Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita niliamka na vitu viwili kichwani mwangu. Kwanza, niliamka na kitu kinachoitwa Simba; kisha nikaamka na kitu kinachoitwa waamuzi wa soka waliopo sasa nchini Tanzania. 

Leo ninajiuliza kati ya haya mawili tuanze na lipi? Okay, nadhani si vibaya tukaanza na Simba, baadaye tukamalizia na waamuzi. 

Weka mbali kabisa matokeo ya mechi ya Simba na Mbeya Kwanza iliyofanyika wiki iliyopita. Kwa kusema ukweli Simba wanapita katika nyakati ngumu sana kwa sasa. 

Ile timu yao iliyowapa heshima kubwa misimu minne mfululizo hapo nyuma, haijabadilika sana. Haipo tofauti na hii iliyopo sasa. Lakini mambo hayaendi vema. 

Sawa, hali kama hii hutokea katika maisha ya soka na ni sehemu ya mzunguko wa kawaida. 

Tatizo kubwa lililopo Simba kwa sasa ambalo mashabiki wanapaswa kulifahamu ni timu yao kuchoka. Wazungu wanaita; ‘second season syndrome’

Mastaa wa Simba wamekutwa na aina hii ya ugonjwa ndani ya msimu unaoendelea.

Simba ileile, wachezaji walewale, wanaocheza kwenye viwanja vilevile, tena karibu wapinzani wao ni walewale, lakini mambo yamekuwa mazito. Simba wamegotea hapa?

Ugonjwa huu, ‘second season syndrome’, umewahi kuwatokea Liverpool katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England. 

Nusura majogoo hawa wa Anfield wakose nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu huu. 

Timu ikishafikia katika hali kama hii, kinachohitajika ni kufanya usajili mzuri ili kuwapumzisha mastaa waliofanya kazi kubwa na nzuri iliyotukuka katika misimu iliyopita.

Tazama usajili unaofanyika kule Liverpool ulivyokuwa. Hawa akina Diogo Jota na Ibrahim Konate wamekuja kuwapumzisha au kuwapa nafasi ya kupumzika akina Mohamed Salah, Sadio Mane na Virgil van Dijk.

Kwa kuwapa nafasi ya kupumzika, wataweza kurudi kwenye hali yao ya kawaida bila kuwa na presha kubwa.

Lakini tazama kilichotokea katika usajili wa Simba. Walivyokwenda sokoni wameshindwa kusajili vema. Mwisho wake wale waliosajiliwa dirisha kubwa wamekuja kuachwa dirisha dogo.

Baada ya mastaa waliosajiliwa kushindwa kuisaidia timu, Simba ikajikuta inarudi kwa mastaa wake waliochoka. Hawana namna.

Kinachotokea sasa katika mechi zao nyingi, mechi hii Simba watacheza vizuri na kuwashawishi watu kuwa wamerejea katika ubora wao, mechi ijayo Simba inarudi tena chini. 

Hiki ni kidonge cha uchungu kinachopaswa kumezwa na manazi wa Simba. Iwe wanataka au hawataki; timu yao imechoka, wala si mbaya. 

Tuhamie upande wa waamuzi. Nadhani waamuzi wetu wamechagua njia ya kushindana kukosea na si kupatia na kutupa kilicho bora katika viwanja vyetu. Wanakosea sana!

Katika pambano la  Simba na Tanzania Prisons kulikuwa na mfululizo wa makosa yao. Makosa ya kizembe waliyoyafanya yamewanufaisha Simba na kuwanyonga Tanzania Prisons. Hali hii mpaka lini?

Kibaya zaidi kinachouma manazi wa Simba wamelifurahia tukio hili. Tena wanawakumbushia manazi wa Yanga tukio la penalti ya mchongo kule Ilulu kwenye pambano la Namungo FC na Yanga. 

Kosa la timu ‘A’ linasawazishwaje na makosa ya timu ‘B’? Nadhani siku hizi tumechagua kuwa na mpira wa hivi. Twende nao tu. Tusiwe tunalalamika.