Mwathirika wa ajali huhitaji ahudumiwe haraka, tena kwa muda mfupi, huku mipango ikiwa inafanywa hadi atakapotokea daktari au atakapopelekwa zahanati ama hospitali kwa tiba inayostahili…

 

Majipu (boils) hutokea ndani ya ngozi inayozunguka kitundu cha kutolea jasho mwilini, penye shina la kinyweleo. Chukua painti moja ya maji ya moto (kiasi cha kujaza chupa) na utie ndani yake chumvi ya haluli (Epsom salts) kijiko kimoja kikubwa. Tumia maji hayo kuliosha jipu. Kamwe usilikamue jipu, kwani kwa kufanya hivyo usaha unaweza ukaingia ndani ya mishipa ya damu na kutia sumu ndani ya damu na kuleta madhara makubwa.

Wakati sehemu hiyo inapoanza yenyewe kutoa usaha, ifunge kwa kitambaa kilicho safi kuzuia usisambae katika sehemu nyingine. Liache jipu hilo limalizike lenyewe kutoka usaha, ambapo itabidi kidonda chake kisafishwe vyema na kufungwa dawa.

 

Jeraha la Jichoni

Ujeruhi kwenye jicho uchukuliwe kama ni janga linaloweza kusababisha upofu. Usilifikiche jicho wala kujaribu kutoa chochote kilichoingia ndani yake, isipokuwa kama kiko juu juu – kati ya mboni ya jicho na ngozi ya kope. Fanya hivyo kwa kutumia kitu kilichotolewa vijidudu vya maambukizo (sterile applicant), ama ncha ya kitambaa safi kilichotiwa kwenye boric solution. Vinginevyo, mpeleke mgonjwa haraka hospitali na umwachie daktari kazi hiyo, hata kama kilichozama jichoni ni kibanzi cha kuni.

Kichaa cha Mbwa

Kichaa cha mbwa (rabies) ni maradhi yanayoweza kuwapata watu na wanyama wanaonyonyesha (mammals). Ugonjwa huu hasa huja ukitokana na kuumwa na mbwa wenye kichaa. Paka na wanyama wengine wanaweza pia wakaambukiza ugonjwa. Mbwa wa mwitu (jackals) nao wamekuwa wasambazaji wakubwa wa ugonjwa huu katika nchi walioko kwa wingi, hasa kwa wanyama wengine.

Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation-WHO) lilikadiria mnamo miaka ya 1970 kwamba watu 5,000,000 huwa wanaumwa na mbwa na kupatwa na rabies kila mwaka duniani. Ingawa ugonjwa huu hauna dawa ya kuutibu lakini kuna dawa zinazotumiwa kuchanja kwa kinga. Asilimia 82 ya watu waliokuwa wanakufa kwa ugonjwa huu wakati huo walikuwa wakazi wa Afrika, ambapo ulikuwa umeenea katika nchi 90 duniani. 

Mbwa au paka akimuuma mtu lazima mnyama huyo apelekwe kwa mganga wa mifugo au polisi achunguzwe kama hana rabies. Jeraha la aliyeumwa na mnyama lisafishwe kwa maji na sabuni, kisha lifungwe kwa kitambaa kilichofuliwa ama kutiwa dawa za kuua viini vya maambukizo. Usichelewe kumpeleka kwa daktari. Hata kuumwa na meno ya binadamu lazima kuchukuliwe kuwa ni jambo la hatari.

 

Kugongwa na Nyoka

Nyoka anapomgonga mtu, sumu yake hupenya mwilini, na mara ngozi ya mwili mzima hupauka na kuwa ya kizambarau-nyeusi. Sumu ya nyoka husafiri haraka kwenye mkondo wa damu. Mgonjwa atasikia mwili umelegea na kukosa nguvu. Mapigo ya moyo huwa ya haraka na punde ataanza kutapika. 

Ili kumwokoa, haraka funga kwa nguvu sehemu ya juu, mbali kidogo na palipoingia meno ya nyoka. Unaweza ukafunga kwa kutumia tai, soksi ama upapi wa kitambaa kilichopasuliwa kutoka kwenye nguo. Chukua wembe ama kisu kikali kilichosafishwa na uchanje kwa nguvu chale kadhaa kuzunguka sehemu iliyojeruhiwa ili damu yenye sumu itoke. Nyonya kwa midomo yako na kuitema damu hiyo ambayo haitakudhuru, isipokuwa kama una kidonda kinywani.

Kati ya aina 650 za nyoka wanaojulikana kuwa wana sumu ni wa aina 200 tu ndiyo wenye sumu ya kuweza kumwua binadamu. Na kinachoua mara nyingi ni wasiwasi wa aliyegongwa wala si sumu yenyewe. Kwa kawaida nyoka humwogopa binadamu kuliko binadamu anavyomwogopa nyoka. Hivyo mara nyingi humgonga mtu akiwa katika harakati za kutaka kujihami. Baada ya huduma ya kwanza, lazima aliyegongwa na nyoka apelekwe hospitali.