Rais Magufuli: Watanzania tukatae kuitwa maskini
Ndugu zangu, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha leo hapa tukiwa wazima na wenye siha njema. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa kunialika kwenye hafla hii ya uzinduzi wa jengo la tatu la abiria ‘Terminal III’ katika Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Jengo hili ni la kisasa kuliko majengo yote ya abiria nchini. Kwa hakika tukio hili ni muhimu katika maendeleo ya usafiri wa anga hapa Tanzania. Vilevile nawashukuru wageni wetu mbalimbali mlioungana nasi kwenye tukio hili. Nimefurahi kuwaona mabalozi na waheshimiwa wabunge ambao ni chachu muhimu katika maendeleo ya ujenzi wa uwanja huu. Lakini nimeshukuru na kufurahi pia kuwaona wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam mkiwa mmejitokeza kwa wingi katika shughuli hii muhimu ya maendeleo ya taifa letu, asanteni sana.
Ndugu zangu, uwepo wa usafiri wa uhakika na wa haraka ni kichocheo kikubwa katika maendeleo ya nchi yoyote. Miundombinu ya usafiri na usafirishaji ni kama mishipa ya damu katika mwili wa binadamu. Kukosekana kwa miundombinu ya uhakika kunapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuongeza gharama za uzalishaji.
Na kwa kuzingatia hilo serikali inajenga barabara, inajenga reli, bandari, viwanja vya ndege na kadhalika ili kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kupitia njia zote tunazoweza kuzitumia nchini kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Ndugu zangu, licha ya kwamba kuna njia kuu nne za usafiri na usafirishaji, njia ya haraka na salama zaidi ni usafiri wa anga. Hii ndiyo sababu watu wengi zaidi duniani husafiri kwa njia ya anga. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga yaani Intenational Air Transport Association (IATA) jumla ya wasafiri milioni 12.5 duniani hutumia usafiri wa anga kila siku.
Lakini mbali na usafiri wa anga na uhakika, kuna manufaa makubwa zaidi kiuchumi katika sekta ya utalii. Ni ukweli usiopingika kwamba maendeleo ya utalii nchini hayawezi kutenganishwa na maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga – ni sekta zinazotegemeana sana.
Ninyi nyote ndugu zangu ni mashuhuda wa jitihada za Serikali kukuza sekta ya utalii ikiwemo kuanzisha hifadhi mpya ya taifa kama vile Burigi, Ibanda -Kyerwa, Rumanyika-Karagwe na si muda mrefu tutakuwa na Nyerere National Park itakayotokana na hifadhi ya Selous.
Vilevile idadi ya watalii imeongezeka hadi kufikia milioni 1.5 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na milioni 1.1 mwaka 2015. Kwa sehemu ya ongezeko hili inawezekana imechangiwa na kuimarika kwa usafiri wa anga. Hatuna budi kufanya jitihada zaidi.
Kwa sababu hiyo, leo nimefurahi sana ndugu zangu kuungana nanyi katika uzinduzi wa jengo hili ambalo litachangia sana kuboresha huduma za usafiri kwenye kiwanja hiki cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Kama tulivyoelezwa, chimbuko la tatu la kujenga jengo la abiria yaani “Terminal III” ni ongezeko kubwa la abiria ambapo kumekuwa na ongezeko la wastani 12.5 kwa mwaka. Nimearifiwa kuwa uwezo wa jengo la kwanza yaani “Terminal I” kama alivyozungumza Chief Executive ni abiria 500,000 kwa mwaka; na jengo la pili ni abiria 1,500,000; na hili tunalozindua leo litaweza kuhudumia abiria milioni 6. Hivyo kwa sasa kiwanja chetu hiki kina uwezo wa kuhudumia abiria milion 8 kwa mwaka. Ni wazi kwamba jengo hili litaongeza kasi ya kuwahudumia abiria wanaosafiri na ndege.
Aidha, nimehadithiwa kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia abiria 2,800 kwa saa nyakati wanapokuwepo abiria wengi (peak hours). Haya ni maendeleo makubwa. Hongereni sana Watanzania.
