Kulikuwa na vilio na simanzi Mtaa wa Vatican, Sinza Dar es Salaam, nyumbani kwa aliyekuwa mwigizaji maarufu ndani na nje ya Tanzania, Steven Charles Kanumba ‘The Great’. Kanumba alifariki dunia alfajiri ya kuamkia Aprili 7, mwaka huu.

Wengi hawakuamini. Hata mimi nilipopigiwa simu na msomaji mmoja saa 10 alfajiri ya siku hiyo, ili kutaka kufahamu ukweli kuhusu tukio hilo, nilipigwa na butwaa.

Taarifa hizo ziliwashitua wengi. Zilivuruga mpangilio wa usingizi kwa alfajiri hiyo, na hata maandalizi ya sherehe za Pasaka. Nilidhani kuwa ni utani tu.

Nikiwa bado natafakari, nikapata simu nyingine kutoka kwa rafiki yangu akinijulisha kuwa Kanumba amefariki dunia. Ndipo nilipoamini kuwa ni kweli hatunaye tena duniani.

Niliumia sana na kujikuta naamka kitandani na kuwasha redio. Tayari wakati huo redio nyingi zilianza kutangaza msiba huo.

Niliumia na kukumbuka mambo yake mengi ya uigizaji niliyokuwa nikiyaona yaliyonifanya nipende kuandalia filamu za Kibongo. Sikupenda kutazama filamu ambayo haikumhusisha Kanumba.

Nilijiwekea msimamo huo kwa sababu niliamini kwamba Kanumba ndiye msanii pekee anayenivutia na ninazipenda kazi zake, ingawa kuna wasanii wengi waigizaji ambao ni mahiri.

Kuvutiwa kwangu na mwigizaji huyo ni pale nilipoona anaweza kumudu kucheza katika nafasi zote na mazingira yoyote. Kila nikifikiria, inaniwia vigumu kuamini kama pengo lake linaweza kuzibwa kirahisi.

Jiji la Dar es Salaam lilizizima kwa masikitiko makubwa, huku wengine wakipoteza fahamu na wengine wakikimbia kwenda hospitali kupata ukweli wa tukio hilo, lakini jibu lilikuwa ni kwamba Kanumba hatunaye tena.

Watu wengi wameumia kutokana na ucheshi, upole na ukarimu wake. Kanumba hakuwa na majivuno wala majigambo. Aliheshimu watu wa rika zote.

Naamini wengi watakuwa wameguswa na kifo cha Kanumba, kwani kimekuwa cha ghafla mno. Ni kipindi kigumu kwa wapenzi wa kazi zake hasa wanafamilia na waigizaji, kwani kifo chake ni pigo kubwa. Mengi aliyafanya na mengi alipanga kuyafanya.

Wengi wamemwelezea Kanumba kwa mtazamo tofauti, lakini hasa waliishia kulia. Nakumbuka wiki mbili zilizopita nilizungumza naye kwa simu. Kitu kimoja alichonifurahisha nacho ni pale nilipomuuliza yeye ni shabiki wa timu gani, akajibu kwamba hana mapenzi kabisa na soka, isipokuwa tasnia ya uigizaji tu.

“Mwanahiba naweza kusema napenda Simba au Yanga, lakini mimi siujui mpira na sina timu, kwa kweli nipo zaidi katika fani hii ya uigizaji ambayo ndiyo niipendayo,” hayo yalikuwa maneno yake Kanumba ambayo hapana shaka ndiyo yaliyokuwa ya mwisho kuzungumza nami.

Nilianza kumfahamu Kanumba mwanzoni mwa miaka ya 2000 akiwa na Kikundi cha Sanaa cha Kaole chenye maskani yake Magomeni. Wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam.

Alikuwa kivutio kwa mashabiki wa sanaa za maigizo akiwa na wenzake kama Niva, Ray na wengine wengi alioshirikiana nao hadi mauti yalipomfika.

