Tunapozungumzia huduma za jamii huwa tunazungumzia masuala ya elimu, afya ,maji, umeme, huduma kwa wazee, huduma kwa walemavu na kadhalika.
Kwa ujumla huduma za jamii ni huduma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya watu wote. Watu wote maana yake ni wananchi.
Hapana shaka kuna malalamiko ya vyama vya upinzani dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu masuala mbalimbali yanayoweza kuchangia katika kuing’oa CCM.
Lakini ukitaka kusema kweli malalamiko ya wananchi dhidi ya CCM ndiyo yatakayo angusha CCM. Hao ndio walio wengi.
Chukua, kwa mfano, kama wapinzani watategemea kushinda kura za maoni kwa kupigania Serikali tatu wasahau.Hawatashinda.
Tunaendelea kukumbushana tena na tena kwamba wananchi wa kawaida (ambao ndio walio wengi ) hawaipendi Serikali. Kwao kila Serikali ni chombo cha ukandamizaji.
Kwa hiyo mwananchi wa kawaida hataki Serikali tatu. Serikali mbili alizoendelea kuwa nazo zinamtosha. Ni vyama vya upinzani vyenye maslahi na Serikali tatu katika mategemeo kwamba moja itakuwa yao.
Serikali inaweza ikajenga mijini barabara za kisasa kama nini. Mwananchi wa kijijini haoni kama kuna kitu kimefanywa na Serikali kama barabara za vijijini haziwezi kusafirisha mazao yake.
Ni huduma za jamii zinazotolewa kwa wananchi mijini na vijijini zitazokazoamua kushinda au kushindwa kwa CCM katika uchaguzi.
Tuanze na elimu. Hakuna asiyekubali kuwa hali ya elimu Tanzania ni mbaya sana. Na sababu yake ni moja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeshindwa kusimamia elimu Tanzania. Ni katika mazingira hayo Waziri wa Elimu nchini Tanzania ameendelea kuitwa ‘mzigo’ hata na chama tawala.
Kusema ukweli juu ya mambo ya nchi yako si kukosa uzalendo. Waliokosa uzalendo ni wale wasiosimamia elimu kwa ufanisi.
Tatizo kubwa Tanzania si kukosekana kwa watu wanaoona mambo yalivyo mabaya na kushauri kifanyike nini. Tatizo moja kubwa la Tanzania ni wale walio serikalini kufanya mambo kwa kiburi na ukaidi kana kwamba elimu ni chombo chao cha mfukoni kumbe elimu ni mali ya umma wote wa Tanzania.
Wananchi wameendelea kupiga kelele kwamba vitabu vinavyotumika mashuleni havifai. Walioko wizarani wanaendelea kuruhusu vitabu hivyo vibovu kuingia mashuleni kwa sababu tu wanapewa rushwa na wachapishaji wa vitabu.
Sasa wametosheka na utajiri walioupata kutokana na kuruhusu vitabu vibovu kuingia mashuleni. Kwa hiyo suala la uteuzi wa vitabu vya kuingia mashuleni wamehamishia Taasisi ya Elimu.
Kusema kweli miaka yote hii watoto wa maskini wa Tanzania wameendelea kupewa elimu mbovu kwa kukusudiwa kabisa. Vitabu vinavyotumika mashuleni vinashindana kwa ubovu badala ya kushindana kwa ubora.
Tunasema kwamba kama upinzani utafanikiwa kushika madaraka ya kuongoza nchi wahakikishe wanawakamata watendaji wakuu wote wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na mawaziri wao kwa kuendelea kuhujumu elimu ya watoto wa maskini ambao ndio walio wengi. Wamekuwa wasaliti wakubwa. Watu na akili zao timamu wanaruhusu vitabu vibovu viingie mashuleni eti kwa sababu wanalipwa na wachapishaji wa vitabu kwa kuvuruga elimu Tanzania.
Fedha ya vitabu vya rada imetumika vibaya. Kadhalika na fedha ya madawati ya rada. Tuna wizara inayosimamiwa wa watu waliokosa uzalendo na uadilifu.