Ndugu zangu, tumesikia jengo hili limegharimu mabilioni ya fedha zaidi ya bilioni 720. Fedha hii imetolewa na Watanzania kwa asilimia 100. Asilimia 15 tumelipa fedha taslimu na asilimia 85 tumekopa. Ndugu zangu mkopo huu tumeupata kwa sababu Serikali yetu inaaminika na inakopesheka. Mkopo huu utarejeshwa kupitia kodi zetu.
Kwa sababu kazi hizi zitakuwa zimeanza na usafiri utaleta manufaa kwa Watanzania, napenda nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kumshukuru Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni mwanzilishi wa wazo hili. Mimi nimekuja kukamilisha tu.
Ndugu zangu, ninawapongeza sana wizara pamoja na TANROADS na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa usimamizi mzuri wa mradi huu. Chief Executive ameeleza kwamba wakati tunaingia madarakani mradi huu ulisimama na ukakosa pesa na mkandarasi akawa anatudai valuation ya fedha za kutokufanya kazi. Tunashukuru tuliweza kuzitafuta fedha kwa haraka na mradi kuufanya ufanyike na sasa umekamilika.
Nawapongeza TANROADS pamoja na wizara husika kwa sababu niseme tu kwa uwazi kwamba TAA walishindwa kuusimamia mradi huu na ndiyo maana tukaamua kwamba viwanja vya ndege vyote nchini sasa viwe vinasimamiwa na TANROADS kama ilivyokuwa zamani. Tunashukuru kazi mmeifanya kwa hiyo Mfugale [Patrick Mfugale –Mtendaji Mkuu wa TANROADS] na watu wako hongereni sana na wizara hongereni sana.
Nampongeza pia mkandarasi yaani Bam International kutoka Uholanzi pamoja na msimamizi wa mradi kutoka Misri wakishirikiana na Advanced Engineering Solution ya Tanzania kwa kweli wamefanya kazi nzuri. Hongereni sana.
Kwa kutambua umuhimu wa usafiri wa anga kama kichocheo cha ukuaji wa sekta mbalimbali hususani utalii. Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zinalolenga kuimarisha sekta ya usafiri wa anga. Hatua hizi ni pamoja na kufufua shirika letu la ndege na sio siri shirika letu lilikuwa katika hali mbaya mbaya mbaya sana. Sitaki kuelezea kwa jinsi hali ilivyokuwa.
Lakini ndugu zangu mradi huu umekamilika na gharama zake ni mabilioni mengi. Nataka nithibitishe kwamba kukamilika kwa mradi huu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya fedha za Serikali na nidhamu ya kuzitumia. Hii ndiyo siri ya mradi kukamilika.
Nimefurahi kuona pia mradi huu wenye thamani hizi zote bilioni 722 unakamilika na ndugu zangu Watanzania tunaweza kinachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya. Bila kuamua Watanzania tutaendelea kuwa wategemezi katika miradi ya maendeleo ya taifa letu.
Tumeamua na tumeendelea kuamua nchi yetu pamoja na miradi yake imeweza kufanikiwa na italeta faida kubwa kwa maendeleo ya Watanzania. Napenda nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Mheshimiwa Spika [Job Ndugai] pamoja na Bunge kwa kuwa wanaikubali hii miradi tunayoamua kwa kutumia fedha za ndani.
Mifano ambayo ni dhahiri ambayo imethibitisha uamuzi wetu na mafanikio yake ni kwamba tuliamua kujenga mradi wa reli (SGR) umegharimu trilioni 7.5. Tuliamua kujenga mradi wa umeme wa Rufiji fedha zinazotumika ni trilioni 6.5 tuliamua.
Tumeamua kujenga interchange Ubungo pale Dar es Salaam gharama yake ni bilioni 247 – Watanzania tumeamua. Tuliamua kujenga Daraja la Kigongo-Busisi ambalo litakuwa refu kuliko madaraja yote ndani ya Afrika Mashariki na Kati bilioni 699.2 zitatumika.
Tumeamua kujenga Daraja la Selander bilioni 270 zitatumika. Tumeamua kujenga barabara ya njia nane Kimara kuendelea kule mbele Kibamba bilioni 140 – fedha za ndani. Ni uamuzi mzuri.
