MOROCCO inaomboleza vifo vya zaidi ya watu 2,000 vilivyosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Ijumaa usiku, wakati timu za uokoaji zikifanya juhudi kuwatafuta watu waliokwama kwenye vifusi.
Wanajeshi na wafanyakazi wa kutoa misaada wameonekana wakipeleka maji na mahitaji mengine katika vijiji vilivyoathiriwa.
Janga hilo, hadi sasa limesababisha takribani watu wengine wasiopungua 2,000 kujeruhiwa wengi wao wakiwa katika hali mbaya kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni huku idadi hiyo na ya vifo ikitarajiwa kuendelea kuongezeka.
Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 6.8 kwa kipimo cha Richter lilitokea umbali wa kilomita 72 kusini magharibi mwa mji wa kitalii na wakihistoria wa Marrakech ambapo liliviharibu vijiji vingi. Familia nyingi katika mji wa Marrakech zimelala nje kwa usiku wa pili baada ya mkasa huo zikihofia kuwa nyumba zao hazina tena usalama.
Mamlaka nchini humo zimetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa wakati mataifa mengine yakiwemo Israel, Ufaransa, Uhispania, Italia na Marekani yametangaza kutoa msaada.
Taifa jirani la Algeria ambalo limekuwa na uhusiano wa mashaka na Morocco lilifungua anga yake ambayo liliifungia Morocco kwa miaka miwili, ili kuruhusu ndege zinazobeba misaada ya kiutu na majeruhi ziweze kulitumia