Haihitaji kueleza wazazi wa Tanzania walivyochoka na fedha ya tuisheni wanayotakiwa kutoa kila siku. Inatisha kukutana hata na watoto wa chekechea wanao rudishwa nyumbani na walimu huku wakidai kuwa wamepigwa kwa sababu tu wazazi wao wamekosa fedha ya tuisheni.
Ni vyema Serikali ikaona ubaya wa tuisheni kwa wazazi na ikachukua hatua ya kurekebisha mambo.
Halafu kuna suala la lugha ya kufundisha Shule za Sekondari. Wadau wa elimu nchini kote wamepiga kelele kudai lugha ya kufundishia shule za sekondari iwe lugha ya Kiswahili
Lakini wakaidi tulio nao hawasikii kitu. Wameshikilia lugha ya kufundishia iendelee kuwa Kiingereza. Watu hawa wanashindwa kujua kuwa Kiingereza ni lugha au chombo cha kupashania habari. Kiingereza siyo elimu.
Ni ujinga ulioje mtu anayeshugulika na elimu kuamini kwamba Kiingereza ni elimu Kiswahili si elimu!
Nchi zilizoendelea (si sisi) zinafahamu kwamba mtu yeyote duniani anaeelewa vizuri na kumiliki maarifa akifundishwa kwa lugha anayoijua sana.
Kwa hiyo nchi hizo zilizoendelea zinafundisha watoto wao kwa lugha zao. Lugha za kigeni zinafundishwa kama somo tu. Waingereza hawafundishi watoto wao kwa kutu mia lugha ya Kigiriki au hata Kirumi kama ilivyofanya huko nyuma.
Leo Waingereza wanafundisha watoto wao kwa kutumia lugha ya Kiingereza Wafaransa kwa kutumia lugha ya Kifaransa, Wanyarwanda kwa kutumia Kinyarwanda, na Watanzania kwa kutumia Lugha ya Kiingereza!
Hebu turudi kwenye Tume ya Makwetta ya mwaka 1980. Hii ni tume iliyoteuliwa na Rais Julius Nyerere kuchunguza mwenendo wa elimu Tanzania. Iliongozwa na Jackson Makwetta, Waziri wa Elimu.
Kwa muda mrefu Serikali ya Mwalimu Nyerere ilikuwa imesikia manung’uniko ya wadau wa elimu kwamba elimu ilikuwa imeshuka kiasi cha kutisha.
Serikali ilikuwa sikivu. Haikuwa ya ukaidi. Ikaunda tume. Tume ikathibitisha kwamba elimu ilikuwa imeshuka. Ikapendekeza hatua za kuchukuliwa kurekebisha hali ya mambo.
Tume ya Makwetta, pamoja na mambo mengine, ilibaini ukweli kwamba mwanafunzi anaelewa vizuri zaidi akifundishwa kwa lugha anayoijua vizuri. Tena huchangia mawazo kirahisi.
Matokeo ya dosari ya kufundisha wanafunzi kwa lugha ya kigeni ambayo hawaielewi yako wazi kabisa .Watoto hawapati maarifa wanayoyahitaji kwa ukamilifu wake. Kwa kawaida watoto huyapata maarifa kwa kukariri tu kwa ajili ya mitihani. Wakitoka shule wanasahau mambo yote. Kikubwa zaidi vipaji vya watoto wetu wa Tanzania hupotea bila kutimika kwa sababu mwanafunzi anashindwa kujieleza.
Ukiuliza sababu kwa nini watu wachache wameshikilia wanafunzi wa shule za sekondari waendelee kufundishwa kwa lugha ya Kiingereza utaambiwa lengo ni kuhakikisha kwamba nchi jirani hazituachi nyuma. Hivi nani hajui kuwa Kenya na Uganda zimetuacha mbali sana kielimu? Wao wana Wizara za Elimu zinazoongozwa na wazalendo na waadilifu.
Lakini unaweza kuambiwa pia kwamba Kiingereza kinaendelea kutumika kama lugha ya kufundishia shule ya sekondari ili vijana wetu wapate ajira. Tuseme kweli.
