Katika toleo la leo tumechapisha taarifa za magendo ya zao la korosho, maarufu kama ‘kangomba’ inayoendelea katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi. Kwa kiasi kikubwa, habari hiyo imejikita katika Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Tunduru.
Watendaji wa umma katika ngazi ya wilaya wametajwa kwa kiasi kikubwa kuhusika katika biashara ya kangomba. Askari PC Mtaki ametajwa kutoa fedha za kununulia korosho kwa raia akidai korosho ni za viongozi wake, lakini baadaye akamsulubu huyo raia.
Si PC Mtaki pekee, bali askari wa kutoka Kituo cha Polisi cha Nakapanya, Tunduru wametajwa kuwa na vituko vya kutisha. Kwa mfano, mwananchi Rashid Chinyang’anyi wamechukua pikipiki yake kufidia fedha walizompa awanunulie korosho za magendo naye akawa hajatimiza ahadi yake.
Mwananchi mwingine, Mohamed Mchanguni, mkazi wa Kijiji cha Msinji, Tunduru amelalamika kuwa polisi wameingia nyumbani kwake usiku akiwa katika lindo shambani mwake wakachukua korosho zake kilo 204 na pikipiki yake.
Pikipiki hiyo ameikomboa baada ya kuwalipa askari polisi Sh 20,000 kama rushwa, wakati awali walikuwa wamemtaka atoe Sh 500,000 akawa hana. Korosho zake bado wanazishikilia kwani hakuwa na Sh 500,000 za kuwapatia kama rushwa.
Raphael Matiku Makanya, mkazi wa Kijiji cha Msinji, anasema naye Novemba 21, 2018 polisi hao hao walimkamata yeye na watuhumiwa wengine 6, kisha wakawambia hawana kosa ila kuachiwa lazima walipe rushwa ya Sh 50,000 kila mmoja. Wakalipa wakaachiwa.
Novemba 26, 2018 mchana, polisi wawili wakiwa na silaha walikwenda tena nyumbani kwa Makanya na kumkuta mtoto wake Makanya Matiku (12), wakamshurutisha afungue mlango na walipoingia ndani chumbani, walipekua hadi kwenye foronya kitandani na kudaiwa kuiba akiba yake ya Sh 400,000.
Kwa matukio ya kushiriki kununua korosho za kangomba, kupora wananchi pikipiki, kuchukua rushwa kama mshahara halali kwao, kupekua nyumba yenye mtoto wa miaka 12 bila uongozi wa mtaa au kijiji husika na kudaiwa kupora Sh 400,000 zilizokuwa kwenye foronya, tunaamini askari hawa wamelidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kiwango cha juu kisichovumilika.
Tunamsihi Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, afuatilie tukio hili na kuchukua hatua dhidi ya askari waliohusika haraka, vinginevyo asipochukua hatua atakuwa anayeyusha imani ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi, suala ambalo ni hatari kubwa. Matendo ya aina hii hayakubaliki katika nchi huru ya Tanzania. Polisi waliohusika wachukuliwe hatua haraka.