Namshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia uhai na wenye afya njema. Kila siku tukiamka ni siku mpya na yenye matumaini kwa misingi kwamba zipo fursa nyingi za kutuwezesha kuyamudu maisha yetu ya kila siku hasa katika Jiji la Dar es Salaam.

Wengi wetu tunajitahidi kuchakalika hapa na pale ili kuweza kuyamudu maisha. Ili kuweza kupata riziki zetu lazima tujiharakatishe. Hapa nimetumia neno “kujiharakatisha” kwa kumaanisha kuhangaika huku na huko kwa kufanya kazi ili mwishowe mhusika apate fedha za kumwezesha kuishi.

Hata maisha ya vijijini kwa kiasi kikubwa yanategemea sana kipato cha mkulima au mfugaji. Kuna mambo mengi yanayohitaji matumizi ya fedha bila kujali unaishi mjini au kijijini.

Hii inamaanisha kuwa maisha sasa yanategemea kipato na bila fedha hali inakuwa ngumu, kwa sababu hakuna cha bure, labda hewa tu ya oksijeni tunayoivuta kwa hisani ya Mwenyezi Mungu. Lakini zaidi ya hapo, lazima uwe na chochote mfukoni ili uweze kupata chakula na mahitaji mengine. Kwa msingi huo, lazima tufanye kazi kila uchao na kwa kuwa maisha si lelemama ni mahangaiko ya hapa na pale, mashambani au mijini, lazima tufanye kazi kwa bidii ili tuweze kupata chakula chetu cha kila siku.

Pamoja na kumwomba Mwenyezi Mungu atujalie tupate riziki au mikate yetu ya kila siku, lazima tufanye kazi. Imeandikwa “asiyefanya kazi na asile.” Hii inamaanisha kuwa wewe ni mtu mzima na mwenye afya njema, lakini hutaki kufanya kazi, basi binadamu wa aina hiyo huna haki ya kupewa chakula. Ni kweli wakati mwingine tunalalamika “maisha yamekuwa magumu sana”, lakini tujiulize, ni wapi imeelezwa kuwa maisha yatakuwa laini laini? “Kwa jasho lako utapata mkate wa kila siku.” Isitohe bila kufanya kazi kwa bidii hakuna maisha poa poa. Ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais anatuambia: “Hapa Kazi Tu” na si maneno maneno – chapa kazi, songa mbele, usikae kusubiri uteremshiwe maisha unayoyataka mwenyewe bila kujibidisha kweli kweli na kwa moyo.

Kwa kuitambua kanuni hiyo, wengi tunaamka mapema ili tufanye kazi na kujipatia riziki zetu. Kwa upande mwingine, tunaishukuru serikali yetu kwa kujenga miundombinu ya aina yake na hatimaye kutupatia huduma za mabasi ya mwendokasi kutoka Kimara hadi Kivukoni (Feri), Morocco na Kariakoo – Gerezani. Hali hiyo imeleta ahueni kwa misingi kuwa ukibahatika kupanda basi la mwendokasi unawahi kufika mjini au nyumbani.

Huduma za mabasi ya mwendokasi zinategemewa na watu wengi. Mimi ni mtumiaji wa huduma hii muhimu, lakini tangu kuanzishwa kwake kumekuwapo kero nyingi.

Mosi, ni uhaba wa mabasi wakati abiria ni wengi sana. Pili, mabasi kujaa sana watu kuliko uwezo wake na kusababisha adha kubwa wakati wa kupanda na kuteremka. Kiini cha changamoto hii ni abiria wengi kukaa muda mrefu vituoni, hivyo kulazimika kujazana kupita kiasi. Vilevile, hatuna utaratibu wa kujipanga kwa mistari ili mabasi yakipatikana watu waingie kulingana na walivyowasili kituoni (first comefirst ride).

Tatu, vituo vya kusubiria mabasi pamoja na kujengwa kwa gharama kubwa, vingi havina huduma za msingi: vyoo; viti (kukaa) na pia huduma za “vioski” vidogo vidogo kupata sharbati (juisi), chai, maji ya kunywa, magazeti na kadhalika.