Tumeamua kujenga barabara katika nchi nzima – zaidi ya kilometa 2,115 zinaendelea kujengwa. Nenda Mpanda mpaka Tabora, nenda Mbinga mpaka Mbambabay, zungumza mahali popote kuna mradi wa barabara, Daraja la Sibiti, daraja la wapi.
Barabara zote ambazo zinajengwa ni zaidi ya kilometa 2,115. Zinajengwa kwa lami. Fedha zinazotumika ni trilioni 5.37. Watanzania tuliamua. Tumeamua kujenga viwanja vya ndege 15 thamani yake ya kuvikarabati na kuvijenga hivyo viwanja ni zaidi ya trilioni 1.868.
Tuliamua kununua na kujenga rada nne Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro tumetumia bilioni 67.3 – ni uamuzi wetu. Tumeamua kujenga meli Ziwa Victoria na Ziwa Nyasa bilioni 172.3 zitatumika. Tuliamua kupanua Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara pamoja na Tanga trilioni 1.2 zinatumika.
Tumeamua kununua ndege 8 mpya kwa kutumia fedha za ndani tumetumia trilioni 1.03 na sasa tumeagiza ndege zingine tatu maana yake tutakuwa na ndege 11. Tumeamua kuhamia Dodoma ili kusudi Dar es Salaam uwe mji wa biashara.
Tumeamua miradi ya barabara hapa Dar es Salaam – kwa mfano sasa hivi kila eneo kuna barabara za lami zinajengwa – tunatumia bilioni 660 – ni sisi tulioamua. Tumeamua uwezeshaji wa vijana – vijana, akinamama na walemavu – mpaka leo zimeshatolewa kwa makundi haya matatu bilioni 54. Tumeamua kujenga miundombinu katika majiji na manispaa na halmashauri trilioni 1.35 zinatumika.
Katika afya kuna ujenzi wa vituo 352 vya afya, zahanati 30, hospitali 67, ukarabati wa hospitali za zamani 21 – bilioni 321.6 zimetumika. Tuliamua ununuzi wa vifaa vya hospitalini bilioni 64 zimetumika. Katika elimu ukarabati wa shule kongwe 62, ujenzi wa madarasa, maabara, nyumba za walimu na kadhalika – bilioni 308.1 zimetumika.
Mikopo ya wanafunzi tangu tuingie madarakani; elimu ya juu trilioni 1.62 zimetumika; elimu bure bilioni 945.987 zimetumika mpaka mwezi huu. Fedha za kununulia dawa, miradi ya umeme, miradi ya kilimo, uvuvi, mifugo, miradi ya mazingira, miradi ya madini, miradi ya maliasili na kadhalika yote imetumia mabilioni ya shilingi. Nisingependa kuitaja yote kwa sababu ya muda.
Kwa vile miradi hii yote tumeamua kuitekeleza kuna faida ya Watanzania basi na miradi hii ni kwa faida ya Watanzania wote. Tuamue pia kulipa kodi ili miradi hii iweze kukamilika mapema.
Ndugu zangu wana Dar es Salaam, leo tupo hapa kwa ajili ya ufunguzi wa mradi huu. Mradi huu wa Terminal III ambao umebeba jina la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni siku nyingine ambapo taifa letu linajenga historia ya pekee. Heshima ya mradi huu iwaendee Watanzania wote, ni sifa ya Watanzania wote.
Miradi hii yote inayotekelezwa ni sifa ya Watanzania wote. Ndugu zangu Watanzania tunaweza. Tuliambiwa mara nyingi kila siku kwamba Tanzania ni maskini nataka niwaambie hilo neno la kujiita maskini tulifute kabisa. Nchi yetu ni tajiri ila tulitaka kuaminishwa na watu wanaotaka kututumia sisi kama maskini.