Hivi mpaka leo ni vijana wangapi wa Tanzania wamepata ajira baada ya kumaliza masomo yao kwa sababu wamefundishwa katika lugha ya Kiingereza?
Wengi hawana kazi kwa sababu hata wakipewa usaili kwa lugha ya Kiingereza hufanya vibaya.
Mbona kuna Watanzania wamepata ajira China ingawa hawajui Kichina? Mbona tuna Wachina wengi Tanzania walipata ajira pamoja na ukweli kwamba hawajui lugha ya Kiswahili?
Cha kushangaza taifa la Tanzania lina lugha yake ya taifa, Kiswahili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alifanya juhudi kubwa katika kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili inakuwa lugha ya taifa.
Ilikuwa Januari 1960 Mwalimu Nyerere alipoongoza Chama cha TANU katika kupitisha azimio kwamba Kiswahili kingekuwa lugha ya taifa baada ya Tanganyika kupata uhuru.
Ikawa hivyo. Februari 13,1963 lugha ya Kiswahili ilianza kutumika kama lugha rasmi Bungeni pamoja na Kiingereza.
Kuna mataifa mengi ya Afrika ambayo lugha rasmi ni Kiingereza au Kifaransa Tanzania ina lugha yake rasmi, Kiswahili. Lakini leo watu wachache wanabeza lugha ya Kiswahili. Hawapendi Kiswahili kichukue nafasi yake.
Pengine unaweza kusamehe lugha ya Kiswahili kutotumika kama lugha ya kufundishia. Lakini huwezi kusamehe kuona kwamba hata somo la Civics (Uraia) linafundishwa kwa Kiingereza.
Ukweli ni kwamba somo la Uraia linahusu maisha ya kila siku ya Mtanzania. Na Mtanzania ana lugha yake ya taifa. Ni kweli Kiswahili hakifai hata kufundishia somo la Uraia? Kwa kweli tunashangaza. Tunafundisha uzalendo na maadili ya taifa kwa kutumia lugha ya kigeni ambayo hata mwalimu mwenyewe hajui vizuri?
Hii ni sababu ya kutosha maadili na uzalendo kuendelea kumomonyoka nchini Vijana wetu hawaelewi lugha inayotumika kuwafundishia uzalendo na maadili ya Tanzania. Wakati wa somo la Elimu ya Siasa ambalo lilifundishwa kwa lugha ya Kiswahili wanafunzi walilielewa vizuri na wakajengeka kizalendo.
Sasa tuangalie huduma za afya. Nazo pia zina matatizo makubwa kuanzia kwa daktari Katika nchi ambayo watu wake walio wengi ni maskini kama Tanzania kumdai mgonjwa ada ya shilingi elfu tano ili aweze kumwona daktari ni mzigo mkubwa sana kwake.
Ajabu ni kwamba ataandikiwa dawa ambazo hatazipata hospitali. Atatakiwa akatafute mahali pengine. Huko akizikuta atalazimika kuzinunua na hana fedha za kununulia dawa.
Kwa hiyo mgonjwa ataendelea kujiuguza bila kupata dawa. Atapona? Na hata kama atauguzwa hospitalini atalazwa sakafuni. Hatalala kitandani.
Kwa hiyo katika hali hiyo unakuta mtu wa kawaida anaichukia CCM na Serikali yake. Huduma za maji nazo pia haziridhishi. Wanawake vijijini wanatumia wakati wao mwingi kutafuta maji badala ya kuendelea na shughuli zao za kuzalisha mali. Nako mijini mambo ni hayo hayo. Wanawake wanatumia saa za kazi kwa kusaka maji mitoni na kando ya bahari.
Hakuna asiyeona kwamba Serikali inafanya kazi nyingi tena nzuri. Katikati ya kazi zote hizo inazofanya Serikali ni vyema ikaweka mstari wa mbele huduma za jamii mijini na vijijini.
Hata wakati wa Azimio la Arusha Serikali ya Mwalimu Nyerere ilitoa bure huduma za elimu, afya, na maji kutokana na umuhimu wake kwa wananchi.
Kwa hiyo hali ya kulegalega huduma za jamii mijini na vijijini inaweza kusababisha anguko la CCM na Serikali yake.