Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar
TUME ya Tehama (ICTC) imesaini hati ya makubaliano na ushirikiano na Taasisi ya Ruge Mutahaba ya kuinua vijana na wanawake waweze kushiriki na kunufaika kiuchumi kupitia matumizi ya teknolojia za kidigitali.
Makubaliano hayo yamelenga kushughulikia maeneo ya utafiti, ukuzaji ujuzi na ubunifu kupitia mafunzo, warsha na mikutano.
Katika hafla fupi iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, makubaliano hayo yalisainiwa ya Dkt. Nkundwe Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu wa ICTC kwa niaba ya Tume na Cynthia Bavo, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Ruge Mutahaba.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Dkt Mwasaga amesema ICTC imefikia makubaliano kwa lengo la kuwawezesha makundi hayo kuwa na uwezo wa kuchangamkia fursa zilizopo katika Uchumi wa Kidigitali.
Amesema Tume ipo tayari kutekeleza jukumu walilokubaliana na taasisi ya Ruge Mutahaba kwa kuwa hiyo ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Tehama na sera nyingine zinazoitegemea TEHAMA kama nyenzo kuu ya kufikia malengo ya sera husika.
“Kwa hiyo tumeona tuongeze nguvu ya ushirikiano katika kuwainua kisekta wanawake na vijana katika maeneo ya utafiti, ubunifu, na kuwajengea ujuzi na uwezo kwa ujumla kwa njia mbalimbali…uchumi wa dunia unakwenda kushikwa na sekta ya tehama hivyo ni vyema wanawake na vijana wakaandaliwa vyema katika eneo husika, kuanzia ubunifu, utafiti na kadhalika,” amesema Dkt. Mwasaga.
Naye Cynthia ambaye taasisi yake ilianzishwa Juni 22, 2022 kwa lengo la kuendeleza maono ya Ruge Mutahaba ambaye enzi za uhai wake alijikita zaidi katika ustawi wa vijana, wanawake na Watanzania kwa ujumla, alisema wana kila sababu ya kuendeleza mazuri ya Ruge.
Taasisi ya Ruge imejikita katika dhima kuu tano ambazo ni ubunifu, uvumbuzi, umahiri, upambanaji na uzalendo, na ili kutekeleza hayo, inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali, sekta binafsi na mashirika ya ndani na ya Kimataifa katika kuendesha miradi ili kutatua changamoto za wanawake na vijana hasa katika eneo la ajira na kutengeneza kipato.
“Enzi za uhai wake, Ruge aliwekeza sana katika ubunifu na ujasiriamali wa vijana na wanawake ili kuwasaidia katika kuinua kipato…hivyo tunalenga kuyapa uhai na kutekeleza maono yake chanya ya kimaendeleo yaliyolenga vijana na wanawake kwa kupitia fursa mbalimbali,” alisema na kusisitiza kuwa, taasisi ina mikakati ya kuendesha miradi ya kusaidia wanawake na vijana kupitia ujasiriamali wenye tija, sanaa na ubunifu.
Mbali na ushirikiano na Taasisi ya Ruge Mutahaba, katika kujenga uwezo na kukuza taaluma ya Tehama nchini, Tume ya Tehama katika mwaka huu wa fedha imejipanga katika kuendelea na ukamilishaji wa vituo vya ubunifu TEHAMA (Soft centers) katika Kanda 5 pamoja na kuanzisha kituo kimoja Zanzibar.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwasaga, tume pia inalenga kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA, kuwezesha uanzishaji wa vituo vya majaribio vya ubunifu TEHAMA katika ngazi za wilaya, kufanya tafiti za maendeleo ya TEHAMA na kufanya tathmini ya kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya TEHAMA;
Tume pia inalenga kuratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za TEHAMA ndani na nje ya nchi, kushirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za TEHAMA ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za TEHAMA hapa nchini, kujenga kujenga kituo cha Akili Bandia na kuanzisha Kituo cha Resilience Academy hapa nchini kwa ajili ya kuendeleza wataalamu wa TEHAMA.
Imelenga pia kuwezesha mafunzo maalumu ya wataalamu wa TEHAMA 500, kukuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogondogo “startup” kwa kushiriki maonesho na makongamano yanayohusu fursa za startups duniani, na kadhalika.
Hivi karibuni, Tume ilipeleka wabunifu saba katika maonesho ya Afrika yaliyofanyika Algiers, Algeria kwa lengo la kuwakutanisha na wabunifu na wawekezaji mitaji wa kimataifa ikiwa na matarajio ya kuongeza fursa kwa kampuni changa za TEHAMA kupanua na kukuza mitaji yao ya kibiashara.