Abiria anajikuta amesimama muda mrefu (zaidi ya nusu saa) akisubiri basi, lakini wapi – hayaonekani. Vituo kama Kimara Mwisho, Korogwe, Fire, City Council (Nyerere Square), Feri (Kivukoni) na Gerezani kuna watu wengi mno na msongamano mkubwa kweli kweli. Hivyo kuweza kupata basi ni shida kupindukia, hasa ukichukulia uhalisia kuwa abiria anakuwa amesimama muda mrefu halafu mabasi yakija yanakuwa yameshajaa.

Je, kero hii itakwisha lini? Kulikoni mwendokasi?  Je, ni ‘laana’ badala ya ‘baraka’? Menejimenti ya mwendokasi iwajibike ipasavyo na kuhakikisha huduma inaboreshwa hata kama mabasi hayatoshelezi. Nashauri yafuatayo kwa faida yetu sote:

(i)   Usimamizi uimarishwe maradufu ili kuhakikisha hayo machache yaliyopo yanatoa huduma ya kuridhisha.

(ii)  Vituo vyenye abiria wengi, kwa mfano, Kimara, Korogwe, Ubungo, Fire (Zimamoto), Msimbazi; Nyerere Square (City Council), Gerezani, Morocco na Kivukoni: utaratibu wa abiria kuweka mistari ili wapande kwa utulivu na amani, gari likijaa liondoke pasipo kusukumana au kukanyagana.

(iii)   Wasimamizi wahakikishe kuwa abiria wanaoteremka wanafanya hivyo kwanza kabla ya wanaopanda. Hali ilivyo, wanaoteremka wanasukumwa na wanaopanda kiasi kwamba inakuwa kero sana.

(iv)   Ni vizuri mabasi yatakayoagizwa yawe na milango ya kuteremkia sehemu ya mbele karibu na dereva na milango ya kuingilia iwe sehemu za kati na nyuma. Hii itarahisisha kushuka na kupanda. Abiria akijua atashuka, asogee mbele kuliko kujibana mwanzoni akisubiri kuteremka na wakati huo huo wengine wanahangaika kuingia.

(v)  Wasimamizi watambue na waelewe vizuri nyakati za abiria wengi (rush/pick hours) – asubuhi hadi saa nne kutoka Kimara na jioni kuanzia saa 10 kutoka Kivukoni, Gerezani na Morocco. Hivi ni vipindi ambavyo abiria huwa wengi kupita kiasi, hivyo inatakiwa menejimenti isimamie vizuri. Kwa maneno mengine, muda huo mabasi yawe mengi na yasimamiwe vizuri na yafanye kazi  ipasavyo.

(vi) Kampuni inayotoa huduma ni moja, endapo imelemewa ziruhusiwe kampuni nyingine ili ziagize mabasi. Kinachotakiwa ni kuboresha huduma, siyo tena kuona abiria wanateseka kwa kutokuwapo mabasi ya kutosha.

   Abiria ni wengi, hivyo mabasi pia yawe mengi hadi tuseme naam! Sasa tuko mwaka 2019 tukielekea uchumi wa viwanda na kipato cha kati bila mizengwe. Kinachotakiwa wenye uwezo wapewe viwango vya mabasi (specifications) kulingana na miundombinu iliyopo. Naamini watafanya kweli.

Mwisho, naipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu sehemu nyingi za Jiji la Dar es Salaam. Kunajengwa barabara za juu (interchange/flyovers) na lami inawekwa katika barabara nyingi za pembezoni katika manispaa zote.

Vilevile, ujenzi wa njia ya mwendokasi kwenda na kutoka Mbagala umeanza na baadaye tutashuhudia kuelekea Gongolamboto na Tegeta ikijengwa. Hiyo ni hatua nzuri na yenye kutia moyo. Kwa miaka mitano ijayo Dar es Salaam itakuwa Bandari Salama (the harbour of peace) kweli kweli na yenye mvuto wa aina yake Afrika Mashariki na Kati.

Wakati hayo yanaendelea, juhudi za makusudi zifanyike kuimarisha huduma za mabasi ya mwendokasi ya Kimara – Kivukoni, Gerezani na Morocco. Kwa kufanya hivyo tutaokoa muda, tutapunguza muda wa kufika kazini na kurejea nyumbani. Hakuna lisilowezekana chini ya jua, tuwajibike ipasavyo. Mwenyezi Mungu Ibariki Tanzania.