Sehemu iliyopita mwandishi wa makala hii alirejea hadithi iliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuhusu msichana mzuri aliyekuwa akichumbiwa. Akaeleza namna Mwalimu alivyohakikisha hageuki jiwe katika kuijenga nchi kwenye misingi ya kijamaa. Hii ni sehemu ya pili na ya mwisho ya makala hii. Endelea…

Basi, kwa ustaarabu wa wenzetu kule ‘majuu’, mtu unaposhindwa katika uchaguzi unakubali matokeo (to concede defeat) na kumpongeza aliyeshinda.

Huku barani Afrika ustaarabu huo hatujaufikia. Ila kinyume chake ni kukosoa na kubeza uchaguzi na kuilaumu tume iliyoendesha huo uchanguzi.

Aidha, kule Ulaya na Marekani chama kinaposhindwa tu, uongozi wa juu unaachia ngazi ili wengine wapite kushika usukani kuongoza gurudumu lile kuelekea kwenye uchaguzi ujao.

Tabia hii kwa Bara letu la Afrika haipo na wala haitakuwapo, maana hapa chama ni mali ya mtu, wala si taasisi ya siasa. Ndiyo maana utasikia chama kinakwenda mafichoni kujipanga upya kwa mapambano yajayo (to re-organize). Hali hiyo mpaka lini?

Hivyo tuite ni demokrasia ya Kibantu au sijui tuiteje? Inalenga kutokuachia ngazi mpaka kieleweke! Inasemekana wameibuka na kaulimbiu ‘Tumejitofautisha Wataiga, Hawataweza Kutekeleza.’

Ningetamani viongozi wa vyama vyetu vyote vya siasa wamwombe Mungu awajalie hekima ya kutawala kama vile alivyojaliwa Mfalme Suleiman hapo kale.

Napenda hapa kunukuu yale maombi ya Mfalme Suleiman. Kwanza ombi lake lilisema: “…Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako na kupambanua mema na mabaya… (Fal. 3:9)”. Majibu ya Mungu: “…Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako: bali umejitakia AKILI ZA KUJUA KUHUKUMU: basi tazama nimekupa moyo wa HEKIMA na AKILI…” (I FAL. 3:11-12)

Hapo ndipo mimi naona taifa letu linahitaji viongozi wenye kuwa na fikra na mitazamo kama ule wa Mfalme Suleiman hapo kale. Waifikirie nchi ya Tanzania kwanza, na sisi wakazi maskini na wanyonge. Tusingependa kuona viongozi wanaweka nafsi zao na matarajio yao ya kisiasa mbele kuliko kufikiria unyonge na umaskini wetu.

Nafikiri viongozi wetu wa vyama vya siasa wajitafakari na waombe kuwa kama yule Mfalme Suleiman wa katika Biblia.

Watufikirie sisi Watanzania na nchi yetu hii kwanza na waweke ndoto zao za kushika dola kama umuhimu wa pili (2nd priority).

 Kufikiria kila wazo la watu wengine ni kupendelea chama tawala na kuchukia upinzani ni ufinyu wa fikra. Katiba ya nchi hii sura ile ya 1, sehemu ya III, kifungu cha 18(a) kinasema: Haki na Uhuru wa mawazo yake namna hii: “Kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.”

Mimi naona Watanzania tukomae kifikra na tuache sasa kuwa na ufinyu wa mtazamo (myopic conception) eti kila maoni yasiyokubalika kwa wao, basi yanalenga kuzorotesha upinzani, hivyo kuunga mkono chama tawala.

Tukubali upinzani endelevu (constructive criticism) kwa maendeleo ya kujenga na tuepuke upinzani kulisambaratisha taifa, wala hauleti mshikamano, bali unatugawa.

Duniani upinzani ni ‘catalyst’ ya maendeleo. Hilo haliepukiki hata kidogo. Na upinzani ukikomaa ndivyo changamoto zinavyoonekana, hivyo kuchochea kasi ya maendeleo. Bila upinzani, watawala watajisahau na  mambo yatakuwa ‘leisure affair.’

Mungu Ibariki Tanzania.