Na Tatu Saad, JAMHURI MEDIA
Kikosi cha Ihefu FC kimeanza rasmi mazoezi ya kujifua chini ya benchi la ufundi la timu hiyo, kuelekea mchezo wa Robo Fainali kombe la shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Simba SC utakaopigwa jijini Da Es Salaam.
Ihefu imerudi kambini na kuanza mazoezi hayo baada ya mapumziko kwa kujiandaa na michezo hiyo miwili itakayopigwa ndani ya mwezi mmoja (April) ambapo yote kwao ni michezo muhimu.
Kocha msaidizi wa Ihefu FC, Zuberi Katwila amesema wanahitaji kujiandaa mapema kutokana na ukubwa na ubora wa mpinzani wao Simba SC kwani wamekuwa na wakati mzuri katika michezo yao ya Kimataifa Ligi Ya Mabingwa wanayoshiriki.
“Tuna dakika 180 ngumu tunahitaji kujiandaa mapema kwa kujiweka fiti kutokana na kukutana na wapinzani ambao wamepata wakati mzuri wa kucheza michezo mingi mfululizo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wanayoshiriki na sisi tulikuwa na mapumziko kupisha michezo miwili ya timu ya taifa.” amesema Katwila.
Amesema katika timu yao ni wachezaji wachache walioitwa kwenye vikosi vya timu za taifa hivyo wanakikosi chakutosha kwa asilimia kubwa hivyo wanajitahidi kujiandaa vizuri ili muda ukifika timu iwe bora sana.
“Kwa asilimia kubwa kikosi kipo ni wachezaji wachache walioitwa timu za taifa hivyo tutaendelea kujiweka fiti ili muda ukifika timu inakuwa bora”, amesema Katwila
Amesema moja ya maandalizi wanayofanya ni kuwandaa wachezaji kisaikolojia na kuhakikisha wanatumia kila nafasi watakayotengeneza ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri.
“ Tunawandaa wachezaji kisaikolojia kuhakikisha wanatumia kila nafasi watakayotengeneza ili kuweza kujiweka nafasi nzuri,” amesema Katwila.
Katwila amesema kikosi kimeimarika baada ya wachezaji kuingia kwenye mfumo na wameanza kuona utofauti na malengo yao yanaenda kutimia kutoka kuwa kwenye presha ya kushuka daraja na sasa kuwania tano bora kwenye msimamo.
Amesema ubora uliopo kwenye kikosi chao hawataki kuona unaanza kupotea kutokana na kutokukaa pamoja kwa muda mrefu ndio maana wamewarudisha wachezaji haraka kambini ili kuendelea kuwaweka kwenye hali ya ushindani