Mwaka 2004 kipaji cha Kanumba kilianza kukua zaidi hasa alipojiingiza katika uigizaji wa filamu. Filamu yake ya kwanza iliitwa ‘Johari’ na ikafuatiwa na ‘Dangerous Desire’ na ‘Sikitiko Langu’.

Kanumba hakukomea hapo. Aliendelea kutoa na kushiriki filamu mbalimbali zilizokuwa na zinaendelea kuvuta hisia za watu wengi. Filamu hizo ni kama ‘Dar to Lagos’, ‘She is My Sister’, ‘Uncle JJ’, ‘Oprah’, ‘Tufani’, ‘Young Billionea’, ‘Gharika’, ‘Baragumu’, ‘Cross My Sin’, ‘Village Pastor’, ‘Family Tears’ na nyingine nyingi.

Akiwa anaendelea kutengeneza filamu zake na kujizolea umaarufu, mwaka 2005 alianza kupata mialiko mbalimbali kutoka nchi za Nigeria, Uingereza, Marekani, Ghana, Afrika Kusini na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao, alikuwa na kasumba ya kutaka kufahamu zaidi juu ya sanaa yake. Kwa sababu hiyo, mara kwa mara alisikika akisema bado safari yake ya sanaa haijafika mwisho.

Kanumba amewahi kuigiza na msanii maarufu wa Nigeria, Ramsey Noah. Pia, amefanya kazi na wasanii wengi wa nchi hiyo na nyingine. Mwenyewe aliwahi kukaririwa akisema kwamba anafurahi kushuhudia na kushirikiana na wasanii wakubwa wa Nollywood – Kampuni ya Uigizaji ya Nigeria – na Hollywood, kampuni ya filamu ya Marekani.

Kupitia msanii huyo, nchini nyingi zimeweza kuijua Tanzania. Malengo yake yalikuwa ni kuitangaza Tanzania na malengo mengine mengi yanayosababisha wasanii wenzake kujikuta wakiwa katika wakati mgumu, kwani wapo wengine aliwaajiri.

Kanumba alikuwa anamiliki Kampuni ya Kanumba The Great Film, inayojihusisha na utengenezaji filamu. Filamu yake ya karibu inayotamba ni ‘Big Daddy’ aliyoitoa Januari, mwaka huu, na ‘Kijiji cha Tambua Haki’ aliyoitoa Februari, mwaka huu. Alikuwa katika hatua ya mwisho ya kutoa filamu yake nyingine kwa jina la ‘Ndoa Yangu’.

Kanumba alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Bugoyi na baadaye akajiunga katika Sekondari ya Mwadui kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary. Baadaye alijiunga katika Sekondari ya Jitegemee kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita.

Kanumba hakuacha mke wala mtoto. Mara zote alisema bado Mungu hajampa mwanamke bora atakayeweza kuwa mkewe.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, Gabriel Mtitu, ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Game Quality Production, Kanumba anatarajiwa kuzikwa jijini Dar es Salaam. Hadi tunakwenda mitamboni, siku ya mazishi iliyopangwa ni leo.

Hata hivyo, kulikuwa na mapendekezo kwamba mwili wake usafirishwe kwenda Bukoba kwa mama yake mzazi kwa maziko. Uamuzi wa mama ulikuwa ukisubiriwa.

Taarifa za awali za polisi zilisema Kanumba alifariki dunia baada ya kusukumwa na mpenzi wake. Inasemekana aliangukia kisogo na hivyo kuumia vibaya kichwani.

Mtuhumiwa alishikiliwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay.

Kanumba ameacha pengo kubwa katika tasnia ya uigizaji. Alipendwa na wengi, lakini Mungu kampenda zaidi.

Tumwombee apumzike kwa amani. Wasanii wanapaswa kumuenzi kwa kuendeleza mazuri yote kwa faida ya jamii na ulimwengu wa wasanii wa filamu.

Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.