Miaka ya karibuni, dhana ya ujasiriamali imeenea kwa kasi kubwa miongoni mwa wanajamii. Kwa sasa kila kona tunasikia ujasiriamali –  kanisani, mitaani, vyuoni na katika mikutano ya kisiasa kunahubiriwa ujasiriamali. Hata hivyo, kuna kibwagizo kinachojirudia kila zinapotajwa changamoto za ujasiriamali – ukosefu wa mitaji!

Inafaa Watanzania wote kufahamu kuwa maisha ni magumu; na kwamba ugumu wa maisha haujaanza jana wala miaka ya karibuni, bali tangu kuwapo kwa dunia hii maisha ni magumu. Wengi huwa hawataki kuukubali ukweli huu.


Ndiyo maana utawasikia wakihuzunika, kunung’unika na kulalamika kana kwamba waliambiwa maisha ni rahisi. Wakati unapoukubali ukweli ya kuwa maisha ni magumu, ndiyo wakati ambao maisha hayawi magumu tena! Ndiyo! Kwa sababu ukijua maisha ni magumu lazima utaishi kwa nidhamu kubwa, na nidhamu ndiyo msingi namba moja wa kutatua matatizo yote katika maisha.


Ukiwa na nidhamu kidogo utatatua matatizo machache, na ukiwa na nidhamu nyingi utatatua matatizo mengi. Nidhamu inahusisha kufanya kazi kwa bidii, kuwapenda na kuwafikiria wengine, kuheshimu sheria za nchi na kila jema unalolijua.


Ukiona unalalamika kuwa maisha ni magumu, rejea katika fikra zako, huenda bado hakujafanyika mapinduzi! Ukiona unaukubali ukweli kuwa maisha ni magumu na wakati huo huo huna nidhamu, ama una nidhamu chache, basi ujue kuwa hujaukubali ukweli wote kuwa maisha ni magumu!


Ujasiriamali unawagusa watu wa kada na umri mbalimbali – vijana wazee na hata watoto. Kwa kuwa kundi la vijana [wasomi na wasio wasomi] ndiyo linaloongoza kwa kutegemewa kwa uzalishaji, nitazungumzia hilo.


Ujasiriamali kwa ujumla ni dhana ambayo ili kukubalika kikamilifu, kunahitajika mapinduzi makubwa ya fikra kwa vijana kuliko elimu ya kawaida. Fikra za kuwatazama wajasiriamali waliofanikiwa na kutoa visingizio kuhusu mafanikio yao, ni fikra zenye matege na ukilemaa na hizo kamwe haziwezi kutufanya tukafanikisha kujikwamua kiuchumi.


Vijana wasio na elimu wanalalamika kuwa hawana elimu ndiyo maana maisha yao ni magumu ama yanasumbua, nao vijana ambao wana elimu katika fani na viwango mbalimbali wanalalamika kuwa ajira hakuna. Unapogusia suala la ujasiriamali katika kundi hili la vijana wenye elimu, utakisikia kilio ambacho kimekuwa kama wimbo sasa nacho ni “ukosefu wa mitaji.” Kwa ufupi ni kuwa vijana wenye elimu wanalia kutokana na ugumu wa maisha na vile vile vijana wasio na elimu wanalia. Wasio na elimu wanawatamani wenye elimu, na wenye elimu wanaitamani mitaji.


Kutokana na hali hii, utagundua kuwa tatizo linalowakabili vijana wengi wa Tanzania katika kujikwamua kiuchumi si mitaji wala ukosefu wa elimu, bali ni la kifikra. Ili kijana aweze kufanikiwa kubuni na kuanzisha mradi, anatakiwa aamini kuwa kujiajiri kuna tija kubwa sawa na kuajiriwa. Kwa sababu ni mara chache mtu anaweza kuwa tajiri kwa kutegemea mshahara wake pekee!


Kwa bahati mbaya katika jamii kuna utamaduni uliojengeka katika jamii zetu wa kuamini sana kuajiriwa. Hata familia nyingi zinaposomesha watoto wao zinawasisitiza wasome kwa bidii ili wafaulu na kupata kazi zenye mishahara mikubwa. Utamaduni huu umefifisha hamasa na moyo wa kupenda kujiajiri miongoni mwa vijana wetu, hasa waliopo katika mifumo ya kielimu.