Nimeitaja baadhi ya miradi niliyoitaja ni matrilioni ya fedha. Saa nyingine huwa nakaa najiuliza kweli hili linawezekana? Tumeweza. Maana yake kila palipo na nia Mungu yupo. Ndugu zangu Watanzania, Mungu yuko pamoja na sisi, mimi siwezi nikasimama mbele za watu nikasema haya ni kwa sababu yangu. Mimi ni dereva tu, lakini pia huwa ninajiuliza ikiwa siku moja Mungu akanichukua atakayekuja atakuja kuyamaliza kweli? Kwa sababu panahitaji moyo. Unafanya hivi huku unatukanwa, lakini inabidi ufanye tu kwa sababu lengo unafanya kwa ajili ya Watanzania. Inahitaji kujitoa sadaka ya kweli na ndiyo maana ninasema kwa dhati ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Ninawashukuru sana Watanzania wenzangu kwa kuendelea kuiniombea na kunipa moyo, lakini tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kulisimamia taifa hili. Nchi yetu imekuwa ya mfano.
Watu wanatuogopa sasa. Wapo wanaouliza mnapata wapi pesa? Ninasema pesa zilikuwa kwa mafisadi sasa zinaenda kwa Watanzania. Fedha zililiwa na mafisadi. Mafisadi wamefanya ya ajabu mno katika nchi yetu. Ni hovyo kweli na hili nataka niwaambie kwa dhati bila woga wowote.
Nchi hii ni tajiri ndugu zangu. Tuliomba fedha kutoka Ubungo kwenda Kibaha kilometa 20 tukawaomba wafadhili fulani sitaki niwataje. Wametuzungusha zaidi ya miaka miwili na masharti na ilikuwa barabara ya njia nne. Nikawaambia Wizara ya Ujenzi tunajenga njia nane na tunajenga kwa fedha zetu. Wametushangaa. Tukiamua tunaweza.
Tumeamua kuhamia Dodoma kwa Mheshimiwa Spika ambaye anatuambia sisi wa kanda ile ile tuwe tunakaa kule kule kwenye “Terminal I na Terminal II”. Amesahau kwamba yeye asubiri mpaka tutakapomaliza Uwanja wa Msalato.
Lakini ninavyozungumza hapa tumeshapata fedha dola zaidi ya milioni 22 kwa ajili ya kuanza kuujenga uwanja mkubwa sana wa Msalato, lakini tumeshapata zaidi ya bilioni 410 kwa kuanza kujenga barabara ya kilometa 110 duo courage way pale Dodoma.
Tumeshapata fedha ya kujenga barabara kutoka Bagamoyo mpaka Pangani ili watu – watani zangu Wazaramo wawe wanaamua kupitia Pangani au wapitie barabara nyingine. Tanzania tunaweza. Miradi ya maji ningeitaja hapa ni ya mabilioni na matrilioni ya fedha.
Arusha kuna mradi wa zaidi ya bilioni 520 wa maji, kuna miji zaidi ya 27 kuna trilioni 1.2 kutoka mkopo wa India kwa ajili ya miradi ya maji. Dar es Salaam hapa tumeanza kuboresha masuala ya maji.
Tumebana mianya, mianya ya ufisadi ndani ya watendaji ndiyo maana ndugu zangu nawaambia hii siyo miujiza ni kwa sababu Serikali iliyopo imeamua kusimamia haki kwa ajili ya wanyonge.
Napenda niwashukuru sana wanaonisaidia – mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tarafa, ma-DAS na Watanzania wote pamoja na wabunge na wananchi kwa hatua tunayoipitia. Hii ni hatua ya kujipongeza sisi wote Watanzania.
Napenda pia kuwashukuru sana viongozi wa dini wa madhehebu yote. Siku zote wamekuwa wakiliweka taifa la Tanzania mikononi mwa Mungu. Bila wao Tanzania haiwezi ikawepo. Niwaombe viongozi msichoke, endeleeni kuliombea taifa hili pamoja na watu wake, likaendelee kukaa kwa amani na likaendelee kuleta maendeleo ya Watanzania wote na hasa wanyonge – hasa wanyonge – hasa wanyonge.
Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania sisi wote tujipongeze. Tujipongeze kwa mafanikio haya na nitaomba tutakapopata nafasi ya kwenda kule wananchi wa kawaida wasiwazuie kuingia kule kuangalia hela zao mahali zilipofanyika kazi.
Ndugu zangu, tunayaweza na uwezo tunao kwa sababu tumeamua kuyatenda. Ndugu zangu, Mungu yuko pamoja na sisi na ataendelea kuwa na sisi katika kuhakikisha haya tunayaweza.
