutwaa Kombe la Dunia.

Julai 31 imetajwa kama siku ya mapumziko nchini Uruguay, baada ya taifa hilo kutwaa Kombe la Dunia lilipofanyika kwa mara ya kwanza.

Tabia ya wachezaji kubadilishana jezi uwanjani ilipigwa marufuku mwaka 1986 na FIFA, kwa sababu haikupenda kuwaona wachezaji wakitoka nje ya uwanja vifua wazi.

Matokeo mengi katika Kombe la Dunia ni 1-0. Rigobert Song wa Cameroon ndiye mchezaji aliyepewa kadi nyekundu katika michuano miwili ya Kombe la Dunia mfululizo. Alipewa dhidi ya Brazil mwaka 1994 na akapewa dhidi ya Chile mwaka 1998.

Mchezaji aliyefunga mabao mengi ya kichwa katika fainali za Kombe la Dunia ni Miloslav Klose wa Ujerumani. Katika fainali za mwaka 2002 alifunga mabao matano kwa kichwa.

Pambano la Kombe la Dunia mwaka 1970 kati El Savador na Honduras lilikuwa na upinzani mkubwa kiasi kwamba nchi hizo ziliingia katika vita ya mtutu kwa siku tatu.

Ni mabara mawili yaliyopata kushinda Kombe la Dunia, ambayo ni Ulaya na Amerika ya Kusini. Ulaya imeshinda mara nane na Amerika ya Kusini imeshinda mara tisa. Mabara ya Asia, Afrika, Amerika ya Kaskazini na Kati hayajapata kutwaa taji hilo.

Brazil ni nchi pekee iliyocheza michuano yote ya fainali za Kombe la Dunia. Pia ndiyo nchi pekee iliyofunga idadi kubwa ya mabao katika fainali za Kombe la Dunia. Imefunga mabao 173.