Mhariri salamu,
Nimeamua kuandika barua hii kwako
Inspekta Jenerali wa Polisi wa Tanzania
(IGP) ikufikie kupitia Gazeti la JAMHURI,
nikiwa raia wa Tanzania na mdau wa
usalama barabarani, nimeona nitoe
mchango wangu wa mawazo katika
kupambana na ajali za barabarani.
Nikiwa mwalimu wa somo la Uraia na mdau
wa masuala ya usalama barabarani,
napendekeza kuanzishwa kwa kampeni ya
kitaifa ya kupambana na ajali za barabarani
itakayobeba ujumbe usemao: “Dereva
Thamini Maisha Yako, Ya Abiria na
Wengine.”
Ajali nyingi za barabarani zimekuwa
zikisababishwa na uzembe wa madereva
kwa ulevi na kutozingatia alama na sheria
za barabarani. Naamini kampeni hii itasaidia
kupunguza ajali za barabarani.
Kampeni hii iwaelimishe madereva na
iwasisitize jinsi wanavyotegemewa na
familia, ukoo, jamii na taifa lao katika
gurudumu la maendeleo. Kampeni
iwaonyeshe jinsi vifo vya madereva
vinavyoleta simanzi kubwa na kuathiri
maendeleo ya nchi.
Hivyo, madereva daima wawapo katika
vyombo vyao vya usafiri, waviendeshe kwa
tahadhari kubwa wakijua kuwa kama ajali
itatokea itakuwa na madhara makubwa kwa
maisha yao. Kutokana na hilo, wathamini
maisha yao kwa kuzingatia alama na sheria
za barabarani kama njia ya kukomesha
ajali.
Kampeni pia iwaelimishe madereva kuwa,
kama wanavyothamini maisha yao pia
wathamini maisha ya abiria waliowapakia
katika vyombo vyao vya moto. Madereva
wazingatie kuwa wamebeba roho nyingi za
abiria ambao wana matumaini ya kufika
salama katika safari zao. Hivyo, madereva
waache uzembe na kuzingatia sheria za
barabarani ili kuepusha ajali ambazo si tu
zinaleta vifo na ulemavu kwao, bali na abiria
wao pia.
Kampeni hii iwahamasishe madereva
kuthamini maisha ya abiria wao ambao
mara nyingi ajali zinapotokea zinakatisha
maisha ya wengi ambao ni nguzo muhimu
kwa familia, ukoo na taifa katika harakati za
maendeleo. Kampeni iwasisitize madereva
kujali maisha ya wapita njia na watembea
kwa miguu, kwani nao wamekuwa wahanga
wakubwa wa ajali za barabarani.
Kampeni ya “Dereva Thamini Maisha Yako,
Ya Abiria na Wengine”
, ilenge kuwajengea
madereva hamasa kubwa ya kuzingatia
sheria za usalama barabani kama njia ya
kupunguza ajali ambazo zimekuwa
zikikatisha uhai wa madereva, abiria na
wengine, huku ukiacha majonzi kwa familia,
ukoo, jamii na taifa na kuathiri kwa kiasi
kikubwa maendeleo.
Naamini kampeni hii italeta matokeo chanya
katika kupunguza ajali za barabarani.
Kampeni ionyeshe namna ambavyo
maendeleo ya taifa lolote duniani
linavyotegemea nguvu kazi. Vifo
vinavyosababishwa na ajali za barabarani
vinaathiri kasi ya maendeleo.
Kampeni ionyeshe kuwa dereva ambaye
anathamini maisha yake hawezi kutumia
kileo wakati akiendesha chombo cha moto.
Hivyo, dereva anayetumia kileo hawezi
kusema anathamini maisha yake na ya
abiria na watumiaji wengine wa barabara,
kwani kwa kufanya hivyo anahatarisha
maisha yake na ya watu wengine.
Sambamba na kampeni hii kuwalenga sana
madereva, pia itoe elimu kwa abiria kuwa
wasikae kimya wanapoona dereva
anaendesha gari kwa mwendo kasi
kupitiliza. Mwendo kasi kupitiliza
unachangia ajali nyingi za barabarani. Abiria
wawapo katika vyombo vya usafiri
waungane na wawe na sauti moja katika
kumuamuru dereva kupunguza mwendo.
Ikiwa dereva atakaidi amri ya abiria wake,
abiria wapige simu Polisi Kitengo cha
Usalama Barabarani kutoa taarifa ili hatua
stahiki zichukuliwe dhidi ya dereva wao.
Naamini kila dereva akizingatia thamani ya
maisha yake, ya abiria na ya watumiaji
wengine wa barabara, ajali ambazo
zinatokana na uzembe wa madereva
zitapungua kwa kiwango kikubwa.
Wasalamu,
Ni mimi Reuben Michael Lumbagala,
Mwalimu wa somo la Uraia na
mdau wa usalama barabarani,
Kongwa, Dodoma.
Simu: 0764 – 666349
Mwisho