Jengo hili limejengwa kwa gharama kubwa sana kwa kutumia fedha za walipa kodi. Naomba ndugu zangu na hasa Wizara ya Ujenzi tulitunze jengo hili kwa sababu tatizo lingine kubwa la sisi Watanzania tunapopata miradi ikishamalizika kinachofuata ni uharibifu.
Niwaombe wizara ambao ndio wasimamizi wa jengo hili pamoja na Watanzania wote watakaokuwa wanalitumia hili jengo ambalo linatoa taswira ya Watanzania na jiji letu la Dar es Salaam, tulitunze tusiliharibu. Natoa wito kwa wana-Dar es Salaam na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa za ajira zitakazotokana na uwepo wa jengo hili.
Ninafahamu patakuwemo na maduka, patakuwemo na mabenki, patakuwemo na huduma zingine mbalimbali – niwaombe Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hakikisheni hayo yanapewa kwa wazawa. Hatuwezi tukajenga jengo kama hili halafu vitu vilivyomo mule kama maduka vimilikiwe na watu ambao si wazawa. Ni lazima wazawa waanze kufaidika na fedha zao zilizotumika kujenga jengo hili.
Suala lingine ambalo napenda nilisisitize hapa tunajua kuanzia juma lijalo tutakuwa na ugeni mzito kabisa katika nchi yetu. Wageni hawa wakiwemo marais 16 wa Jumuiya ya Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) watafika kwa ajili ya kuhudhuria mikutano mbalimbali ya jumuiya yetu ya SADC.
Ninaomba tuwapokee wageni wetu kwa shangwe na ukarimu mkubwa, lakini pia changamkieni fursa zitakazotokana na ugeni huu. Nasema changamkieni fursa zote, narudia tena fursa zote namaanisha maendeleo kwa wananchi.
Ndugu zangu, tuko hapa kuhudhuria uzinduzi wa jengo hili jipya, lakini pia nitumie fursa hii kuipongeza Wizara na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) chini ya Mtendaji Mkuu Ndyamukama kwa maandalizi mazuri ya hafla hii. Shughuli imefaa sana.
Lakini niwapongeze waimbaji wetu, bendi yetu ya TOT kwa kutuchangamsha sana. Ninawashukuru pia wageni wote waliohudhuria, lakini nawashukuru sana waandishi wa habari kwa kuendelea kuitangaza Tanzania. Hii ni Tanzania yetu, hakuna mtu mwingine atakayetutangazia mazuri ya Tanzania. Ni ninyi wawakilishi wetu waandishi wa habari.
Msichoke. Endeleeni kuitangaza Tanzania katika mema yanayopatikana, katika mazuri yanayotendeka Tanzania. Tanzania ni nchi nzuri, Tanzania tunaenda vizuri, ni miongoni mwa nchi tano katika Afrika ambapo uchumi wake unakua kwa asilimia 7; inflation ni 3.5.
Tanzania ni nzuri, miradi yote ninyi ndio wagharamiaji na ndio maana nimesisitiza ndugu zangu suala la uadilifu na ulipaji wa kodi. Sasa ninyi wana-Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla mmekuwa mashahidi wa fedha zenu zinatumika wapi. Tuhimizane ndugu zangu katika kulijenga taifa hili.
Ni matumaini yangu jengo hili litaonyesha taswira ya kweli ya Watanzania. Ni matumaini yangu watakaopewa nafasi ya kufanya kazi mle watafanyakazi kwa uadilifu mzuri kwa kuitangaza Tanzania.
Uwanja huu utumike kutangaza hata mbuga zetu za wanyama. Lile suala la Mheshimiwa Spika ambalo amelichomekea hapa mimi naona ni suala la msingi kwa hiyo ni jukumu kwa wizara chini ya uongozi wa Waziri Mkuu kukaa na kulijadili na kuangalia ni namna gani fukwe zetu kutoka Moa [Tanga] hadi Msimbati [Mtwara] – kilometa zaidi ya 1,422 zitatumikaje katika kuboresha uchumi na utalii.
Lakini ninachotaka kuwaeleza ndugu zangu Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano iko pamoja na wananchi. Tutajitahidi na tunaomba Mungu aendelee kutulinda – tujitahidi kutekeleza yale tuliyoyaahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili.