Wiki iliyopita niliandika kuwa ujenzi wa uzio (fensi) pekee kwenye kiwanja si uendelezaji halisi kwa mujibu wa kanuni mpya za sheria ya ardhi tofauti na tulivyozoea. Leo tena tunatazama sehemu ya (iii) Kanuni ya saba ya kanuni mpya, kanuni za Sheria ya Ardhi kupitia Tangazo la Serikali Namba 345 la Aprili 26, 2019.

Kanuni ya 7(1) inasema kuwa mwenye kiwanja/shamba ambalo halijaendelezwa au lenye uendelezaji hafifu, endapo ataomba mkopo na kuweka rehani ardhi hiyo, atatakiwa ndani ya miezi sita tangu siku alipoweka rehani apeleke taarifa kwa Kamishna wa Ardhi kuonyesha ni namna gani fedha yote au sehemu ya fedha alizokopa zimetumika katika kuendeleza ardhi husika.

Kutokana na kanuni hii, maana yake ni kuwa ardhi unayokopea inatakiwa kuwa imeendelezwa au kama haijaendelezwa, basi kiasi cha fedha unachopata kupitia mkopo lazima kitumike kuendeleza ardhi hiyo uliyotumia kukopea bila kujali umekopa fedha ili kuzifanyia nini. Na hii ni kwa ardhi zenye hatimiliki. Mwenye ardhi atatakiwa ndani ya miezi sita tangu kuweka ardhi yake rehani apeleke taarifa maalumu kwa Kamishna wa Ardhi kuonyesha ni namna gani fedha zote au sehemu ya fedha alizopata zilivyotumika kuendeleza ardhi aliyoweka rehani.

Mfano, una kiwanja chenye hatimiliki lakini hakijaendelezwa (un-developed) au kimeendelezwa lakini uendelezaji wake ni hafifu (under-development) kama kujenga uzio tu, au ‘kijumba’ kibovu cha mlinzi. Sasa unaomba mkopo benki wa Sh milioni 50 na rehani yako ni kiwanja hicho. Benki watatazama na kuona kuwa kiwanja unachoweka rehani hakijaendelezwa au kina uendelezaji hafifu.

Watakueleza sharti hili la sheria mpya kuwa aidha ukiendeleze ndipo urudi kwao kuchukua mkopo au wakipokee kama rehani lakini kuwe na makubaliano maalumu kuwa ndani ya miezi sita kiasi cha fedha kutoka hizo Sh milioni 50 wanazokupatia kitumike kuendeleza kiwanja, na wao hilo watalisimamia kuhakikisha linafanikiwa, kwa kuwa bila kiwanja kuendelezwa mkopo utakuwa batili na wao watapoteza.

Kama utakubali utapata mkopo, kama utakataa hautapata mkopo kwa sababu bila hivyo mkopo utakuwa batili kwa mujibu wa mabadiliko haya ya sheria. Hivi ndivyo itakavyokuwa. Tafsiri kwa ujumla wake ni kuwa ardhi ambayo haijaendelezwa au ina uendelezaji hafifu kama kujenga uzio haiwezi tena kutumika kuchukua mkopo hata kama ina hatimiliki.

Aidha, kama benki wataamua kukupatia mkopo kwa masharti ya kuendeleza, basi ndani ya miezi sita tangu upokee mkopo huo ni lazima kupelekwa taarifa maalumu kwa Kamishna wa Ardhi kuonyesha ni namna gani mkopo huo umetumika kuendeleza ardhi iliyowekwa rehani, na hii ni hata kama mkopo huo unatoka kwa mafungu (installment).

Vilevile hii yote ni bila kujali unakopa ili hizo fedha ukazifanyie nini. Hata kama unataka kununua gari au kufungua biashara, sharti ni kuwa kiasi cha fedha kitoke kuendeleza ardhi. Kazi itabaki kwako umekopa kiasi gani, kiasi gani utumie kuendeleza ardhi, kiasi gani kitabaki kwa ajili ya biashara zako, na kama hilo kwako litawezekana ukarudisha fedha za watu zikiwa salama baada ya kuzikatakata hivyo.

Zaidi, taarifa ya namna fedha zilivyotumika kuendeleza eneo itakuwa katika fomu maalumu ambayo imeanzishwa na sheria hiyo – fomu namba 551.

Kwa ujumla haya yote ni tofauti na ilivyokuwa kabla ya Aprili 26, 2019 yalipoanza kutumika mabadiliko haya, ambapo kilichokuwa kinaangaliwa ni thamani tu ya ardhi bila kujali zaidi uendelezaji wake. Kwa mabadiliko haya, maana yake mwenye ardhi ambayo haijaendelezwa eneo la Masaki, Dar es Salaam kwa mfano, anaweza kuukosa mkopo na mwenye ardhi iliyoendelezwa Kimbiji, Pwani akapata mkopo.

Lengo kuu la sheria hii lilikuwa ni kuwadhibiti matajiri wanaoomba ardhi kubwa kwa malengo ya kilimo na badala yake wakipewa ardhi hiyo wanaitumia kuchukua mkopo wa fedha nyingi, na fedha hizo huzitumia kwenye biashara nyingine tofauti na kilimo na hata kuziwekeza nje ya nchi huku wakiitelekeza ardhi iliyotumika kama dhamana miaka na miaka, jambo ambalo pia limekuwa likisababisha migogoro mingi ya ardhi kwa wananchi na hao matajiri (wawekezaji).

Hata hivyo athari za lengo la sheria hii zimewagusa wamiliki wa kawaida wa ardhi hasa wale wa viwanja ambao hutumia viwanja hivyo kukopea kama tulivyoona hapo juu.

Mwisho, udanganyifu wowote katika mchakato huu ni jinai inayoweza kumfunga mhusika jela kifungo kisichozidi miaka miwili au faini, au vyote viwili kwa mujibu wa kanuni ya 9.

Kuhusu  sheria  za  ardhi, mirathi, kampuni, ndoa tembelea  SHERIA YAKUB BLOG.