*Wadau wa uhifadhi, maendeleo kuibadili Mugumu kuwa ‘Serengeti Smart City’
*Iwapo Dodoma itaidhinisha mpango huu, Senapa itabaki kileleni daima
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mara
Kwa miaka mitatu mfululizo, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) imetajwa kuwa miongoni mwa sehemu bora zaidi ya kutembelewa duniani.
Mkurugenzii wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, anasema kwa miaka huyo Serengeti imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika.
Senapa ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini (kilomita za mraba 14,763) ikizifuatia hifadhi za Nyerere (30,893) na Ruaha (19,822), na sasa idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka.
“Kwa mujibu wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC), asilimia 90.7 ya watalii wa Tanzania hutembelea vivutio vya Senapa, Ngorongoro na Zanzibar,” anasema Matinyi, akiweka wazi kuwa haya ni matokeo chanya ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Ni wazi kuwa juhudi za pamoja miongoni mwa wadau wa utalii na maendeleo ndani na nje ya nchi, zinahitajika ili kuifanya Serengeti idumu kileleni.
Tayari Serikali mkoani Mara imekuja na mkakati kabambe wa ‘uhifadhi endelevu’ na utalii wa uhakika si kwa Senapa pekee, bali kwa taifa zima.
“Tumeshakamilisha mipango ya kujengwa wa mji wa kisasa rafiki kwa mazingira (Serengeti Smart City). Upembuzi yakinifu umekamilka. Andiko lipo serikali kuu na wakati wowote ujenzi utaanza,” anasema Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk. Vincent Mashinji.
Mashinji, aliyekasimishwa na Serikali ya Mkoa kazi ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa mpaka kati ya Senapa na wakazi wa vijijii saba vinavyopakana na hifadhi wilayani humo, anasema:
“Mgogoro huu uliodumu kwa miaka 15 umemalizika kwa mazungumzo nje ya mahakama. Sasa tunadhani ni wakati muafaka kwa wananchi kufaidi matunda ya hifadhi hii bora Afrika iliyo jirani nao.” anasema.
Uwindaji haramu na tabia ya wananchi kuingiza mifugo hifadhini ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya migogoro inayotishia ustawi wa hifadhi.
Dk. Mashinji anasema mbali na utamaduni wa uwindaji wa makabila ya maeneo hayo, sababu ya migogoro ni kukosekana kwa mipango madhubuti ya matumizi bora ya ardhi.
Tafiti zinaonyesha kuwa takriban watu 300,000 wanaishi na kufanya shughuli zao ndani ya kilomita za mraba 2,300 tu.
“Hatuwezi kuiacha Serengeti ife huku tunaiona kwa sababu zaidi ya asilimia 12 ya GDP (pato la taifa) huchangiwa na hifadhi ya Serengeti. Senapa ni zaidi ya mgodi,” anasema Mashinji.
Ni kutokana na ukweli huo ndio maana Dk. Mashinji na wasaidizi wake wamepeleka andiko na mji huo utakapokamilika, hakutakuwapo tena migogoro ya kiuhifadhi kwa kuwa utazingatia matumizi bora ya ardhi.
Anasema mji huo wa kisasa utakaojengwa eneo la Mugumu, utakuwa na hoteli za kitalii, viwanja vya ndege, barabara za kisasa huku ukitumia umeme wa nguvu ya jua.
“Utakuwa mji wa kuvutia. Arusha wajipange,” anasema kwa utani Dk. Mashinji.
Mkuu wa Hifadhi azungumza
Akionyesha kufurahia kumalizika mgogoro, Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Stephen Msumi, anaahidi ushirikiano na wananchi wa vijiji hivyo.
“Matumizi bora ya ardhi yatapunguza watu kuingia hifadhini. Lakini kazi yetu sisi itabaki ile ile. Kulinda uhifadhi na kuendeleza utalii. Tunasimamia utekelezaji wa sheria. Atakayeingia au kuingiza mifugo hifadhini atakamatwa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.”
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhii Msumi anasema ombi la kujengwa kwa barabara ya kudumu kama alama ya kutenganisha hifadhi ya vijiji linafanyiwa kazi.
“Kuweka uzio wa umeme (kuzuia wanyama kuingia makazi ya watu) ni gharama. Tumeanza majaribio eneo la Ikorongo, tutaona namna ya kufanya,” anasema.
Tayari orodha ya vijana 120 watakaoajiriwa katika kambi zilizopo ndani ya hifadhi kutoka jamii inayoishi jirani na Senapa, imeandaliwa.
Wananchi wa Serengeti wamekuwa wakiiomba TANAPA kuwashirikisha kwa kuwajumuisha vijana wao kufanyakazi ndani ya Senapa.