Watanzania tunaoishi vijijini tuna wajibu wa kutetea maslahi yetu. La sivyo ni rahisi sana kusahaulika.
Sababu kubwa ya mwito huu ni wingi wetu. Inakadiriwa kati ya asilimia 66 hadi 80 ya Watanzania wote tuko vijijini. Shida zetu zinaweza kuwa zinafanana na wa mjini: maji, nishati ya uhakika, ajira, chakula – lakini kwa wingi wetu tunapaswa kupewa kipaumbele.
Nimewahi kutofautiana na rafiki yangu tulipozungumzia mtazamo wa maisha. Nilimwambia ninapofika kwenye ukumbi hukaa viti vya nyuma na hubaki huko huko mpaka niitwe mbele. Mfano huu uko kwenye Biblia.
Yeye alinishangaa, akasema dunia ya leo ukijirudisha nyuma utabaki huko huko na hakuna mtu atakayekuita usogee mbele. Sana sana watatoka watu nyuma yako wakukanyage mabegani na kichwani ili wasonge mbele.
Alisisitiza kuwa unapata huduma au haki kwa kuipigania. Usitarajie sana kuulizwa kama una shida. Nashawishika kuanza kukubaliana naye.
Majuzi nilimpigia simu afisa mwandamizi wa taasisi muhimu yenye ofisi jijini Mwanza nikitaka anielekeze ilipo ofisi yao ili nipate maelekezo juu ya suala muhimu. Namba yake ya simu niliipata kwenye tovuti yao. Alinielekeza ilipo ofisi na jina la afisa mwenzake wa kuonana naye.
Nilipogundua kuwa ofisi ipo nje ya jiji na sikuwa na muda wa kufika huko kwa siku hiyo nilimuomba anipe namba ya simu ya afisa mwenzake ili niliyotaka kuyauliza ana kwa ana uso niyaulize kwa njia ya simu.
Hapo hatukuelewana. Ilikuwa kama vile nimeomba fomu ya kugombea urais wa Afrika, nafasi ambayo haipo.
Hakuhitaji kunieleza mengi kuelewa msimamo wake: ile namba ya simu ni taarifa nyeti kama ulivyo mshahara wa mtumishi wa umma (ingawa hata hilo sikubaliani nalo), au nywila yake ya kutolea pesa benki.
Aliniambia kuwa kama nahitaji huduma ni lazima nifike ofisini. Nilimwambia naishi kijijini na haitakuwa rahisi kurudi. Alinielekeza niende kwenye ofisi yao iliyopo mkoani Mara. Alinipunguzia tatizo, lakini kwa kuendeleza mfumo mbovu wa huduma.
Hoja zangu mbili: kwanza, nina haki ya kuhudumiwa kwenye simu sawa sawa na mtu aliyefika ofisini. Pili, kwa sababu simu nyingi za mezani hazifanyi kazi kwa kutolipwa ankara za matumizi, basi ile namba ya simu si tena mali binafsi, bali ni taarifa ya umma.
Simu za viganja zimetapakaa kote Tanzania na hakuna ulazima tena wa kumshurutisha raia ambaye yuko kijijini aende kwenye makao ya wilaya au mkoa kupata ufafanuzi wa suala ambalo linaweza kupatikana kwa urahisi kwa njia ya simu.
Nimeshuhudia mara nyingi ndani ya ofisi za umma simu ya mezani ikiita na kupuuzwa mpaka ikatike bila kupokewa. Na wala sitashangaa nimkute mtu yule yule ambaye namba yake ya simu sikupewa akiitumia saa za kazi kuangalia video za WhatsApp zikionyesha paka wanacheza rumba.
Kuna hitilafu ya baadhi ya watumishi kushindwa kubaini tatizo kwa kukosa uzoefu wa tatizo lenyewe. Wengi wetu tunaweza kufananishwa ha Malkia wa Ufaransa ambaye, kwenye kisa cha kutungwa, aliposikia masikini wanaandamana kwa sababu ya kukosekana mkate akauliza: “Kwanini hawali keki?”
Somo: ukikaa mbali sana na shida unasahau kama zipo. Ukikaa sana mjini ni hivyo hivyo. Unasahau kuwa unaposema ‘njoo ofisini’ kwa shida inayoweza kumalizwa kwa mazungumzo ya kwenye simu unaongeza tatizo lingine juu ya mengi mengine ambayo yapo kijijini.
Siku moja, miaka mingi iliyopita, nilimsikia rais mstaafu akisema: “Nawafahamu sana watu wangu. Ni rahisi sana kusema ‘hapana’ kuliko kutoa suluhisho.”
Alikuwa akizungumzia watumishi wa serikali na ugumu wao wa kupokea ushauri kutoka nje ya mfumo rasmi waliozoea.
Wakati mwingine kusema ‘hapana’ inakuwa njia ya kuepuka kuwajibika zaidi na suala ambalo likipewa jibu la ‘ndiyo’, basi litahitaji mchakato mrefu zaidi wa utekelezaji.
Wakati mwingine ‘hapana’ ni gia ya kuhamisha mazungumzo kutoka kwenye mfumo rasmi wa uwajibikaji na kuyaelekeza kwenye mfumo unaoruhusu kitu kidogo, rushwa.
Lakini yapo mazingira ambako ‘hapana’ hutolewa si kwa uzembe wala rushwa, ila ni ugonjwa wa baadhi ya watumishi wa umma wa kupenda kujiweka juu ya wale wanaowatumikia. Ni njia ya kumkumbusha mwenye shida kuwa afisa huyo ana uwezo wa kukataa jambo hata bila kuwapo sababu ya msingi.
‘Hapana’ ya aina hii inaweza kutolewa pia kwa kutoelewa au kutojali ni kwa jinsi gani jibu hilo litaongeza mzigo kwa mwenye shida.
Huu ni mwaka wa ishirini tangu karne ya 21 kuanza, lakini bado wapo watoa huduma ambao wanaishi kwa mtazamo wa karne ya 19. Simu, na hasa simu ya mtumishi wa umma, ni chombo cha mawasiliano; mawasiliano yale yale ambaye watu wawili watapeana wakiwa ana kwa ana.
Kama zipo sheria zinaainisha kuwa simu ya kiganjani ya mtumishi wa umma ni mali binafsi, basi upo ulazima wa kurekebisha sheria zilizopo. Halafu zifuate semina elekezi kwa watumishi wote kuwapiga msasa juu ya umuhimu wa kuhudumia Watanzania wote kwa usawa.
Barua pepe: [email protected]