Hebu tumtafakari kijana anayesema kuwa amekosa mtaji ndiyo maana ni maskini. Ni dhahiri kuwa vijana wengi mara kwa mara huwa wanabahatika kupata shilingi elfu ishirini. Kijana akitumia ubunifu, kwa mfano, anaweza kununua kuku wawili wa kienyejji wa kufugwa, kila mmoja shilingi elfu saba.


Hawa wakifugwa kwa miezi minne wanaweza kutotoa vifaranga kumi. Baada ya mwaka mmoja kuku wanaweza kufikia sitini! Kuku sitini ukiwauza kwa shilingi elfu saba kila mmoja unakuwa na zaidi ya laki nne. Tayari huyu kijana anakuwa ameanza safari ya kujikwamua na umaskini.


Tunawahitaji wajasiriamali vijana kuandika vitabu vinavyoeleza namna walivyofanikiwa, ili kutia hamasa na kubadilisha fikra za vijana wengine wanaosuasua kujikita katika ujasiriamali kwa visingizio vya kukosa elimu na mitaji.


Ujasiriamali unahusisha kujenga fikra madhubuti za kujitegemea na kutegemewa. Kwanza ni kuwa akili ya mtu inapanuka na kuwaza zaidi na zaidi kutegemeana na mahitaji yaliyopo katika fikra. Ukiwaza kupata fedha kidogo ya kujikimu ubunifu wa akili yako utajikita katika upatikanaji wa fedha hiyo kidogo! Ukiwaza kuwa na fedha nyingi akili yako inapanuka kuwaza namna ya kupata fedha nyingi.


Ni vema vijana wote wafahamu kuwa “fedha ni mawazo.” Kama fedha ni mawazo basi kujikwamua kiuchumi ni mawazo pia. Kama ni suala la kuwaza, kwa nini asiye na elimu asiwaze? Kama ujasiriamali unaanza na mawazo, kwa nini wenye elimu walilie mitaji? Sikatai kuwa mitaji ni suala la msingi katika ujasiriamali, lakini ifahamike kuwa uthubutu wa kuanza na kujaribu wazo hata kwa sehemu ndogo ndiyo msingi wa mafanikio ya mjasiriamali yeyote.


Nchi ya Tanzania ina ajira na fursa nyingi za kiuchumi za kumtosha hata mtoto atakayezaliwa kesho! Sioni sababu ya mhitimu wa darasa la saba kukosa ajira, kwanini mhitimu wa kidato cha nne na sita wakose kitu cha kufanya chenye kuwakwamua kiuchumi katika nchi tajiri kama Tanzania? Kwa wale ambao ni wahitimu wa vyuo vya kati na vya elimu ya juu, sioni haja ya kuwaandikia kwa sababu inatosha sana kwao kutengeneza ajira kwa wengine.


Tatizo jingine linalowasibu vijana wengi wa Tanzania kiasi cha kushindwa kupoka (seizing) fursa za kijasiriamali na fikra potofu za kutaka kuanza na mafanikio. Kama ni kijana msomi anawaza kuanza na kampuni yenye mtaji wa mamilioni. Yatatoka wapi mamilioni bila kuanza na kidogo? Kwa wale ambao hawana elimu kubwa wengi wamevia kimawazo kwa kuota kuokota fedha ama kuokota elimu!


Kama ulikosa elimu hupaswi kulalamika wala kunung’unika kwa sababu huko ni kupoteza muda, bado unayo nafasi kubwa ya kufanikiwa. Fikra za kupata vya bure bila kuhangaika ndiyo zinazosababisha Watanzania wengi kujiingiza katika michezo mingi ya bahati nasibu kwa matarajio kuwa watatoka! Cha ajabu ni kuwa michezo hiyo, ama mingineyo inawapotezea fedha badala ya kuwasaidia, hapa yanahitajika mapinduzi ya kifikra.


Maisha bora na ya uhakika kwa vijana yanawezekana ikiwa kutafanyika mageuzi makubwa katika sekta binafsi, ujasiriamali. Ili ujasiriamali ufanikiwe na kufanywa na vijana kwa uhakika, lazima vijana wote wakubali kufanya mapinduzi ya fikra zao za kitegemezi.


Tukisema ujasiriamali hatumaanishi ujasiriamali wa kujikwamua wewe kijana peke yako, bali tunagusa pia katika utanuzi wa fikra za kuanzisha kampuni, huduma na bidhaa mbalimbali zenye ubunifu mpya kwa kuvitumia vipaji kikamilifu.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiujasiriamali!

[email protected], 0719 127 901